Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Kusini Unguja, Ramadhan Abdalla Ali amefariki dunia nyumbai kwake visiwani Zanzibar.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Jumanne Julai 27, 2021, Katibu wa Itikadi na Uenezi Zanzibar, Catherine Nao amesema kifo cha mzee huyo sio tu pigo ndani ya chama pekee bali Taifa kwa ujumla.
“Amefariki kweli taratibu za mazishi zinapangwa na familia lakini anatarajiwa kuzikwa kesho,” amesema Nao.
Nao amemwelezea mwenyekiti huyo kwamba alikuwa ni hazina, mbali na nafasi yake ya uenyekiti wa chama lakini alikuwa mzee anayefahamu na kuchanganua mambo mengi.
Kwa mujibu wa Nao, Mzee Ali alikuwa mwalimu wa kisiasa ambaye walimtumia katika madaraka ya itikadi kuwaelewesha vijana, wakina mama ilipotoka Afro Shiraz na kwa nini yalifanyika mapinduzi visiwani humo “kwahiyo alikuwa hazina kubwa sana.”