Mwezi na kiza, siyaamshe mapenzi.

Mwezi na kiza, siyaamshe mapenzi.

Dotto C. Rangimoto

JF-Expert Member
Joined
Nov 22, 2012
Posts
1,985
Reaction score
1,286

mume na mke..jpg

Alichonong'ona mwezi, Kiza imekisikia,
Usiwe kama mkizi,uketi kwa kutulia,
Niseme nawe kwa wazi, mwanangu hebu sikia,
Siwache hisia wazi, mapenzi kuyapupia.
Siyaamshe mapenzi, kama wataka jazua.

Kilichosemwa na jua, Nuru imekisikia,
Utampata tambua, nyonda aliye tulia,
Moyo utaanza jua, mwili utafuatia,
Mwili japo wasumbua, na kuomba vumilia.
Siyaamshe mapenzi,kama wataka jazua.

Kilichotegwa na wingu, mvua imekitegua,
Wewe kwake ni mkungu, yeye ni chungu tambua,
Haikufaa mizungu, uliza wenye kujua,
Mapenzi kizunguzungu, kwa waja wasojijua.
Siyaamshe mapenzi,kama wataka jazua.

Alichoficha bahari, upwa umekifichua,
Mwenyenzi na akustiri, naiomba hino dua,
Useme na yako siri, sivyo itakuumbua,
Waja wapate habari, mwana unavyougua.
Siyaamshe mapenzi, kama wataka jazua.

Miti yote husikia, ukulele wa upepo,
Miti yapenda tulia, msumbufu ni upepo,
Mwenza asipo tulia,utakesha kama popo,
Mito utailalia, muhibu wako hayupo.
Siyaamshe mapenzi, kama wataka jazua.

Kilichomliza kitanda, kuta nne wakijua,
Buibui kulitanda,kusiwe cha kuanua,
Pete kwenye chako chanda, juba utalifungua,
Mahaba kama ya kunda, ndio mapenzi tambua.
Siyaamshe mapenzi,kama wataka jazua.

Kilichompata ala, jambia linakijua,
Mkataji wa milala,Chatu anamtambua,
Mapenzi si tu hewala,yapo yenye kusumbua,
Mwenye kupenda jalala, apendwaye huchafua.
Siyaamshe mapenzi,kama wataka jazua.

Yalo ndani ya mtungi, mwenye kuyajua kata,
Ndani utaona mengi, matamu na kuchochota,
Waweza kwaa kigingi, na naseti ya kukata,
Yote siri ya mtungi, ujue weye ni kata.
Siyaamshe mapenzi, kama wataka jazua.

Haraka ya bwana Chura, ngozi ikambabuka,
Somo lataka subira, ndipo utaelimika,
Mwana sifanye papara, nisemacho hebu shika,
Usije pata hasara,na ukaja bahashika.
Siyaamshe mapenzi, kama wataka jazua.

Kila muomba chumvi, huombea chungu chake,
Aliyeuchonga mvi, alijua windo lake,
Mwenye kutandika jamvi, moyoni yuko na lake,
Sidharau mwenyemvi, jifunze kutoka kwake.
Siyaamshe mapenzi, kama wataka jazua.

Njano5.
0784845394.
 
Back
Top Bottom