Mwitikio wa Wananchi kupata huduma za uzazi wa mpango Halmashauri ya Mji wa Korogwe watajwa kuongezeka

Mwitikio wa Wananchi kupata huduma za uzazi wa mpango Halmashauri ya Mji wa Korogwe watajwa kuongezeka

informer 06

Member
Joined
May 11, 2024
Posts
66
Reaction score
49
Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Monica Nalinga amesema idadi ya watu wanaonufaika na huduma za Uzazi wa Mpango imeongezeka ikiwa ni matokeo ya ushirikiano baina ya Serikali na wadau ambao wamejitokeza kuunga mkono jitihada ambazo zimekuwa zikifanyika.
6907aa5a-508f-4f10-b47f-3b568818392b.jpeg

Akizungumzia huduma hizo Monica amesema kuwa katika kipindi ambacho Halmashauri ya Mji wa Korogwe imeshirikiana taasisi ya Marie Stopes Tanzania, idadi ya Watu waliopatiwa huduma za uzazi wa mpango imeongezeka kutoka takribani watu elfu 7 hadi elfu 12.

"Tunawashukuru wadau kwa kutuwezesha kutoa huduma za Uzazi wa Mpango, kabla ya kuwa na shirika la Marie Stopes Tanzania tulikuwa tunahudumia wateja lakini sio kwa kiwango kikubwa kama tulivyo sasa baada ya kuwapata. Wametusaidia tumeweza kufikia watu zaidi ya elfu 12 maana kipindi cha nyuma tulikuwa na watu takribani elfu 7."amesema Monica

Monica alieleza kuwa wadau hao kwa kushikiria na Serikali wamekuwa na utaratibu wa kuwajengea uwezo baadhi ya wahudumu wa afya ambao wanatoa huduma za Uzazi wa Mpango, ambapo amesema jambo hilo limeongeza tija katika utoaji wa huduma.

"Wadau hao wametusaidia kuweza kuwainua watoa huduma kwenye maeneo mbalimbali, kutokana na pale wanapokuja kwenye vituo vyetu wanatujengea uwezo jambo ambalo limechangia watoa huduma kuwa na uweledi mkubwa katika kuhudumia." amesema Monica

Pia amebainisha wazi kwamba katika vituo vya afya 18 vilivyopo Halmashauri ya Mji wa Korogwe tayari wadau hao wamefikia vituo 13 ambavyo wanashirikiana kutoa huduma za uzazi wa mpango, lakini ameendelea kutoa wito kwa wadau wengine kujitokeza ili kuongeza nguvu kwenye vituo vingine.

Aidha Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Msambiazi Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Imani Mgaya amesema mwitikio kwenye kituo hicho umekuwa ukiongezeka hasa baada ya uwepo wa ushirikiano na wadau.

Amesema kwa mwaka wa fedha 2024/2025 waliweka lengo la kutoa huduma za Uzazi wa Mpango kwa Watu elfu 1, ambapo anadai kwamba lengo hilo linaonekana kufanikiwa mapema kutokana na kuwafikia watu zaidi ya 700 katika kipindi cha miezi mitatu tokea mwaka wa fedha ulipoanza.

"Sasa kama unaangalia kama lengo nimepewa Watu 900 na bado kuna awamu tatu, maana yake tunatoa huduma nzuri. Ni kwamba tukifanya vizuri watu wanaenda kupeleka taarifa vijijini" amesema Mgaya September 22, 2024 wakati akitoa tathimini ya wa utolewaji wa huduma hizo

Aidha Mratibu wa Huduma za Uzazi wa Mpango Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Siboyi Mike Kidoma akizungumza October 23, 2024 amesema kwamba kwa muda wa wiki tatu kuanzia October 7, 2024 ambapo walikuwa wakitoa huduma za Uzazi wa Mpango kupitia 'Huduma Mkoba' kwa kushirikiana na Marie Stopes wamepata mwitikio mkubwa hususani wa kundi la vijana.
4caa65ad-7c49-49c4-a541-c8f6fd28406b.jpeg

"Tangu tumeanza mwitikio umekuwa ni mkubwa kwa sababu kwa siku tunao uwezo wa kuona watu zaidi ya 90, kwa hiyo tumekuwa tukipata watu wengi hasa kwa kipindi hiki tumepata mwitikio mkubwa wa vijana kwa sababu kwenye data zetu umri ambao upo kwa wingi ni wa vijana." amesema Siboyi

Baadhi ya wanufaika wanaeleza

Sima Mdepo Yohana ambaye ni Kijana (28) Mkazi wa Kijiji cha Msambiazi dereva Bajaji, amesema kuwa awali hakujua kama kuna umuhimu wa wanaume kupata elimu ya uzazi wa mpango, lakini anaseama baada ya kupata elimu hiyo ataongeza umakini na kuifikisha kwa vijana wengine.

"Awali mimi sikujua kama kuna umuhimu wa kupata hii elimu ya uzazi wa mpango lakini kwa nondo (uelewa) tuliopewa na wataalamu kwenye kituo chetu cha Msambiazi nimeweza kuelewa kwanini elimu hii inatakiwa kutolewa kwa sana. Mfano, mimi nina Watoto wawili kwa Wanawake tofauti lakini tuliwapata katika mazingira ambayo hakuna aliyepanga wala kutegemea, hili linanionesha wazi kwamba hata wale binti hawakuwa na hii elimu"amesema Yohana

Alisema hayo baada ya wataalamu kuwapatia vijana matumizi ya njia za Uzazi wa Mpango ikiwemo matumizi sahihi ya kondomu ambayo ni kati ya njia za Uzazi wa Mpango za muda mfupi.

Vilevile Mwanamke anayefahamika kwa jina la Mama Aziza (36) ambaye ni mnufaika wa huduma za uzazi wa mpango kutoka Halmashauri ya Mji wa Korogwe anadai kwamba kwa miaka mitano amekuwa akitumia njia za uzazi wa mpango huku akisema kuwa elimu aliyoipata kutoka kwa wataalamu ndiyo ilimuwezesha kufanya machaguo ya njia ipi atumie.

"Kwa sasa natumia njia ya kitanzi lakini zamani nilikuwa nikitumia sana sindano, njia hii nilianza kuitumia baada ya kupata elimu kuhusu matumizi ya njia mbalimbali, awali nilikuwa naisikia njia hii lakini nilikuwa nina taarifa tofauti. Lakini kwa sasa ndiyo naitumia na imenisadia kulea watoto wangu kwa kuwapishanisha kidogo"anaseama Mwanamke huyo

Aidha kwa niaba ya Marie Stopes Halmashauri ya Mji wa Korogwe ambaye ni Afisa Muuguzi, Emelda Mtega wakati akiongea na Waandishi wa habari kwenye Kituo cha Afya cha St. Raphael kilichopo Halmashauri ya Mji wa Korogwe mkoani Tanga amesema elimu ya Uzazi wa Mpango ambayo inaendelea kutolewa imekuwa chachu ya kuongeza mwitikio na kupunguza mitazamo hasi kuhusu njia mbalimbali.

"Kipindi cha nyuma ilikuwa ni kazi sana kumuelimisha Mtu mpaka akaelewa kulingana na imani potofu kwamba uzazi wa mpango unasababisha Watu wanapata Kansa, kwamba Mama akitumia uzazi wa mpango huwezi kufurahia nae katika suala zima la tendo la ndoa" amesema

Lakini mtaalamu huyo anasema kwa sasa kumekuwepo na mwitikio zaidi unaotokana na elimu pamoja na huduma ambazo zimekuwa zikitolewa bure katika vituo vyote vya afya ambayo vipo chini ya Serikali katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe.

Ikumbukwe kwa mujibu wa utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria ambao ulichapishwa rasmi mwaka 2022, unataja njia mbalimbali za Uzazi wa Mpango za kisasa ambazo ni kufunga kizazi kwa mwanamke na mwanamme , sindano, kitanzi (IUDs),vidonge, vipandikizi, kondomu ya kike na kondomu ya kiume, njia ya dharura, njia ya kalenda .
 
Wanawake wanatia sumu kwenye miili yao.. Nisiulizwe maswali mengi. Naishia hapo
 
Back
Top Bottom