Kibanga Ampiga Mkoloni
JF-Expert Member
- Aug 9, 2007
- 18,772
- 8,939
MUHTASARI
Kulingana na Kituo cha Utafiti wa Udongo cha Mlingano cha mkoani Tanga chini ya Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, Tanzania ina jumla ya Kanda Kuu saba (7) za Kiutafiti wa Kilimo. Ndani ya kanda hizo kuu saba, zipo Kanda ndogo 64 za kiikolojia zinazoonyesha aina ya mazao yanayoweza kuzalishwa kwa wakati muafaka. Kanda hizo Kuu ni Kanda ya Kaskazini yenye mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, na Manyara; Kanda ya Kati inayojumuisha mikoa ya Dodoma na Singida; Kanda ya Kusini mikoa ya Lindi na Mtwara; Kanda ya Magharibi mikoa ya Kigoma na Tabora; Kanda ya Mashariki mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Pwani na Tanga; Kanda ya Nyanda za Juu Kusini mikoa ya Iringa, Katavi, Mbeya, Njombe, Rukwa, Ruvuma na Songwe na Kanda ya Ziwa yenye mikoa ya Geita, Kagera, Mara, Mwanza, Shinyanga na Simiyu. Mwongozo huu umeandaliwa kwa kuzingatia hali ya udongo, mtawanyiko wa mvua na joto na pia umeonesha picha kwa baadhi ya mazao yanayolimwa katika Kanda husika.
Katika Mwongozo huu, mazao ya chakula ni yale ambayo huliwa moja kwa moja na/au baada ya kuyasindika kabla ya kuliwa. Mazao ya biashara ni yale ambayo hayatumiki kwa chakula kutokana na uhalisia wake na baadhi yake hutumika kama chakula baada ya kuyasindika; kwa mfano Korosho, Miwa, Kahawa na Chai. Hata hivyo, kutokana na uwingi wa uzalishaji, mazao ya chakula pia yanaweza kutumika kama ya biashara hususan pale ambapo yakizalishwa zaidi ya mahitaji hususan katika ngazi ya kaya na au yamezalishwa mahususi kwa ajili ya kuuzwa (commercial production).
Kutokana na maelezo hayo, Mazao Makuu ya Chakula yanayozalishwa nchini ni ya jamii ya wanga hususan nafaka, mizizi na jamii ya migomba. Mazao hayo ni mahindi, muhogo, mpunga na mtama. Mazao mengine ni ndizi, viazi vitamu na mviringo, ngano, ulezi na uwele; kwa ujumla wake mazao hayo hupelekea taifa kujitosheleza kwa chakula. Mazao Makuu ya asili ya biashara ni korosho, miwa kwa ajili ya sukari, pamba, mkonge, tumbaku, pareto, kahawa na chai. Mazao mengine yanayozalishwa ni ya jamii ya mafuta hususan alizeti, ufuta, mawese, karanga na mbegu za pamba. Kundi la mazao mbalimbali ya bustani ni pamoja na matunda, mbogamboga, maua na vikolezo (spices). Kundi jingine ni la mazao jamii ya mikunde yenye uwingi wa protini na hurutubisha udongo kutokana na uwezo wake wa kutengeneza virutubisho vya nitrojeni kutoka hewani (nitrogen fixation).
Pamoja na Tanzania kuwa na Kanda Kuu saba (7) za Utafiti wa Kilimo na 64 ndogondogo za Kiikolojia, kwa muda mrefu tija katika uzalishaji wa mazao hayo imekuwa ndogo kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa mazao kutozingatia kanda hizo za kilimo za kiikolojia. Aidha, gharama za uzalishaji wa mazao nje ya ikolojia yake ni kubwa zaidi hususan wakati miundombinu ya umwagiliaji maji inapohitajika.
Mwongozo huu unakwenda sambamba na azma ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa kuwa uzalishaji kulingana na kanda za kiekolojia utaongeza tija na hivyo kutoa malighafi ya mazao kwa viwanda vinavyojengwa nchini. Uwepo wa viwanda hivyo utaongeza kasi ya uwekezaji katika kilimo kwa kutumia teknolojia za kisasa na kwa gharama nafuu endapo zao litalimwa kwenye kanda yake ya asili ya kiikolojia. Mwongozo umeainisha ni wapi na ni zao gani linastahili kuzalishwa. Kwa mfano, maeneo yanayopata mvua chache yatatumika kwa kuzalisha mazao yanayostahimili ukame kama vile Mtama, Muhogo, Viazi vitamu na mazao ya jamii ya mikunde (mbaazi na kunde). Kwa upande mwingine, fursa za kuzalisha mazao yenye soko hazijatumika ipasavyo kutokana na wakulima kutokujua fursa ya kuzalisha aina ya mazao katika maeneo yao. Mwongozo huu utawezesha kuratibu shughuli za kilimo nchini kulingana na mtawanyiko wa vituo vya utafiti, viwanda na masoko kwa kuzingatia kanda za uzalishaji.
Ili mwongozo utumike kikamilifu, pia kalenda ya kilimo imeandaliwa hususan kwa kuzingatia mwenendo wa mvua katika mikoa mbalimbali nchini. Hata hivyo, kwa kuwa kumekuwepo na mabadiliko ya tabianchi kilimo kinachohimili mabadiliko hayo kinahamasishwa, pia wadau katika sekta ya kilimo wanashauriwa kuwasiliana na watafiti na wataalamu wa kilimo walioko katika maeneo yao. Serikali itaendelea kuhimiza matumizi ya huduma za ugani kwa kuzingatia mwongozo huu ili kutoa ushauri, mafunzo na maelekezo kuhusu kanuni za kilimo bora kwa mazao yatakayozalishwa katika ikolojia yake.
Mamlaka za Mikoa na Wilaya zinashauriwa kutunga sheria ndogondogo katika maeneo yao na kubuni njia bora za kutumia mwongozo huu. Kwa upande wake, Wizara itaendelea kutoa ufafanuzi kila inapohitajika ili kuhakikisha lengo la mwongozo huu linafikiwa ili kuleta mapinduzi halisi katika kilimo hapa nchini kwa manufaa ya mtu mmoja mmoja, jamii na taifa kwa ujumla. Mwongozo huu pia unapatikana katika wavuti ya Wizara www.kilimo.go.tz. Mikoa na Wilaya zinaelekezwa kuzalisha mazao ya biashara na ya chakula kulingana na hali ya kiekolojia ya maeneo yao ili kutekeleza kikamilifu awamu ya pili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP II).