
Baadhi ya wanajeshi wa Urusi wanakataa kurejea kupigana nchini Ukraine kwa sababu ya uzoefu walioupata wakiwa mstari wa mbele mwanzoni mwa uvamizi huo. Hii ni kwa mujibu wa wanasheria na wanaharakati wa haki za binadamu wa Urusi. BBC imezungumza na mmoja wa askari mmoja hao.
"Sitaki kurejea [Ukraine] kuua na kuuawa," anasema Sergey - sio jina lake halisi - ambaye alitumia wiki tano katika mapigano nchini Ukraine mapema mwaka huu.
Sasa yuko nyumbani nchini Urusi, baada ya kuchukua ushauri wa kisheria ili asirudishwe kwenye uwanja wa mapambano. Sergey ni mmoja tu kati ya mamia ya askari wa Urusi wanaofahamika kuwa wamekuwa wakitafuta ushauri kama huo.
Sergey anasema ameumizwa na alichokipitia nchini Ukraine.
"Nilifikiri kwamba sisi ni jeshi la Kirusi, jeshi bora na lenye nguvu zaidi duniani," kijana huyo alisema kwa uchungu. Badala yake walitarajiwa kuingia kwenye vita bila hata vifaa vya msingi, kama vile vifaa vya kuona usiku, anasema.
"Tulikuwa kama paka kipofu. Ninashtushwa na jeshi letu. Isingegharimu sana kutupatia vifaa. Kwa nini haikufanyika?"
Sergey alijiunga na jeshi kama mwanajeshi - vijana wengi wa kiume wa Kirusi wenye umri kati ya miaka 18-27 lazima watumikie mwaka mmoja wa huduma ya kijeshi ya lazima. Lakini, baada ya miezi michache, alifanya uamuzi wa kusaini mkataba wa kitaaluma wa miaka miwili ambao pia ungempa mshahara.
Mnamo Januari, Sergey alipelekwa karibu na mpaka na Ukraine kwa kile alichoambiwa itakuwa mazoezi ya kijeshi. Mwezi mmoja baadaye - 24 Februari, siku ambayo Urusi ilizindua uvamizi wake - aliambiwa avuke mpaka. Mara moja kikosi alichokuwepo kilijikuta kikishambuliwa.
Waliposimama jioni kwenye shamba lililotelekezwa, kamanda wao alisema: "huu sio mzaha."
Sergey anasema alishtuka sana.
"Mawazo yangu ya kwanza yalikuwa 'Je, hili linanitokea kweli?'
Walikuwa wakishambuliwa kwa makombora kila mara, anasema, wakati wakisonga kuingia Ukraine na hata wakati wa kupumzika usiku kucha. Katika kikosi chake cha watu 50, 10 waliuawa na wengine 10 walijeruhiwa. Karibu wenzake wote walikuwa na umri wa chini ya miaka 25.
Alisikia kuhusu uwepo wa baadhi ya askari wa Kirusi wasio na ujuzi kwamba "hawakujua jinsi ya kupiga risasi".
Anasema msafara wake - unaosafiri kaskazini mwa Ukrainia - ulivunjika baada ya siku nne pekee wakati daraja walilokuwa wakikaribia kulivuka lilipolipuka, na kuua askari wengine wa Urusi waliokuwa mbele yao.
Katika tukio lingine, Sergey anasema alilazimika kuwapita wenzake waliokuwa wamekwama ndani ya gari lililokuwa likiungua mbele yake.
"Ililipuliwa kutokana na kurushiwa guruneti au kitu kama hicho. Ilishika moto na kulikuwa na askari [wa Urusi] ndani. Tuliendesha gari kuizunguka na kuendelea na safari, tukifyatua risasi huku tukienda. Sikutazama nyuma."
Kikosi chake kiliendelea kupitia maeneo ya maporini ya Ukraine, lakini kulikuwa na ukosefu wa mkakati wazi, anasema. Vikosi vyenye silaha za nguvu vilishindwa kufika na askari walikuwa na vifaa duni kuweza kuteka jiji kubwa.
"Tulienda bila helikopta - tulitembea tu, kana kwamba tunaelekea kwenye gwaride."
Anaamini kwamba makamanda wake walikuwa wamepanga kuteka ngome na miji muhimu haraka sana - na alikuwa amehesabu kwamba Waukraine wangejisalimisha tu.
"Tulikimbilia mbele kwa muda mfupi bila uchunguzi. Hatukuacha mtu yeyote nyuma, hivyo ikiwa mtu aliamua kuingia kwa nyuma na kutupiga hakuna ulinzi.
"Nadhani [wengi wa] vijana wetu walikufa kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya hili. Kama tungesonga hatua kwa hatua, kama tungeangalia barabara za migodi hasara nyingi zingeweza kuepukika."
Malalamiko ya Sergey kuhusu ukosefu wa vifaa pia yameibuka katika mazungumzo ya simu yanayodaiwa kuwa kati ya wanajeshi wa Urusi na familia zao, yaliyonaswa na kuwekwa mtandaoni na idara za usalama za Ukraine.
Mwanzoni mwa Aprili, Sergey alirudishwa kwenye mpaka kwenye kambi ya upande wa Urusi. Wanajeshi walikuwa wameondolewa kaskazini mwa Ukraine na walionekana kujipanga tena kwa ajili ya kushambulia eneo la mashariki. Baadaye mwezi huo alipokea amri ya kurudi Ukraine - lakini akamwambia Kamanda wake kwamba hakuwa tayari kwenda.