Nadhari Zinazoumba Uhalifu

Nadhari Zinazoumba Uhalifu

Amavubi

JF-Expert Member
Joined
Dec 9, 2010
Posts
30,156
Reaction score
13,258
Kuna dhana mbalimbali za kuhusiana na sababu zinazosababisha uhalifu wa jinai na kuibuka kwa makundi ya kihalifu na ugaidi. Baadhi ya dhana hizo zinajadiliwa kama ifuatavyo:-

  1. Sababu za Kisaikolojia / Dhana ya Kisaikolojia yaani Psychoanalitic Theory kama ilivyoelezwa na Sigmund Freud (Kuzaliwa 1856 , Kufariki 1939)
Sigmund Freud (1856 -1939) anaeleza kwamba makuzi ya mtu ya kisaikolojia yanaweza kumfanya awe mhalifu au asiwe mhalifu.

sigmund-freud.jpg

Sigmund Freud

Hii inatokana hasa na makuzi ya mtu ya utotoni, Mtu akiwa anakuwa huku akijengewa chuki ya kitu au watu fulani, basi hukua na hali hiyo hiyo na huweza baadae kuwa mhalifu na kujiingiza katika makosa ya jinai. Angalia mifano ifuatayo:-

(i) Adolf Hitler, Dikteta na mtawala wa zamani wa Ujerumani (Reich), alikuwa na chuki tangu utotoni dhidi ya Wayahudi na alipoitawala Ujerumani aliwaangamiza Wayahudi kwa kuwaua kwa wingi mno katika mauaji ya Wayahudi (Holocaust).

Adolf-Hitler-300x200.jpg

Adolf Hitler

Mauaji haya yalikuwa ni mwendelezo wa saikolojia aliyokuwa nayo Hitler tangu utotoni ya kuwa Wayahudi ni watu wabaya kwake na hawastahili kuishi. Pia kitabu cha Hitler cha Main Kampf yaani My Struggle au Harakati Zangu, ambacho kilikuwa kama ilani ya chama cha Nazi cha Hitler, kilikuwa na mawazo yake mengi yaliyoathiriwa na mfumo wa maisha aliyokulia

(ii) Watoto wa Wafuasi wa makundi kama vile Al Aqsa Martyrs, Hamas na Hizbollah, huaminishwa kwamba raia yeyote wa Israel ni adui yao na anastahili kuuawa na wao kwa namna yoyote ile. Hali hii hujengeka kwa watoto hawa mpaka ukubwani na hufikia hatua ya kujitoa mhanga kwa kujilipua kwa mabomu ili kuua raia yeyote wa Israel huku wakijitambulisha kama wapigania uhuru wa Palestina na Israel wakiwatambua kama magaidi.

  1. Sababu za Kibaiolojia / Dhana ya Kibaiolojia yaani Biological Theory kama inavyoelezwa na Cesare Lombroso:-
Mwaka 1871 mwanasayansi wa Italia aliyejulikana kama Cesare Lombroso alikutana na mhalifu maarufu aliyeitwa Giuseppe Villella ambapo Lombroso baadae aligundua mhalifu huyo kuwa na dosari kadhaa za kuzaliwa nazo katika viungo vya mwili wake.

cesare-lombroso.jpg

Cesare Lombroso

Lombroso aliyekuwa daktari wa jeshi la Italia, alifanya baadae utafiti wake kwa wanajeshi wa Italia, wafungwa na wahalifu na kuibuka na dhana kwamba watu wanazaliwa wakiwa wahalifu, na watu wenye dosari katika viungo vya miili yao, huwa wahalifu tofauti na watu wasio na dosari katika viungo vya miili yao.

  1. Dhana ya Mapepo / Demonological Theory
Dhana hii imejikita katika masuala ya kidini. Baadhi ya dini huamini kwamba wahalifu huwa wanatenda uhalifu kwa kusukumwa na roho ya mapepo yaani demons ambayo huwafanya watende uhalifu. Imani iliyopo ni kwamba ili mhalifu aache uhalifu, inabidi atolewe pepo hilo ambalo huwa ni pepo la tabia fulani ya kihalifu, kama vile wizi (pepo la wizi).

BIBLIA TAKATIFU

Biblia Takatifu katika kitabu cha Matendo ya Mitume Sura ya 5, Mstari wa 15 mpaka wa 16, imeandikwa kwamba:-

(i) Mstari wa 15 unaeleza :

“hata ikawa katika njia kuu hutoa nje wagonjwa, na kuwaweka juu ya majamvi na magodoro, ili Petro akija, ngawa kivuli chake kimwangukie mmojawapo wao.’’

(ii) Mstari wa 16 unaeleza:

“Nayo makutano ya watu wa miji iliyoko kandokando ya Yerusalemu wakakutanika, wakileta wagonjwa, nao walioudhiwa na pepo wachafu; nao wote wakaponywa’’.

Tafsiri yake:-

Nukuu tajwa ya Biblia Takatifu inaonesha uwepo wa watu waliokuwa wakisumbuliwa na mapepo wachafu (ambao waliwapelekea watu hao kufanya vitendo viovu yakiwemo makosa ya uhalifu wa jinai.

Pia Biblia Takatifu inaeleza tena katika Kitabu cha Luka Mtakatifu, Sura ya 9, Mstari wa Kwanza, kwamba :-

“Akawaita wale Thenashara, akawapa uwezo na mamlaka juu ya pepo wote na kuponya maradhi”

Tafsiri yake:-

Nukuu tajwa ya Biblia Takatifu inaonesha uwepo wa mapepo ( ambayo yana uwezo wa kumfanya mtu atende vitendo vya kihalifu), na mapepo hayo yanaweza kudhibitiwa na mtu mwenye mamlaka ya kuyadhibiti ( kupitia imani ya mtu huyo ambayo hutokana na ucha Mungu wa mtu huyo).

KURANI TUKUFU

Kitabu cha Kurani Tukufu katika Suratul _ Jinni, Aya ya 6, kinaeleza : –

Na hakika walikuwako wanaume katika watu waliokuwa wakitafuta kujikinga kwa wanaume wa kijini; kwa hivyo wakawazidisha madhambi’

Tafsiri yake: Aya hii inaelezea juu ya uwepo wa majini (mapepo) ambayo baadhi ya hayo majini yaliwafanya wanaume waliokuwa nayo watende madhambi zaidi (pamoja na madhambi ya jinai).

Pia Kitabu cha Kurani Tukufu katika Suratul _ Jinni, Aya ya 5, kinaeleza tena : –

Nasi tulidhani kuwa watu na majini hawamzulii uwongo Mwenyezi Mungu

Tafsiri yake: Aya hii inathibitisha na kutambua uwepo wa majini (mapepo) ambayo nayo pamoja na watu, wamekuwa wakitenda madhambi mbalimbali kama vile kumzulia uongo (neno ambalo katika aya tajwa limeandikwa ‘uwongo’) Mwenyezi Mungu.

Imani iliyopo ni kwamba pepo la kutenda uhalifu wa aina yoyote, litatolewa kupitia maombi ya mtu mwenye imani na uwezo wa kutoa mapepo hayo na pindi pepo hilo likitoka, basi mhalifu ataacha tabia ovu.

4. Dhana ya Udhibiti/Control Theory

Dhana hii imejikita katika kueleza kwamba ukosefu wa udhibiti husababisha watu kujiingiza katika vitendo vya uhalifu. Suala lililopo ni kwamba watu wa karibu wa mhalifu kama vile wazazi, walimu au wafanyakazi wenzake wa mhalifu walishindwa kudhibiti aidha kwa kukemea au kuzuia mhalifu kujihusisha na vitendo vya kihalifu. Kwa mfano, walimu na wazazi wanapaswa kudhibiti vitendo vya kihalifu vya mtoto tangu akiwa mdogo. Pia wafanyakazi, wanapaswa kudhibiti vitendo vya kihalifu vya wafanyakazi ambao ni wakiukaji wa maadili kwa kutenda jinai kama vile ufisadi, wizi na vitendo vingine vya kihalifu.

Pia wahalifu huelezwa kwamba hushindwa kujidhibiti wao wenyewe ili kuepuka kujiingiza katika vitendo vya kihalifu kama vile wizi. Wapo ambao hutawaliwa na tamaa kama vile za kumiliki mali na vitu vya anasa, na tamaa hizo huwapelekea kujihusisha na vitendo vya kihalifu kama vile wizi.

  1. Dhana ya Migogoro au Migongano /Conflict Theory
Dhana hii humaanisha kwamba vitendo vya kihalifu hutokana na migongano au migogoro katika jamii. Migogoro inayoweza kusababisha maovu katika jamii inaweza kuwa ya kisiasa, kiuchumi au kijamii. Mgogoro wa kisiasa nchini Burundi chini ya Rais Pierre Nkurunzinza, unaosababisha machafuko na vitendo vya kihalifu kushamiri nchini humo, unatokana na kugombea madaraka katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Jamii ya Wakurdi waliopo Uturuki wana mgogoro mkubwa na serikali ya Uturuki na sababu kubwa ikiwa ni ubaguzi wanaodai kufanyiwa Wakurdi na Uturuki katika masuala ya kiuchumi na haki za kijamii, hali hii imesababisha machafuko na uvunjifu wa Amani nchini Uturuki.

kurd.jpg

Wapiganaji wa Kikurdi

Mwanafalsafa Karl Marx aliyekuwa akiamini katika sera za mrengo wa Ujamaa, aliamini mfumo wa uchumi wa ubepari huwa na matabaka ya wenye nacho na wasio nacho.

KARL-MARX.jpg

Karl Marx

Matabaka hayo kiuhalisia huwa hasimu na mabepari hutaka kuendelea kuwakandamiza wanyonge ambao nao hutaka kuwa wenye nacho, hali hii huibua migongano katika jamii ambayo hupelekea kuibuka kwa maovu ya aina mbalimbali katika jamii.

  1. Kujifunza/Kuiga Kupitia Jamii yaani Social Learning Theory
Dhana hii inamaanisha kwamba watu hujifunza uhalifu kupitia jamii inayowazunguka. Wapo watu waliojifunza uhalifu kutokana na kujifunza kupitia marafiki zao wa karibu ambao walikuwa wahalifu.

  1. Kupachikwa uhalifu yaani Labelling Theory
Wapo watu waliowahi kukamatwa mara kwa mara na vyombo vya dola na kutiwa hatiani kwa makosa mbalimbali na kuachiliwa au kumaliza kutumikia vifungo au hata kutotiwa hatiani. Watu hawa hujikuta baadhi yao wakibaguliwa na jamii katika masuala mbalimbali na pindi wakijiingiza kufanya shughuli halali ya kuwaingizia kipato halali, hutengwa au hujikuta wakihisiwa au kutuhumiwa na jamii kutofanya shughuli halali. Hali hii ya kutengwa na kubaguliwa huku wakionekana ni wahalifu, huwafanya baadhi yao wajiingize katika vitendo vya kihalifu.

  1. Dhana ya Kimazingira yaani Environmental Theory
Kuna baadhi ya maeneo yana rekodi kubwa ya vitendo vya kihalifu. Maeneo kama Lunga Lunga na Kibera nchini Kenya ni baadhi ya maeneo yaliyogubikwa na matendo mengi ya jinai. Hali hii husababisha watu wanaoishi katika mazingira haya kujikuta wanatenda jinai hata wakati mwingine wakiwa wanajihami dhidi ya vitendo vya jinai vilivyokithiri katika maeneo hayo hatarishi.

  1. Dhana ya mawazo/vikwazo/visasi au umaskini yaani Strain Theory
Watu wengine hujikuta wamejiingiza katika vitendo vya kihalifu ili kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili.Matatizo hayo yanaweza kuwa matatizo ya kifedha au hata msongo wa mawazo. Matatizo mengine husababishwa na umaskini kumgubika mtu ambaye huona njia mbadala ya kutatua umaskini huoni kujihusisha na vitendo vya kihalifu. Pia wapo watu ambao wamejiingiza katika vitendo vya kihalifu ili kulipa visasi kwa mabaya waliyotendewa.

  1. Dhana ya Kuamua kuwa Mhalifu yaani Rational Choice Theory.
Dhana hii imejikita katika kueleza kwamba mtu hujihusisha na uhalifu kama chaguo la maisha yake. Mhalifu huona ni sahihi kujihusisha na vitendo fulani vya kihalifu kama vile ujambazi ambavyo yeye ameviona ni njia sahihi ya kuendesha maisha yake.
 
Back
Top Bottom