SoC01 Nakulilia sana MamaTanzania

SoC01 Nakulilia sana MamaTanzania

Stories of Change - 2021 Competition

Gnyaisa

Member
Joined
Jul 13, 2021
Posts
23
Reaction score
24
Nikiitazama Tanzania ya nusu karne ijayo napatwa na furaha kubwa moyoni! Naiona Tanzania yenye kila namna ya neema na mafanikio ambayo taifa lolote lenye maliasili lukuki inapaswa kuwa nayo. Naiona Tanzania iliyojaa raia wengi wa kigeni hasa kutoka mataifa mbalimbali ya bara la Afrika wanaomiminika kwa wingi kujitafutia riziki na mafanikio ya maisha. Kama alivyokuwa kitovu cha ukombozi wa nchi nyingi za Afrika wakati wa kupigania uhuru miaka ya sitini na ya sabini, namuona mama Tanzania huyu huyu kwa mara nyingine tena akiwa kitovu cha ukombozi wa kiuchumi kwa nusu karne ijayo.

Kwa msomaji wangu ambaye pengine una mashaka na maono haya niliyonayo, basi ni Imani yangu mashaka hayo yataondoka hivi punde.

Tanzania ni Taifa la pili barani Afrika kwa kuwa na maliasili nyingi nyuma ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na hivyo kulifanya kuwa taifa lenye mvuto wa kipekee katika taswira ya dunia. Amani na utulivu iliyodumu kwa miaka nenda rudi inaendelea kuwa tunu muhimu katika kuvutia uwekezaji na kuifanya Tanzania kuwa mahali salama pa kuishi kuliko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inayoandamwa na machafuko ya mara kwa mara.

Nishati ya gesi asilia iliyozinduliwa hivi karibuni katika mikoa ya kusini mwa taifa letu inaipaisha Tanzania na kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa maliasili hiyo duniani. Kwa manufaa ya wasomaji wangu ni kwamba kwa mujibu wa hotuba ya waziri wa Nishati na Madini iliyotolewa hivi karibuni bungeni, kiasi cha gesi iliyogundulika nchini mpaka sasa kinafikia ujazo wa futi trilioni 56 sawa na mapipa ya mafuta bilioni 10.08! Gesi ambayo thamani yake ni Zaidi ya dola za kimarekani bilioni 831.62. Fedha ambazo zinaweza kutosheleza bajeti ya nchi kwa Zaidi ya miaka 50 mfululizo bila kutoza wananchi kodi yoyote! Utafiti huo wa gesi bado unaendelea na inasemekana kuna hazina nyingine kubwa bado haijazinduliwa!

Tanzania imegundulika hazina kubwa ya madini ya urani (Uranium) katika mikoa ya katikati ya nchi yetu yanayofikia thamani ya paundi milioni 119.4. Uzalishaji huu utaipaisha tena Tanzania na kuwa nchi ya tatu barani Afrika kwa uzalishaji wa madini hayo baada ya Niger na Namibia. Ni dhahiri Tanzania inaweza kuruhusiwa na umoja wa mataifa kuwa na vinu vyake vya urani kama ikitimiza masharti muhimu yaliyowekwa na umoja huo. Kwa manufaa ya msomaji wangu, madini ya Urani pamoja na mambo mengine yanatumika kuzalisha nishati ya umeme kwa kiwango kikubwa pamoja na kutengeneza silaha hatari za nyuklia.

Katika eneo la Engaruka lililopo Monduli mkoani Arusha imegundulika akiba kubwa ya magadi soda yenye mita za ujazo trilioni 4 na milioni 700 na hivyo kuifanya Tanzania iwe nchi ya tatu duniani kwa kuwa na akiba kubwa ya Magadi soda baada ya Marekani na Uturuki!

Miongoni mwa sababu zinazoifanya Malawi iingie katika mgogoro usiokwisha na taifa la Tanzania kwa kutaka kuchukua umiliki wote wa Ziwa Nyasa ni kwa sababu ziwa lile hasa kwa upande wa Tanzania limejaa hazina kubwa ya mafuta! Katika mikoa ya kusini inapopatikana gesi kuna ugunduzi wa hazina kubwa ya mafuta pia!

Tanzania ni miongoni mwa mataifa machache kabisa barani Afrika yenye fukwe ndefu ya bahari na iliyo salama kwa biashara za kimataifa! Ufukwe wa bahari ya Hindi iliyo mashariki mwa Tanzania ni miongoni mwa fukwe ndefu na salama Afrika hasa kwa upande wa Tanzania. Tayari bandari za Tanga, Bagamoyo na Mtwara zimeanza kujengwa kwa kiwango cha kimataifa ili kukidhi mahitaji ya soko kwa nchi za Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zenye uhitaji mkubwa wa huduma katika bandari hizo.

Tanzania ina akiba ya madini ya dhahabu inayofikia wakia milioni 36 hivyo kuifanya ishike nafasi ya tatu kwa orodha ya wazalishaji wakubwa wa madini hayo nyuma ya Ghana na Afrika ya Kusini

Hayo ni baadhi tu ya maeneo yanayonifanya niwe na maono yenye kunipa furaha kila nikiitafakari Tanzania ya nusu karne tu ijayo. Hapo sijazungumzia makaa ya mawe pale Kiwira yenye ujazo wa tani milioni 50.94 ambayo bado yako ardhini, wala sijazungumzia madini ya Tanzanite kule Mirerani, utitiri wa mbuga za wanyama kama Serengeti na Mikumi, visiwa Mashuhuri duniani vya Zanzibar, maelfu ya hekta za ardhi nzuri ya kilimo cha umwagiliaji, maziwa makuu duniani ya Tanganyika, Nyasa na Viktoria na utitiri mwingine wa maliasili!

Furaha yangu mara zote hukatishwa na kugeuka kuwa huzuni kila niitazamapo jamii ya watanzania wa leo hasa jamii ya vijana ambayo haioneshi kabisa kufanana na utajiri huo.

Nakulilia mama Tanzania kwa sababu licha ya utajiri mkubwa ulionao, viongozi wetu hawaoneshi dhamira ya dhati ya kuwaandaa wananchi wake kuumiliki na badala yake wamegeuka kuwa mchwa wa kutafuna rasilimali zetu na mawakala wa kuingia mikataba ya siri isiyo na masilahi yoyote kwa taifa.

Nakulilia mama Tanzania kwa sababu Vijana hasa wasomi ambao ndio tegemeo la taifa wamegeuka kuwa wanasiasa wa majukwaani wakiamini njia pekee ya kumkomboa mwananchi ni kugombea Urais, Ubunge au Udiwani badala ya kupambana katika kuanzisha makampuni ya kizalendo na kuchangamkia fursa zitokanazo na rasilimali lukuki tulizonazo!

Nakulilia mama Tanzania kwa sababu vijana wako wanakesha kwenye mitandao ya kijamii wakitumiana picha za “bethidei pati”, kutukanana, kusifiana na kuilalamikia serikali yao kutotimiza ahadi ya kuwatafutia ajira ilhali Wachina wakiendelea kuingiza nchini vijiti vya kuchomea mishkaki, pamba za kutolea uchafu masikioni na midoli ya kuchezea watoto.

Nakulilia mama Tanzania kwa sababu nusu karne ijayo uchumi wa taifa lako utakuwa mikononi mwa wakenya, waganda, wanigeria, wachina, waingereza na mataifa mbalimbali duniani yanayojua thamani ya utajiri uliopo nchini ilhali watu wako wakiishia kuwa vibarua katika mahoteli, viwanda na mashamba ya wageni kwa sababu kuajiriwa na kulipwa mshahara mkubwa ndio ndoto pekee aliyonayo msomi wa taifa hili!
 
Upvote 0
Back
Top Bottom