SoC02 Namna bora ya kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi

SoC02 Namna bora ya kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi

Stories of Change - 2022 Competition
Joined
Sep 15, 2016
Posts
18
Reaction score
9
Habari wapendwa,

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo kwa neema ya Mwenyezi Mungu. Kupitia jukwaa hili la "Stories Of Change" napenda kushiriki kwa kuja na mada isemayo "Namna Bora ya kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi"

Kwanini nimeamua kuja na mada hii?
1. Naamini ni njia mojawapo ya kuishauri serikali yetu yenye nia njema kwa Watanzania wote.

2. Naamini mada hii ndio hitaji kubwa la watu wengi Nchini kutokana na hali halisi ya kiuchumi na kipato cha mtu mmoja mmoja.

JE, NINI MAANA YA UKALI WA MAISHA?
Ni hali duni ya kiuchumi kwa wananchi ambayo hutokea kwa kipindi fulani kutokana na sababu mbalimbali za kisiasa, kijamii na hata kiutamaduni. Kwa mfano, ukali wa maisha wa sasa hivi umechangiwa kwa kiasi kikubwa na Vita kati ya Urusi na Ukraine, janga la UVIKO-19 na Usimamizi hafifu wa rasilimali za Taifa.

JE, KUNA VIASHIRIA VYOVYOTE VYA UWEPO WA UKALI WA MAISHA?
Hapa jibu ni Ndio. Viashiria hivyo ni kama vile wananchi kulalamika kupitia mitandao ya kijamii kuhusiana na bei za bidhaa na tozo mbalimbali Nchini, ukosefu wa ajira kwa vijana, Wananchi kusimamisha misafara ya viongozi mbalimbali na kuelezea hali zao, na mengi kadhalika.

JE, IPI NAMNA BORA YA KUPUNGUZA UKALI WA MAISHA KWA WANANCHI?

Zipo njia kadhaa ambazo ninazipendekeza kwa serikali yetu, lakini pia kwa mtu binafsi na zitaweza kuleta ahueni kwa wananchi.

1. KUSIMAMIA KWA UMAKINI RASILIMALI ZA TAIFA
Kumekuwa na usimamizi hafifu wa rasilimali fedha za umma katika miradi mbalimbali ya serikali jambo ambalo huibuliwa katika taarifa ya mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali (CAG). Baadhi ya Taasisi za umma huwa na matumizi yasiyo ya lazima au yasiyopangwa na kupelekea upotevu mkubwa wa fedha ambazo zingeelekezwa kuinua maisha ya wananchi. Hivyo nashauri uwepo usimamizi makini wa fedha za umma.

2. MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA KUKUSANYA MAPATO YOTE YA SERIKALI
Hii ni njia kubwa sana ambayo serikali inaweza kuitumia kudhibiti mapato yake yote na kuziba mianya ya upotevu wa fedha na rushwa ambazo zinaumiza Wananchi wa hali ya Chini. Hivyo nashauri Serikali yetu kuandaa mifumo maalumu ya "Digital Sale and Buy Direct Tax" kwa maana ya kwamba ni kodi ambayo kila Mtanzania ataweza kuilipa kidigitali moja kwa moja kila anunuapo na kuuza bidhaa. Hapa namaanisha serikali ije na kadi maalum kwa ajili ya manunuzi. Kadi hii itafanya malipo pale mteja atakaponunua bidhaa, ataskani tu kwenye "POS" ya muuzaji na kuandika "Amount" kisha risiti itatoka hapohapo ikiwa na majina pamoja na kodi aliyolipa kwa kununua ile bidhaa sokoni au dukani au popote pale. Ni rahisi tu kusema mfumo wa "Cash payment" uondolewe. Hii itapunguza ukiritimba katika huduma na bidhaa nyingi hivyo kuisaidia serikali kupata fedha nyingi ili kuwahudumia wananchi ipasavyo.

3. KUPUNGUZA MATUMIZI YASIYO YA LAZIMA NA KUPUNGUZA BAJETI ZA MATUMIZI YA LAZIMA KATIKA TAASISI ZA UMMA.
Kwa mfano, mtumishi mwenye mshahara mkubwa kuliko hata yule mtu wa chini anawezaje tena kupewa kile kinachoitwa "marupurupu"? au fedha ya mawasiliano, sijui mafuta n. k. Je huyu mwalimu wa mshahara wa laki 2, anapewa na nani hayo? Tunaweza kujibana kwa kipindi fulani kwa manufaa ya Taifa na Wananchi wote wafurahie matunda ya Nchi yao.

4. WANANCHI KUACHA KUCHAGUA KAZI ZA KUFANYA, LAKINI PIA KUPENDA KILE WANACHOFANYA.
Ni vema kila mwanachi kuwa na shughuli halali yoyote ya kumuingizia kipato na kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kujinusuru na ukali wa maisha.

5. SERIKALI KUTOA AHUENI KWA KODI NA TOZO MBALIMBALI NCHINI
Tanzania yetu bado ni Nchi inayoendelea, Tangu tupate uhuru mwaka 1961 hatujaweza kufikia malengo yote katika kupambana na ujinga, maradhi na umaskini, hivyo sioni sababu kubwa sana ya kutaka kumaliza hayo yote kwa haraka. Tuende taratibu kama Taifa tutafika tu. Kodi na Tozo ni muhimu sana kwa Taifa lakini Wananchi na maisha yao ni muhimu zaidi.

Tupunguze kodi katika huduma za mawasiliano ili kuiwezesha "ISPs" watoe huduma bora na zenye gharama nafuu, pia Tuondoe au tupunguze tozo katika miamala ya simu na Benki kuongeza mzunguko wa fedha Nchini. Kuhusu mfumuko wa bei (Inflation) tuna wastani mzuri kulinganisha na majirani zetu, haiwezi kushindwa kuhimilika kabisa.

Ruzuku katika mafuta iongezwe kutoka asilimia kadhaa katika matumizi ya serikali yatakayopunguzwa ili Wananchi katika Ajira za Bajaji na Bodaboda au daladala wapate unafuu. Hii itapunguza hata bei ya usafiri huo kwa Wananchi wote.

Baada ya kusema hayo, Natanguliza shukrani zangu za dhati kwa watu wote wenye nia Njema na Taifa letu. Tuzidi kuwaombea viongozi wetu wa Serikali hasa Mheshimiwa Rais, Mawaziri, Wabunge na viongozi wengine wote Mungu azidi kuwapa Hekima Katika kuliongoza Taifa Hili. Amen.
 
Upvote 2
Back
Top Bottom