SoC04 Namna Nchi yetu inavyoweza kufanya mapinduzi makubwa ya sayansi na teknolojia

SoC04 Namna Nchi yetu inavyoweza kufanya mapinduzi makubwa ya sayansi na teknolojia

Tanzania Tuitakayo competition threads

Quartz360

Senior Member
Joined
Mar 27, 2023
Posts
133
Reaction score
317
TANZANIA TUITAKAYO

MWANZO WA ANDIKO

Katika karne hii ya 21, hapana shaka ya kuwa mapinduzi ya sayansi na teknolojia yamekuwa ni makubwa kiasi cha kuleta mapinduzi makubwa ya viwanda sehemu nyingi sana duniani, kuzalisha ajira nyingi, kutatua matatizo katika jamii na kurahisisha namna ya ufanyaji wa kazi, zaidi ya yote mapinduzi hayo yameweza kuzalisha mabilionea wengi sana duniani. Katika hili Tanzania hatuwezi kujiweka pembeni kwani kupitia mapinduzi ya sayansi na teknolojia ndipo maendeleo katika sekta zote yatapatikana kwa kiwango cha juu. Kutokana na taarifa za kielelezo cha kimataifa cha ubunifu, Global Innovation Index (GII) iliitaja Tanzania kuwa nchi ya 103 duniani katika maendeleo ya teknolojia kwa mwaka 2022. Hii inaonyesha ni kwa kiasi gani bado tuna kazi ya ziada ya kufanya kuendana na mabadiliko hayo.

KIINI CHA ANDIKO

Ili kuweza kufanya mapinduzi makubwa katika eneo la sayansi na teknolojia, mikakati ifuatayo haina budi kufanywa.

1. Kufanywe uhakiki wa mitaala yote inayojikita kuzalisha wataalamu wa sayansi na teknolojia. Mitaala yote inapaswa kufanyiwa maboresho ili kuendana na mabadiliko ya dunia inavyokwenda, mitaala hiyo ijikite katika kuwajengea uwezo wataalamu wa masuala ya sayansi na teknolojia kama vile wataalamu wa mifumo ya kompyuta, wahandisi na madaktari, ili waweze kuwa na umahiri thabiti utakao ibua fikra jengefu katika ulimwengu wa teknolojia na kuleta mapinduzi makubwa katika teknolojia.

2. Serikali iongeze bajeti katika eneo la ubunifu na tafiti kwa kuhakikisha wataaalamu wa masuala ya teknolijia wana pata vitendea kazi muhimu, mazingira na maarifa sahihi yatakayowasaidia kufanya gunduzi zenje tija, kutatua matatizo ya kiteknolojia, kuimarisha mifumo ya kiusalama na kuinua uzalishaji mali katika taifa letu. Bajeti hiyo ilenge pia katika kuboresha mifumo ya ujifunzaji kwa wanafunzi, hii itawapa uwanda mpana wa kuweza kubuni mawazo bora zaidi.

3. Kuwepo na senta moja kwenye kila mkoa itakayokuwa kitovu cha ugunduzi katika mkoa husika, kituo hicho kiwe na wataalamu wa sayansi na teknolojia watakao fanya kazi ya kuwawezesha wagunduzi mbalimbali katika mkoa husika, kuwapeleka katika vituo hivyo, kuwasaidia kuboresha mawazo yao, kuwapa rasilimali stahiki na usaidizi wowote wa kitaaalamu katika kukuza, kuimarisha na kuendeleza ubunifu wao. Vituo hivi pia vianzishe mikakati maalumu ya kuibua wanasayansi wachanga katika jamii watakao kuwa msaada wa baadae katika taifa letu.

4. Kuanzishwe mashindano ya kitaifa na kimataifa katika eneo la sayansi na teknolojia, mfano kila mwaka kunapaswa kuwe na mashindano ya ubunifu kwa vyuo na taasisi zote nchini, mashindano haya yalenge kupata wabunifu bora wa masuala ya sayansi teknolojia na baada ya kuwapata washindi zawadi zitolewe, misaada ya kifedha itolewe, hati miliki ya ubunifu wao na wapewe nyezo zote muhimu za kuboresha na kuuza ubunifu wao, vilivile washindi wote katika ubunifu wa sayansi na teknolojia waunde timu itakayo iwakilisha nchi yetu katika mashindano ya kimataifa, hii italeta hamasa ya kufanya bunifu zenye ushindani, itawaongezea maarifa na ari ya kuweza kufanya gunduzi nyingi zaidi zitakazoleta heshima, kuwatangaza ulimwenguni wao binafsi pamoja na taifa lao kwa ujumla na mwisho taifa na dunia kwa ujumla iweze kufaidika na ubunufu huo.

5. Kuanzishe kituo kikuu cha sayansi na teknolojia kitakachokuwa ndicho kitovu cha mapinduzi katika nchi yetu. Kituo hiki kitakuwa ni kioo cha maendeleo ya teknolojia katika nchi yetu, kitawaleta wabobezi wote kutoka katika kila vituo vya ugunduzi vya kila mkoa, ambapo kazi kuu ya kituo hicho kikuu itakuwa ni kutafsiri gunduzi zote kwenda kwenye vitendo, kwa maana hiyo vituo vya mikoani vitafanya upembuzi wa mawazo, kukuza uwezo wa bunifu na kuboresha mawazo yao, na kituo kikuu cha kitaifa cha ubunifu kitakuwa na kazi moja tu ya kuhakikisha mawazo ya wabunifu hao yanawekwa kwenye vitendo mara moja ili kuweza kuchochea mabadiliko katika nchi yetu.

6. Serikali ianzishe programu ya kupeleka wataalamu kwenda nje ya nchi kila mwaka. Nchi nyingi zimeweza kuendelea katika mapinduzi ya kiteknolojia kwa kuwatuma wataalamu wake wa ndani kwenda kujifunza nje ya nchi na mwisho kuleta gunduzi hizo na kufanya maboresho muhimu tayari kwa matumizi katika nchi zao. Hivyo, ni wakati sasa wa nchi yetu kuandaa programu ya kuwapeleka wataalamu wetu katika mataifa ambayo ni imara kwenye eneo la teknolojia mfano Afrika kusini, Nigeria, Misri na Kenya kwa hapa Afrika pamoja na China, Marekani, Japan, Ujerumani, Uingereza, India, Urusi na Korea. Ushirikiano wa kidiplomasia katika nchi hizo uwe ni mwanya wa kupenyeza wataalamu wetu kwenda kujifunza na kuleta maarifa hayo ndani ya nchi yetu, kwa sababu maarifa daima hayana mpaka wa kijiografia, hivyo tunaweza kufaidika na programu hizo kupitia wataalumu wetu watakao kwenda kupata maarifa mapya ya kibunifu nje ya nchi.

7. Serikali itengeneze sera na sheria madhubuti zitakazo chochea ubunifu. Ili kuhakikisha mapinduzi ya sayansi na teknolojia inakuwa ni ajenda ya kitaifa, kuwepo na sheria thabiti zitakazo linda haki za wataalumu wa masuala ya sayansi na teknolojia, hii itawapa uhuru na hamasa ya kuweza kuleta mawazo yao katika uhalisia bila kusumbuliwa na mtu ama taasisi yeyote, sheria hizi pia zitalinda masirahi yao kwa kuwapa haki ya kisheria kufaidika na ugunduzi wao, sera zenye kuhimiza gunduzi mbalimbali pia ni muhimu ziundwe, na zile zilizopo ziboreshwe ili ziendane na maono ya taifa katika maendeleo ya sayansi na teknolojia.

MWISHO WA ANDIKO
Jukumu la kuleta mabadiliko katika nchi yetu yako mikononi mwetu pekee, daima hatuwezi kufanya mapinduzi ya sayansi na teknolojia kwa kusubiri taifa ama mtu flani kutoka nje aje atusaidie, tuna jukumu la kuanza na kile tulichonacho kama taifa, kwa kutumia rasilimali zetu chache tuweze kuunganisha nguvu zetu,tuwe na mikakati thabiti na ari ya kuimarisha teknolojia yetu ili tuweze kuifikia Tanzania tuitakayo, Tanzania ya viwanda itakayokuwa kiini cha mabadiliko na mfumo mzima wa maisha ya watanzania kwa kikazi cha sasa na cha baadae.
 
Upvote 2
Back
Top Bottom