SoC04 Namna taifa letu linavyoweza kufaidika na balozi zake zilizo nje ya nchi

SoC04 Namna taifa letu linavyoweza kufaidika na balozi zake zilizo nje ya nchi

Tanzania Tuitakayo competition threads

Quartz360

Senior Member
Joined
Mar 27, 2023
Posts
133
Reaction score
317
TANZANIA TUITAKAYO

UTANGULIZI
Kwa kiasi kikubwa nchi nyingiulimwenguni huweza kuwa na ubalozi katika nchi mbalimbali duniani kwa lengo la kuwakilisha na kulinda maslahi ya taifa husika katika nchi nyingine, kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia, kusaidia raia wa nchi yake wanaoishi nje pamoja na kukuza ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kitamaduni.

Katika hili, serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania haijaachwa mbali, kwani ina balozi katika nchi mbalimbali duniani kma vile Kenya, Uganda,Afrika Kusini, China, Marekani, India, Japan, Ujerumani, Uingereza na kwenye nchi mbalimbali kwa lengo la kulinda maslahi ya Tanzania katika nchi husika.

KIINI CHA ANDIKO
Katika kuifikia Tanzania tuitakayo, kama taifa hatuna budi kuzitumia vyema balozi zetu zilizo nje ya nchi kwa maslahi mapana ya taifa letu katika nyanja zote kwa kufanya yafuatayo;-

SEKTA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Kupitia balozi zetu zilizo nje ya nchi tunaweza kuinua hali ya elimu katika nchi yetu kwa kila ubalozi husika kujenga mahusiano na taasisi za kielimu huko nje kama vile vyuo vikuu na taasisi za utafiti zitakazokuwa na mahusiano ya moja kwa moja na vyuo vikuu vilivyopo katika nchi yetu, hii itatoa wasaa kwa wataalumu kutoka katika vyuo ama taasisi hizo kubadilishana maarifa na wataalamu wetu wa ndani, pia itatoa wasaa kwa wanafunzi wetu kwenda kupata elimu iliyo bora zaidi katika taasisi hizo na kuwajenga kikamilifu katika kuleta mabadiliko katika nchi yetu, vilevile nchi itapata darasa juu ya namna gani iweze kubadili mifumo yake ya elimu kwa kujifunza namna nchi zingine zinavyofanya katika mifumo yao ya elimu.

SEKTA YA AFYA
Kupitia mahusiano ya kidiplomasia nje ya nchi, sekta ya afya inaweza kuimarika kwa kuandaa program maalumu kila mwaka zenye lengo la kupeleka wataalamu wetu kwenda kujifunza katika mataifa hayo, na kutoa wasaa kwa nchi kupokea wataalamu wa afya kutoka kwenye nchi hizo kwa lengo la kuja kuwaongezea maarifa, ubunifu na uwezo wataalamu wetu wa ndani mfano madaktari na manesi. Vile vile kupitia balozi zetu, kama taifa tutaweza kuboresha mifumo yetu ya afya kwa kutumia teknolojia ya kisasa inayoendana na hali ya ulimwengu kwa sasa na hivyo kuimarisha afya za watanzania na wale wote watakaopata huduma nchini kwetu.

SEKTA YA KILIMO
Kulingana na taarifa ya wizara ya kilimo iliyosomwa na waziri wa kilimo Mheshimiwa Hussein Bashe katika bunge la bajeti la 2023/2024 nchini Tanzania zaidi ya asilimia 70% ya watanzania wanafanya shughuli za kilimo, lakini ni asilimia chache sana ya pato la taifa hutoka kwenye kilimo ukilinganisha na idadi ya watu katika sekta husika. Hii inaonyesha dhahiri namna sekta yetu ya kilimo ilivyo na changamoto nyingi, hivyo kwa kutumia balozi zetu zilizo nje ya nchi tunaweza kupeleka wataalamu wetu wa masuala ya kilimo kwenda kujifunza njia bora za kuinua sekta yetu ya kilimo, mabadiliko ya sera na miongozo ya kilimo, kuwa na makongamano ya kimataifa ya kilimo kati ya nchi washirika, kuwatafutia masoko ya uhakika watanzania wanao zalisha bidhaa za kilimo ndani ya nchi yetu, ambao wengi wao hushindwa kupata faida katika kilimo kwa kukosa masoko ya uhakika ndani ya nchi. Hivyo kutekeleza mikakati hiyo italeta fursa lukuki katika sekta yetu ya kilimo.

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
Bila shaka nchi yetu ni miongoni mwa nchi iliyojaaliwa vivutio vingi sana vya utalii kama vile milima, maziwa, mito, misitu, maporomoko ya maji, tamaduni za asili, mbuga za wanyama na madini mbalimbali, hivyo vyote ni chachu ya maendeleo katika nchi yetu. Hivyo ni vyema kwenye kila nchi ambapo kuna ubalozi wetu kuwe na programu za mara kwa mara zinazowakutanisha wadau wa nchi husika katika kutangaza vivutio vya nchi yetu, ni vyema kila ubalozi uwe na chaneli ama kipindi maalumu katika moja ya vituo vya televisheni katika nchi husika hii itatoa wasaa kwa ubalozi kutangaza hazina zetu kama taifa ili kuweza kuvutia watalii kuja nchini kwetu, vilevile kuwe na majarida maalumu yatakayochapishwa kila baada ya mda flani mfano kila mwisho wa mwezi yanayoelezea kwa undani kuhusu nchi yetu, hazina zetu na fursa za uwekezaji zilizo katika nchi yetu. Vile vile balozi zetu zitoe fursa kwa wanafunzi kutoka hizo nchi kuja kujifunza nchi kwetu mambo mbalimbali, hii itaamusha ari ya ukuaji katika sekta yetu ya utalii.

KATIKA SEKTA YA MICHEZO
Tuna balozi zetu katika nchi ambazo ni imara katika sekta ya michezo kwa mfano Uingereza, Ujerumani, Uholanzi, Ufaransa na nchi nyinginezo. Hivyo ni vyema kukawekwa ajenda ya kitaifa yenye lengo la kuboresha sekta ya michezo nchini kwa kutumia balozi zetu kuimarisha mahusiano na mashirikisho ya nchi husika katika sekta ya michezo. Inapaswa kuwe ya mikakati ya kuwatafutia nyezo nje ya nchi watanzania wenye vipaji katika michezo kwa kushirikiana na balozi zetu nje ya nchi ambapo vijana wetu watapata nafasi ya kwenda nje ya nchi ili kuweza kuboresha vipaji vyao, kupata maarifa thabiti na ushindani utakaoleta manufaa kwa mtu binafsi, jamii na taifa kwa ujumla. Vile vile kuwepo na mashindano ya mara kwa mara kati ya nchi washirika hii italeta chachu ya maendeleo katika sekta yetu ya michezo.

SEKTA YA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI
Balozi zetu zitengeneze mikakati wezeshi itakayofungua fursa za uwekezaji na maendeleo ya viwanda katika nchi yetu. Inabidi kuwe na njia shirikishi zitakazo wapa fursa wafanyabiashara wa Tanza nia kuweza kupata masoko ya bidhaa zao nje ya ya nchi, kukutanishwa na wafanyabiashara kutoka nje ya nchi, kuimarisha sera na sheria za ufanyaji biashara na kutoa taarifa sahihi na nyezo sitahiki kwa wawekezaji kutoka nje ya nchi kuja kujionea fursa za uwekezaji zilizo katika nchi yetu.

HITIMISHO
Hakuna kitakachotuzuia kama taifa kuweza kuifikia nchi ya ahadi, mathalani hatuna sababu ya kushindwa kupata mabadiliko hasa ya kiuchumi katika nchi yetu. Balozi zetu ziwe nyezo muhimu na thabiti katika kuchochea maendeleo katika nchi yetu, tunahitaji Tanzania yenye nguvu, tunahitaji Tanzania ambayo kila raia atajivunia kuishi, Tanzania ambayo itakuwa mfano wa kuigwa kote duniani, hivyo serikali iandae mpango madhubuti utakaotoa mwelekeo chanya kwa kuhakikisha balozi zetu nje ya nchi zinakuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo nchini.
 
Upvote 0
Back
Top Bottom