SoC03 Namna utawala bora utakavyotukwamua kiuchumi

SoC03 Namna utawala bora utakavyotukwamua kiuchumi

Stories of Change - 2023 Competition

MombaDier

Senior Member
Joined
Jul 24, 2022
Posts
123
Reaction score
232
Teknolojia ni moja ya nyenzo ya maendeleo duniani kote karne hii ya 21, jamii yenye kukimbizana na kasi ya ukuaji wa kiteknolojia ni jamii iliyoamua kuifata njia sahihi ya maendeleo. Maendeleo ni mchakato uhusishao matumizi ya sayansi na teknolojia yanayopelekea mabadiliko chanya kiuchumi, kiutamaduni, kisiasa na kijamii. Moja ya kitu muhimu katika taifa lolote linaloendelea ni kuwa utawala bora.

Utawala ni mpango wa udhibiti na usimamizi wa rasilimali za umma kwa faida ya jamii, utawala bora huchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia mifumo ya uwajibishwaji kwa wavunjaji wa sharia. Uongozi wenye kuwajibika kwa kusimamia misingi ya kidemokrasia kama vile usawa, uwazi na uzingatiaji wa haki za binadamu hutambulika kama utawala bora.

Jamii nyingi barani Afrika viongozi na raia wake kwa ujumla wameshindwa kuendana na matwakwa ya uwajibikaji kwani vitendo kama vile rushwa, ubaguzi na kujilimbikizia mali  vimekua ni alama ya kudumu mithili ya ndui iliyoko bega la kushoto la mtanzania, yaani hatozaliwa nayo ila atazikwa nayo. Raisi mstaafu Hayati Mwalimu J.K. Nyerere alisema “Hatuwezi kutatua matatizo yetu kwa kujidanganya kuwa hayapo, ndiyo hapa naizungumzia rushwa.

Rushwa sasa umekuwa ni wimbo usiohitaji mapati mfululu ili upate mwitikio wa kutosha kwa wasikilizaji wake. Rushwa imetapakaa barabarani, hospitalini, katika ofisi za umma na taasisi binafsi, shuleni, vyuoni, kwenye ajira, michezo na siasa ni Rushwa! Rushwa!! Rushwa!

Kwa hali ilivyo sasa rushwa imekuwa ni dini watu wanaiabudu na wala hawataki kuiacha mana imekuwa ikiwanufaisha kila kukicha. Viongozi mpaka raia wake wamekuwa wapenzi wa mserereko nani wakuikomesha sasa, yaani kuiweka rehani sehemu ya mwili kwa kitendo cha muda usiozidi saa moja, kwa kumburudisha mtoa fursa katika chumba na kitanda ghali tena burudani yenyewe ni ile ya nipe nikupe raha tupate alafu baadaye anampatia fursa yenye malipo ya kila mwezi na hapungukiwi chochote kwanini akamchomeshe. Yaani kumpatia elfu tano mhudumu wa ofisi ya umma ili akuharakishie jambo lako ukaepukana na kupoteza muda kwenye foleni utapungukiwa nini. Hivi ndivyo namna ambavyo rushwa imeendelea kujiongezea wigo katika maisha yetu ya kila siku.

Swala la ubadhilifu wa mali za umma limeendelea kuwa changamoto barani Afrika, viongozi wengi wamekua wakijilimbikizia mali bila uwoga wala kificho. Mwalimu J.K. Nyerere alisema “Utumishi wa umma ni kazi ya kujitolea sio pa kujilipa mamilioni”. Kwa kiasi kikubwa wametuvunja mioyo raia wao kwani kila kiongozi tuliyemwamini akawe mtetezi wa mali za umma badala yake ndiyo wamekuwa watesi wakubwa wa mali hizo. Kujilimbikizia mali ekari kwa ekari, mamilioni kwa mamilioni kwao umekuwa mchezo mwepesi mno kuushinda hata ule wa tule tumbakishie baba kwani amekosekana kabisa wa kumfunga paka kengele na hatimaye kila aliyechaguliwa ameamua kula kutokana na urefu wa kamba yake mithili ya mbuzi aliyefungwa kwenye malisho yaliyo karibu na nyumbani.

Usiginaji wa haki za binadamu pia limekuwa ni janga kubwa barani Afrika linaloutafuna utawala bora. Kama zilivyoelezewa katika Azimio la kimataifa la haki za binadamu la mwaka 1948, haki za binadamu ni pamoja na haki ya kuishi, kupata elimu, kumiliki mali, kupiga kura katika uchaguzi huru, kutoa maoni yake kwa uhuru, kupinga pamoja na wengine maazimio ya serikali kwa njia ya Amani, kutokamatwa kwa kosa la mtu mwingine, kuwa salama na kutotishwa. Kwa kiasi kikubwa kumekuwa na upuuzwaji wa haki hizo kwani hata yule aliyebahatika kuipata elimu hakuweza kukwepa kutishiwa ama kukamatwa kwa kosa la mtu mwingine.

Kwa hili ningependa zaidi niizungumzie nchi yangu ya Tanzania ambayo vitendo vya kukatishana maisha kwa wivu wa kimapenzi, Imani za kishirikina ama tamaa za kumiliki mali na kupanda cheo kwa njia zisizo halali vimekuwa vya kawaida mithili ya kuagiza supu kwa chapati mbili. Licha ya kuripotiwa na vyombo vya habari kwa ukubwa wake na hata katika ofisi mbalimbali za maswala ya kisheria na haki za binadamu lakini utekelezaji wake umekuwa ni wa duni sana (hili nalo limekuwa halina tofauti na zimwi likujualo).

Kwa upande mwingine haki kama vile kupiga kura katika uchaguzi huru, kutoa maoni kwa uhuru pamoja na kupinga maazimio ya serikali kwa njia ya Amani zimekuwa si haki tena. Hili nalisema wazi nikilielekeza kwa viongozi wa taifa hili kwani Baba wa taifa katika uhai wake aliwahi kusema “Itakuwa ni kosa na haina umuhimu kudhani kuwa ni lazima tusubiri hadi viongozi wafariki kabla ya kuanza kuwakosoa”. Kiukweli viongozi wetu wameshindwa kututekelezea haki ya kuwa na uchaguzi huru chini ya tume huru ya uchaguzi, chaguzi nyingi zimetuletea viongozi wa hovyo wanaojali matumbo yao kwasababu zimekuwa zikiendeshwa kihuni. Mwalimu Nyerere alisema “Utii ukizidi unakuwa uoga, uoga huzaa unafiki na kujipendekeza mwisho wake ni umauti”, binafsi naweza kuwa na uoga ila siupendi unafiki. Ukweli ni kuwa nchini mwetu swala la kutoa maoni kwa uhuru pamoja na kupinga maazimio ya serikali kwa njia ya Amani ni haki ambazo zinasiginwa waziwazi kwani nani hakuwepo kipindi kile mikutano ya vyama vya siasa ilivyopigwa marufuku pasi na sababu ya msingi? Ama ni nani ambaye hasikii kupigwa marufuku kwa maandamo mbalimbali ya Amani kupinga kile kinachofanywa na viongozi wetu?

Ni lazima viongozi wetu waturejeshee haki hizi walizotunyanganya kwa manufaa ya ustawi wa taifa letu. Kwa uhalisia tunaachwa mbali mno na kasi ya ukuaji wa teknolojia hali ambayo inatupelekea kuwa nyuma kimaendeleo. Afrika kama bara, Tanzania kama nchi ni muda sahihi sasa kupambana na maadui zetu rushwa, ubadhilifu wa mali za umma pamoja na usiginwaji wa haki za binadamu kwani maadui hawa wamesababisha upofu kwa viongozi wetu wa umma ambao wamejitenga na uwajibikaji na kuwasahaulisha kuhusu utawala bora.

Kukosekana kwa utawala bora kumetufanya tushindwe kupiga hatua za haraka katika kuyaendea maendeleo ya kichumi, kitamaduni, kisiasa na kijamii yanayochochewa na ukuaji wa teknolojia na hatima yake ni huu umasikini unaotuandama hadi kenye kucha. Tukiutua mzigo huu toka kwa viongozi wetu pia ni muhimu kwa umoja wetu kuikemea na kuikataa rushwa kwa kuvitaarifu vyombo husika pale tuonapo dalili za kuwepo kwake. Maswala ya ubadhilifu na usiginaji wa haki za binadamu pia si vitendo vya kuvifumbia macho ni muhimu kuviweka wazi pale tu zionekanapo dalili zake. Mwisho niombe tujiepushe na vitendo vya kuwakatili wenzetu kwa kuwakatisha uhai kwa mambo yasiyo ya msingi eti tamaa ya mali ama wivu wa kimapenzi.

Ni mimi fahari ya Tanga, karibuni kilindi.
 
Upvote 3
Back
Top Bottom