SoC01 Namna wananchi, Vyama vya Siasa, Serikali na Taasisi mbalimbali wanapaswa kuona umuhimu wa Katiba Mpya nchini

SoC01 Namna wananchi, Vyama vya Siasa, Serikali na Taasisi mbalimbali wanapaswa kuona umuhimu wa Katiba Mpya nchini

Stories of Change - 2021 Competition
Joined
Dec 10, 2020
Posts
15
Reaction score
14
Kwanza katiba ni nini? Katiba ni mwongozo wa kanuni na taratibu za kila siku za nchi. Katiba tunaweza kusema ndiyo nchi yenyewe maana hata viongozi na raia wapo chini ya mwongozo wa katiba.

Katiba ndiyo huleta muundo na mustakabali wa sheria, serikali na vitu vyote vinavyolihusu taifa. Katiba nzuri ndiyo msingi mzuri wa taifa na uzuri wa katiba hupimwa na kukidhi mahitaji ya wakati huo wa sasa na wa baadae, si dhambi kubadili katiba kulingana na uhitaji na kuna wakati linakuwa jambo la lazima kama kuna mahitaji ya lazima.

Zipo nchi ambazo zina katiba nzuri kutokana na kutengenezwa kwake kwa kukidhi mahitaji ya wakati uliopo na wakati mwingi ujao hii ni kutokana na umakini mkubwa mno katika utengenezaji au uundaji wake mfano wa nchi hizo ni kama Marekani.

Uhitaji wa katiba mpya hapa kwetu ukoje? Bila kwenda mbali sana inabidi kuweka kumbukumbu kwamba katika kipindi cha serikali ya awamu ya nne tayari mchakato wa katiba mpya ulikuwa umeshaanza hapa nchini ambapo tayari bunge maalumu lilikuwa limeundwa na rasimu zilikuwa tayari zimeshaanza kukamilika ikiwa ni pamoja na rasimu ya Warioba na mchakato wa kukusanya maoni ulikuwa unaendelea. Hii inadhihirisha wazi kuwa tayari uhitaji wa katiba mpya hapa nchini ulikuwa unaulazima.

Kusitishwa kwa mchakato huo bado kunaweza kuibua hoja za kwa nini haikuweza kuendelea katika awamu ya tano na ukizingatia kuwa mchakato huo ulikuwa chini ya mwendelezo wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi na bado awamu ya tano ilikuwa chini ya chama kile kile. Mpaka hapo nadhani kwa uelewa halisi mtu anaweza kujiridhisha kuwa uhitaji wa katiba mpya ni jambo linalohitajika kwani hii inatoa funzo kubwa kuwa huenda kutokana na hali kama hiyo mambo mengi ya muhimu hayakamiliki hasa kutokana na udhaifu wa katiba maana tungetaraji hata mchakato huo ungekuwa umeshakamilika kama Katiba iliyopo ingekuwa inahimiza vitu vingi kukamilika.

Lakini pia bado umuhimu wa uhitaji wa katiba mpya hapa nchini ni mkubwa na jamii nzima na umma wa watanzania unapaswa kuelewa mambo mengi juu ya uhitaji huo lakini Kabla ya kwenda mbele zaidi ni vyema kuweka msistizo kuwa katiba si takwa la chama fulani ama kimo madarakani kwamba kinaona katiba mpya itakitoa madarakani ama hakimo madarakani kinaona katiba mpya itakiingiza madarakani hapana!Hilo si takwa la katiba, katiba ni takwa la kitaifa.

Vyama vya siasa, wananchi wa kawaida, taasisi mbalimbali, serikali na asasi za kiraia na zisizo za kiraia kwa pamoja wanatakiwa kutambua dosari za katiba ya awali kuweka mipango kwa ajili ya kuweka katiba mpya imara ambayo itasimama kwa ajili ya taifa hata kama chama fulani au vyama vyote vilivyopo havitakuwepo ila katiba iweze kusimama na kulitetea, kulilinda, kulikuza na kulijenga taifa kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiteknolojia.

Ni vyema pia kukumbuka kuwa, serikali makini na uongozi makini ndiyo inaweza kulikomboa taifa hata kama haitakuwepo ama hawatakuwepo waliofanikisha hayo, bado tunaona mifano mizuri ya viongozi kama J.K. Nyerere alivyolikomboa taifa hili. Hapa niweke wazi tu kuwa moja ya jambo ambalo linaniumiza ni kwa nini hayati rais Magufuli hakuendeleza mchakato wa Katiba. Hii ni kwa sababu umakini wake mkubwa na uongozi wake shupavu aliokuwa nao angeweza kuacha katiba imara yenye maono makubwa na ya msingi sana kwa nchi hii, Mungu ampumzishe salama.

Lakini hata hivyo bado hatujachelewa bali ni jambo tu la kuweka utambuzi na kuweka moyo wa kutaka kufanya na kukamilisha kitu hiki cha msingi kabisa katika taifa bila kujali vyama vyetu vya siasa, dini, makabila itikadi na tofauti ndogondogo ambazo katika misingi ya kitaifa tunapaswa kuzisahau.

Labda tuanzie hapa kwa nini kuna umuhimu wa katiba mpya hapa nchini, lakini kama tulivyoanza ni kwamba, kuanza tu kwa mchakato katika awamu ya nne ni dhahiri kuna uhitaji, kwanza kabisa tutaanza na kuelezea japo tuone tu kwa ufupi katika masuala muhimu na umuhimu wake wa katiba mpya tukianzia kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiteknolojia japo tukigusia kidogo kidogo kila sehemu sababu mambo hayo ni mapana sana hivyo jamii ipate tu walau mwanga.

Tukianzia na uchumi, tumrejelee rais Magufuli pindi alipoanza kurekebisha mikataba mibovu ya madini ni wazi kuwa nchi yetu tayari ina rasilimali na utajiri mkubwa wa madini ambayo tayari yameshagunduliwa na ambayo pengine bado hayajagunduliwa. Suala la rais Magufuli kuanza kurekebisha mikataba mibovu ya madini tayari tunaona kuwa kuna kasoro katika katiba yetu! Sababu ya msingi ni kuwa katiba haijaweka msingi thabiti na imara wa usimamizi na ulinzi imara katika kuhakikisha rasilimali zilizopo zinalinufaisha zaidi taifa letu ikiwa ni pamoja na kuleta kipato na thamani ya nchi.

Kukosekana kwa msingi huo ndiyo maana viongozi wanakuja na sera na sheria ambazo zinaliathiri taifa ikiwa ni pamoja na kutia saini mikataba mibovu na hapo katiba haina sahemu ya kumwajibisha kwa kutotunza rasilimali ya taifa lake.

Halikadhalika, katika kipengele cha kisiasa bado tunahitaji Katiba yenye kuweza kuweka misingi imara ikiwa ni pamoja na mipaka ya nguvu za uongozi mfano kiongozi wa juu wa serikali iorodheshe vitu anavyopaswa kufanya na visivyopaswa kufanywa ikiwa ni pamoja na uwezo wa kujiondoa mwenyewe madarakani ikibainika kafanya isivyotakiwa kikatiba. Hata hivyo tumeona hata baadhi ya mataifa viongozi wakijiuzulu kutokana na takwa la kikatiba.

Lakini pia kuwepo na mpaka wa kuleta ajenda zinazohusiana na uchaguzi mara baada ya uchaguzi kuepusha kero nyingi katika uongozi na kuheshimu uongozi hii ni kwa sababu kuna uchochezi mwingi katika siasa na hata hivyo, ikitokea kiongozi kakosea kuwe na takwa la kikatiba linalomlinda kutokutukanwa hovyo bali akosolewe, na pia vyama vyote vijikite katika kushawishi watu na si kutumia nguvu sababu demokrasia si nguvu ya matusi, nguvu ya fujo bali ni ushawishi.

Katika kipengele cha kijamii, hapa mfano wa suala la elimu utatumika, na hapo tuangalie kwa nini nchi inahitaji katiba, moja kwa moja ni sababu kuu kuwa mfumo wa elimu unahitaji kujengwa katika katiba iliyo hai, hasa katika kuweka malengo makuu na madogo madogo na kwa kuzingatia ukubwa wake na kwa vizazi na vizazi, hii ni kutokana na hali ya hivi kuribuni kuonekana elimu ni kitu cha kuchezeachezea kadiri kiongozi/uongozi unataka mfano, kumekuwepo na ajenda nyingi ambazo hazina tija mfano kati ya mwaka 2012 na 2013 kuna ajenda iliyokuwa inatakiwa kuondoa sifuri yaani mtahiniwa aliyepata sifuri asiwe na sifuri kidato cha nne awe na daraja V lakini pia mwaka 2013 ule ule itakumbukwa watu walio hitimu kidato cha nne mwaka huo walikuwa na pointi hadi 30 na hilo ni daraja la tatu na bado mwaka uliofuata mambo yalibadilika na kurejeshwa kama ilivyokuwa awali.

Bado haikuishia hapo mwaka 2015 wale waliohitimu kidato sita vyeti vyao havikuwekwa katika madaraja bali katika Mfumo wa Wastani wa alama za ufaulu GPA yaani (Grade Points Average) na mwaka uliofuata wakabadilisha. Huu ni uthibitisho kuwa elimu imekuwa ya kuchezea na hii ni kutokana na kutokuwekewa takwa la katiba linaloweza kuwaongoza viongozi wakajikita katika kuleta matokeo chanya kama elimu kuzingatia ajira na kujiajiri na si kujaribu kila mmoja anavyotaka katika kipindi chake hii ni hatari sana kwa taifa. Katiba nzuri itaiweka elimu katika mikono salama na yenye manufaa.

Katika teknolojia bado tunahitaji kuweka namna nzuri ya kikatiba katika kuweza kuweka mlengo mzuri wa kuweza kukabili teknolojia, mfano namna ya kuweza kupambana na athari zake, namna ya kuweza kuendeleza, namna ya kuweza kuileta katika taifa, kuikuza n.k. Hii itaweza kulisaidia taifa kujipanua kimaendeleo. Lakini pia namna ya kuitumia.

Mfano, tuchukulie hivi karibuni tozo za miamala ya simu, bado tunaona kuwa kutokana na katiba ya sasa ndiyo maana hata viongozi wanashindwa kupata mwongozo wa kuweka vizuri ni vipi waanze na tathmini nzuri (projection) hapa tunaona wabunge wakipitisha hata vitu vinavyohitaji muda mrefu na vinahitaji utafiti kwa muda mfupi tu na bila kujali athari zake na hata maslahi ya wananchi wao.

Tunaona kwa mfano mataifa ya wenzetu, wao wanao uwezo wa kukaa na kuweza kujadili jambo vizuri bila kutaka kumfurahisha kiongozi wa juu bali kwa umakini mkubwa na hatma njema kufikiwa lakini inaonekana sisi bila katiba hatuwezi kufanya hivyo. Mfano mzuri ni kuangalia wenzetu wa ulaya wameweka makubaliano mazuri na wakazingatia muda kwamba ifikapo mwaka 2030 wataanza kutokupokea magari yanayotumia mafuta. Hapo wametoa nafasi ya kuchunguza kwa kina na kujitayarisha kwa walaji na wauzaji na watengenezaji wa bidhaa hizo, tofauti na sisi ambapo tunakumbwa na athari kubwa kutokana na viongozi kukosa umakini hasa kutokana na kukosekana Kwa kitu ambacho kinaweza kuwaamsha hasa katiba nzuri.

Kwa hayo machache ni vyema kuukumbusha, umma, serikali na vyombo vyote vyenye kuhitaji kuiweka nchi katika hali nzuri vikiwemo vyama si vyama pinzani pekee bali hata chama tawala kuweza kuangalia namna ya kujenga nchi kupitia katiba na hii itavifanya vyama vyote kuweza kupitia katika mlango huo mzuri wa katiba na maendeleo ya umma pasipo kutegemea huyu anasema nini na anataka nini kwa wakati huu bila kujali athari za baadae hivyo, ni vyema kuweza kutilia maani suala hili na si nguvu ya vyama vya siasa bali ni jambo la nguvu ya wananchi raia wote wa Tanzania wakiwemo rais, wamaziri, wabunge na viongozi wote wa serikali.

Suala hili si kwa ajili ya kujipatia kiti au kukuondolea kiti bali kiti kitatokana na siasa yako nzuri na ushawishi mzuri kwa watanzania na hii ni kwa wanasiasa pekee ambao wanathamini madaraka kuliko kuthamini nchi wananchi pamoja na mali zao na taifa lao.

Mambo mengi yanahitaji katiba kama falsafa ya nchi, maendeleo kwa ujumla amani na ulinzi wa taifa.
 
Upvote 3
Back
Top Bottom