Kuujenga upya Al-Kaabah
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wasallam) alikuwa na umri wa miaka thelathini na tano wakati Makureshi walipoujenga upya Msikiti wa Al-Kaabah, kwa sababu miaka mingi ilikwishapita tokea Nabii Ismaaiyl alipoujenga na hapakuwa na kilichobaki katika jengo hilo isipokuwa rundu la udongo lenye urefu wa kiasi cha dhiraa sita, bila ya kipaa, jambo lililowarahisishia wezi kuingia ndani na kuiba hazina zinazowekwa humo.
Na kwa vile miaka mingi ilikwishapita tokea kujengwa kwake, kanuni za maumbile zilikwishafanya kazi yake. Kuta zilikuwa na nyufa, na miaka mitano kabla ya kupewa utume (Swalla Llaahu alayhi wasallam) yalitokea mafuriko makubwa yaliyosababisha maji kuingia ndani ya Msikiti na kubomoa sehemu kubwa za Msikiti huo, na kwa ajili ya yote hayo Makureshi wakaamua kuujenga tena Msikiti huo.
Wakakubaliana kuwa zisiingizwe katika ujenzi wa jengo hilo pesa zozote za haramu. Zisiingizwe pesa za mahari ya mzinzi, wala pesa za riba, wala pesa alizodhulumiwa mtu n.k.
Walikuwa wakiogopa kuubomoa Msikiti na kuanza kuujenga upya wasije wakadhurika, mpaka alipotangulia Al Walid bin Mughiyrah na kuianza yeye kazi hiyo, na wenzake walipoona kuwa hapana kilichomsibu, ndipo nao wakaingia kazini. Wakawa wanaendelea kuubomoa mpaka walipozifikia nguzo zilizosimamishwa na Nabii Ibraahiym (Alayhis salaam), kisha wakaanza kuujenga upya Msikiti huo, na kila kabila likapewa sehemu yake ya kujenga, na kila kabila lilikuwa likikusanya mawe yake ya ujenzi, na msimamiaji wa ujenzi alikuwa Mrumi aitwae Baqum.
Kazi ilikwenda vizuri mpaka ulipofika wakati wa kulirudisha jiwe jeusi mahali pake, ndipo mzozo ulipoanza kila kabila likataka kupewa heshima hiyo ya kulirudisha mahali pake.
Mgogoro uliendelea muda wa siku nne au tano na mambo yakawa magumu hata watu wakakaribia kutaka kupigana vita, panga mkononi mpaka pale Abu Umayyah bin Mughiyra Al Makhzumiy alipotoa rai kuwa; wa mwanzo kuingia Msikitini kupitia mlangoni ndiye atakayeamua baina yao, na wote wakaridhika na rai hiyo.
Mwenyezi Mungu akataka Mtume wake (Swalla Llaahu alayhi wasallam)) awe mtu huyo, na walipomuona tu akiingia, wote kwa pamoja wakapiga ukelele wa kuridhika:
"Huyu Muaminifu! Sote tumeridhika naye, huyu Muhammad."
Alipojulishwa juu ya uamuzi huo, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wasallam) (hii ilikuwa kabla ya kupewa utume) alikubali, na kwa utulivu akaomba kiletwe kitambaa, akakitandaza na kuliweka jiwe jeusi juu yake, kisha akawataka viongozi wa makabila yote kila mmoja akamate upande wa kitambaa, kisha wanyanyuwe kwa pamoja. Wakalinyanyua na walipopafikia mahali pa kuliweka, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wasallam)) akalinyanyua yeye kwa mikono yake miwili na kulirudisha mahali pake.
Kwa njia hii Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wasallam) aliweza kulitatua tatizo lililokaribia kuleta umwagaji wa damu mkubwa baina ya Makabila ya Kikureshi, na kila mmoja aliondoka hapo akiwa ameridhika.
Wanaishiwa na pesa za halali
Makureshi walishindwa kuukamilisha Msikiti baada ya kuishiwa na pesa za halali, wakaamua kupunguza kiasi cha dhiraa sita upande wa kaskazini mwa Al-Kaabah na hii ni ile sehemu inayojulikana kwa jina la Al Hijr (Hijr Ismaaiyl) wakashindwa kuunganisha Msikiti pamoja na Hijri Ismaaiyl ambayo asili yake ilikuwa imekamatana na Msikiti. Wakaunyanyua mlango kiasi cha dhiraa mbili kutoka juu ya ardhi asiweze kuingia isipokuwa wanayemtaka wao tu, na urefu wa jengo ulipotimia kiasi cha dhiraa kumi na tano wakaezeka sakafu juu ya nguzo sita, na baada ya kumalizika kazi hiyo, Al-Kaabah ikawa na umbo la mraba lenye urefu wa mita kumi na tano, na upande wa jiwe jeusi pamoja na upande wa pili yake (mkabala wake) pande zote mbili kila moja ilikuwa na urefu wa mita kumi.
Na jiwe jeusi liliwekwa juu kiasi cha urefu wa mita unusu kutoka juu ya ardhi, na upande wa mlango na upande wa mkabala wake ukawa na urefu wa mita kumi kila upande, na mlango ukanyanyuliwa kiasi cha mita mbili kutoka juu ya ardhi, na upande wa nje ya Al-Kaabah ikaachwa ikiwa imezungukwa na msingi ulionyanyuka kutoka juu ya ardhi kiasi cha robo mita na upana wa kiasi cha nusu mita.
Na sehemu hii ilikuwa ikiitwa Ash Shadherwan, sehemu ambayo asili yake ilikuwa ndani ya jengo la Al-Kaabah, lakini Makureshi iliwabidi waiache sehemu hii bila kuijenga, na kwa ajili hiyo Msikiti ukawa na umbo la mraba badala ya umbo lake la asili lililofanana na herufi D iwapo utaunganishwa na Hijr kama ulivyojengwa na Nabii Ibraahiym (Alayhis salaam).