Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,984
- 13,760
Mawaziri wa Afya wa nchi 5 ikiwemo Tanzania, Rwanda, Sierra Leon, Ethiopia na Jamhuri ya Afrika ya Kati wamekutana na kuweka mkakati wa kutoa mafunzo rasmi angalau ya mwaka mmoja, hatimaye kuajiri Wahudumu wa afya ngazi ya jamii kwa ajili ya kuimarisha Huduma za Afya ya Msingi.
Haya yamejadiliwa jana kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Mawaziri wa Afya wa Afrika unaofanyika Jijini Kigali-Rwanda, ambapo wanajadili mifumo endelevu na stahimilivu ya uimarishaji wa huduma za afya ikiwemo masuala ya kuwatumia Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii.
Mkutano huu umeandaliwa na Taasisi ya Susan Thompson Buffet Foundation (STBF).
Wahudumu hao watatekeleza afua jumuishi ngazi ya jamii ikiwemo huduma za afya ya mama na mtoto, afua za lishe na afua za tahadhari na kinga dhidi ya magonjwa ya mlipuko. Vilevile nchi wanufaika zitatumia mifumo ya ulipaji fedha Serikalini katika utekelezaji wa mpango huo sambamba na kuweka utaratibu wa kuwawezesha Wahudumu hawa kujiendeleza kitaaluma (career development systems).
Akizingumza katika Mkutano huo Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kuwa Serikali ya Tanzania tayari inayo Muundo wa Utumishi (Scheme of Service) unaoitambua kada hiyo katika kutekeleza majukumu yao kama Wasaidizi wa Afya (Health Assistants) ngazi ya vituo vya kutolea huduma za afya na katika ngazi ya jamii
“Tanzania ina uzoefu wa kuendesha mafunzo ya mwaka mmoja kwa kada rasmi ya wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii ambapo zaidi ya Wahudumu 9,800 walihitimu mafunzo hayo kwa mwaka 2017 hadi 2019”.
Waziri Ummy ameongeza kuwa Wizara yake itajikita katika kutekeleza Mpango huo kwa kuwajengea uwezo na kuwaajiri Wahudumu 15,000 kwa kipindi cha miaka mitatu yaani mwaka 2023/24 hadi 2025/26 ambapo kwa kuanzia Wahudumu wapatao 5,000 watapewa mafunzo kupitia Vyuo vya Afya vya kati kwa mwaka wa fedha 2023/24.
“Wahudumu hawa watatekeleza afua jumuishi ikiwemo Afya ya Mama na Mtoto, Lishe, Magonjwa Yasiyoambukiza, Magonjwa ya Mlipuko na Magonjwa Yanayoambukiza (VVU/UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria), Amesema Waziri Ummy.
Chanzo: WAF-Rwanda