Fumo Liyongo
New Member
- Sep 12, 2021
- 4
- 5
[CHANZO: Pinterest]
Wasifu wa mhenga wa kigeni
Kabla hawajazaliwa wazee wa wazee wetu, katika shamba moja mbali sana kutoka kijijini kwetu, alizaliwa mtoto. Kabla hujaweka maneno katika aya zangu, huyu si yule mtoto wa vitabuni, aliyezaliwa katika zizi la ng’ombe na kuletewa zawadi nyingi na wanajimu. Hata hivyo, huyu mtoto naye alikuwa ni wa kiume. Mama yake hakujua kuzisoma wala kuziandika herufi na baba yake alikuwa ni kibarua, aliyefanya kazi yoyote ile kwa kadiri njaa ilivyomuamuru.
Familia ya mtoto iliishi porini, maisha ya kijijini yalikuwa ghali mno kwao. Waliishi katika kibanda cha miti. Kibanda hakikuwa na sakafu, milango wala madirisha. Pande tatu za kibanda chao zilifunikwa kwa vipande vya miti na upande wa nne ulikuwa wazi. Pepo na baridi vilikuwa na ridhaa kuingia kibandani kadri vilivyotaka na kuwaadhibu wakaazi yaani mtoto na familia yake.
Japo mtoto hakuishi katika zama za binadamu wa kale tunaowafahamu katika somo la historia, lakini familia yake haikuwa na maziwa, matunda, magimbi wala mbogamboga. Waliishi kwa kula mawindo ya mwituni na vyakula jamii ya njugu.
Siku moja, mamaye mtoto alipatwa na maradhi. Mwili ulikuwa dhaifu. Mikono na miguu yake ilikuwa ya baridi mno ila mama alihisi kama viungo vyake vya ndani viliwaka moto. Nguvu zilimuishia, hakuweza hata kunyanyua kichwa juu ya mto na sauti yake ilififia. “Pendaneni wanangu, ishini vizuri kama nilivyowafundisha na muabuduni Mungu.” Haya ndiyo yalikuwa maneno ya mwisho ya mama kwa mtoto na mdogo wa kike wa mtoto.
Siku tisa baada ya maradhi kumpata na miaka tisa tangu mtoto alipozaliwa, mama alifariki. Familia haikuwa na majirani huko mwituni. Ilimbidi baba wa familia kufungasha mbao na vipande vya miti kutengeneza jeneza. Kwa hisani ya punda wawili, baba alibeba jeneza la mama wa mtoto na kulipeleka juu ya kilima mbali kidogo na makazi yao. Akiwa peke yake, baba alichimba kaburi na kumpumzisha mkewe. Hakukuwa na matanga wala ibada ya mazishi.
Wakati haukuganda, miaka ilisonga mbele. Akiwa na umri wa miaka kumi na tano, mtoto alianza kuzijua herufi za alfabeti. Aliweza kusoma kidogo lakini kwa shida sana. Hakuweza kuandika kabisa. Akiwa na umri huo, mwalimu aliyekuwa akizunguka zaunguka alianzisha shule takribani maili nne kutoka shambani alikoishi mtoto. Ilimbidi mtoto pamoja na mdogo wake wa kike kutembea kupita kati ya misitu na vichaka kwenda na kurudi kutoka shule. Naomba usifikirie hizi shule tuzijuazo, shule aliyosoma mtoto kimsingi lilikuwa ni banda la miti lisilo na madirisha. Madawati yalitengenezwa kwa vipande vya magogo.
Nyakati hizo, karatasi zilikuwa ghali na adimu. Hivyo, mtoto aliandika kwa mkaa katika vibao vya kibanda alichokiita ‘nyumbani’. Vibao vilipojaa maandishi na michoro, mtoto alikwangua kwa kisu na kuanza upya zoezi lake la kuusaka umahiri katika stadi ya mawasiliano ya kuandika.
Hata hivyo, shule ilikuwa ya msimu kulingana na ujio na kuondoka kwa hawa walimu wa msimu waliokuwa wakiranda-randa huku na huku. Miaka mitano baadae, jitihada zake za shule zilifikia ukomo na hakurudi shule tena. Ndani ya miaka yote hiyo, siku mtoto alizosoma shule hazikuzidi miezi kumi na miwili. Miaka mingi baadaye, mbele ya waliostaarabika, upo wakati mtoto akiwa mtu mzima aliulizwa ana elimu gani. “Yenye hitlafu.” Hilo ndilo lilikuwa jibu lake.
Ningependa kuyasema mengi zaidi, yaliyomuhusu huyu mtoto. Ila kwa kuthamini ufinyu wa muda wako, na wingi wa majukumu uliyonayo, niruhusu niishie hapa. Hii ni sehemu ndogo tu ya maisha duni na ya dhiki ya huyu mtoto. Kuna wakati nilipokuwa nikisoma wasifu wa huyu mtoto nilifikiri ni hadithi ya kutunga. Bahati mbaya sana, haikuwa hadithi. Yalikuwa ni maisha halisi ya mojawapo wa viongozi bora na wenye sifa njema waliowahi kuhudumu juu ya uso wa nchi. Abraham Lincoln, Rais wa kumi na sita wa taifa la Marekani.
Ndugu Lincoln aliliongoza taifa lake katika mojawapo ya vipindi vigumu sana katika historia ya taifa hilo. Taifa lilikuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Majimbo ya kusini yalipambana dhidi ya majimbo ya kaskazini ya Marekani. Chini ya huduma ya Lincoln katika uongozi, vita viliisha taifa likiwa limeunganishwa kuwa kitu kimoja. Watu weusi waliokuwa watumwa waliachiwa huru katika majimbo yote na Marekani ilianza safari rasmi kuwa taifa lenye nguvu duniani kama tunavyolijua leo.
Kile walichoota wahenga wazawa
Karne mbili zimepita tangu alipozaliwa Lincoln, nami natumia fursa hii kumuandikia machache kijana wa kiafrika. Leo hatutawalaumu viongozi wetu kwa masuala ya rushwa, ufisadi, ukosefu wa ajira na umasikini wa watu wetu. Leo hatutawalaumu wazazi wetu kwa kushindwa kutuandalia mtandao mzuri wa watu wanaofahamiana nao yaani ‘connection’ ili tufanikiwe kama watoto wa wenye nacho, tuliozoea kuwaita ‘wa kishua’. Leo hatutaulaani na kuutukana mfumo wa elimu kwa ubovu na udhaifu wake wa kushindwa kutuandaa kukabiliana na uhalisia wa maisha bila kuajiriwa.
Leo hatutawalaani mabeberu kwa ukoloni mamboleo na namna wanavyonyonya rasilimali za bara letu kujinufaisha wenyewe. Leo, hatutajilaumu wenyewe kwa uzembe wetu wa kufikiri, kujifunza na kushindwa kujituma. Hatutajilaumu kwa fursa tulizoacha zipite na pia hatutojilaumu kwa kuwaangusha wazazi na jamii yetu, waliowekeza kwetu lakini hatuna mwelekeo wowote wa kuwafanya waone fahari juu yetu. Leo hatutolaumu. Hatujilaumu sisi wenyewe, hatumlaumu Mungu, hatumlaumu yeyote wala chochote.
Badala yake, leo tutautafakari upande wenye nuru na tumaini. Tukiwa vijana, watu wetu wanatutegemea. Kama Mwalimu Nyerere alivyowahi kusema, jamii imechukua chakula chote kilichosalia katika ukame huu wa umasikini. Imetupa sisi hicho chakula kama vijana twende nchi ya mbali ili tuwaletee watu wetu chakula na kuwaokoa katika njaa kali. Watu wetu wanataraji kuyaona mabadiliko kupitia sisi.
Najua kila mmoja ana hadithi yake binafsi, na ninakiri, baadhi ya wenzetu wana hadithi zisizo na tumaini wala nuru hata kidogo. Lakini katika giza hilohilo, nina shauku kuwa mwanzo huu duni tuliouona wa ndugu Lincoln umpe moyo yule kati yetu aliyekata tamaa na kujiona hafai. Yule anayejiona si kitu kwa kuwa alifeli shule, yule anayeona elimu yake si kitu kwa kuwa hana ajira, yule binti anayedhani hawezi kuleta chochote kwenye meza iliyojaa wanaume, yule kijana mlemavu anayejiona mzigo na tatizo kwa familia yake, yule ambaye hata kumudu maisha yake binafsi ni jinamizi na suluba. Simulizi hii ya kweli ya Ndugu Lincoln, moja ya viongozi bora, si tu huko marekani lakini mfano bora kwa ulimwengu mzima, iachilie tumaini ndani yetu sote, vijana wa Afrika.
Bado hatujachelewa, tunayo nafasi. Na hii safari, tunazo nguvu za kuisafiri. Robin Sharma, mwandishi mashuhuri wa vitabu kutoka Kanada katika kitabu chake, ‘Kiongozi ambaye hakuwa na cheo’ anafundisha kwa kina namna mtu yeyote anaweza kufanya mambo kwa ufanisi na kuacha alama katika jamii hata kama hatokuwa na wadhifa wa kiuongozi. Naamini pia hili ni la msingi kwetu vijana wa Afrika. Hatutasubiri tuwe wabunge au mameneja wa makampuni ili kuacha alama na kuendeleza Afrika yetu. Kila mmoja awajibike kwa moyo, ustadi, ubora na ufanisi katika chochote afanyacho kwa ajili ya bara letu na watu wetu.
Wahenga wa kiafrika walisema, “Ukitaka kwenda haraka nenda peke yako ila ukitaka kwenda mbali, sharti uende pamoja na wenzako.” Naamini hekima hizi za wahenga zatufaa sana vijana wa sasa wa kiafrika. Bara letu lina changamoto nyingi na ni vigumu mtu mmoja kuzitatua peke yake. Lazima tushikane mikono na kuzikabili kwa umoja. Huu sio wakati wa kubaguana kwa itikadi, elimu, imani, jinsia, makabila wala chochote kinayofanana na hayo. Kila mmoja amuone mwenzake kama ndugu, mshirika na rafiki. Tuinuane, tujengane, tushirikiane, tusitupane, tusisemane, tusipingane. Sisi ni jamii, jamii ya Afrika.
Asante kwa kusoma.
Tafadhali naomba usiache kupiga kura kwa kubonyeza alama hii ...^… hapo chini.
Kura yako moja ni muhimu sana.
Natanguliza shukrani!
Upvote
3