Shabiki huyo ni wa kijiji cha Sangamaganga tarafa ya Ifakara wilaya ya Kirombero mkoa wa Morogoro ambaye alikuwa akifatilia mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Simba na Yanga kwa njia ya TV akiwa na mashabiki wengine kwenye ‘kibanda umiza.’
Sports Extra imezungumza na ndugu ambaye alikuwa pamoja wakifuatilia mechi hiyo kwenye kibanda umiza, ndugu huyo alizngumza na Peter Andrew na kueleza tukio zima lilivyotokea.
“Siku ya mechi nilikuwa na ndugu yetu tumekaa nae, kabla ya mpira kuanza mwenzangu akawa anasema kwamba leo lazima tuwafunge Yanga badae mechi ikaendelea hadi kufika hatua ya penati, mimi naipenda Simba lakini yeye anapenda zaidi maana kila mtu ana namna yake ya kupenda kitu.”
“Zilipoanza kupigwa penati, Yanga wakakosa penati ya kwanza Simba wakafunga kwa hiyo furaha ikawa inazidi kuongezeka, ilipofika zamu ya Niyonzima kwenda kupiga penati shabiki mwingine wa Simba akasema huyu lazima akose, marehem akamwambia usiseme hivyo utatutia mkosi atakosa kweli.”
“Niyonzima akapiga penati akafunga, alivyofunga tukaona mwenzetu ametulia kwenye kiti, kuna dogo alikuwa amekaa nyuma yake akasema, jamani hyu jamaa amezimia watu wakasema achana nae ngoja tuendelee kuangalia penati itakuwa furaha imemzidi tu.”
“Wakati inapigwa penati ya mwisho ya mchezaji wa Yanga jamaa alikuwa tayari ameshazimia kwa hiyo hata penati ya mwisho ya Mohamed Hussein Tshabalala hakuiona, tunakuja kushtuka Tshabalala anakosa penati tnasikia jamaa anakoroma, tukamtoa nje tukaanza kumpepea tukachukua gari kumpeleka zahanati.”
“Tulipofika zahanati tukaambiwa tayari alishafariki, kumbe alishafariki palepale kwenye kibanda umiza lakini hakuna mtu aliyegundua.”
“Kabla ya mchezo marehem alikuwa vizuri kabisa mimi nilikuwa nae kuanzia mida ya saa nne akaenda kwenye mambo yake ya vikoba baadae akaja kwenye eneo la kuangalia mpira. Hali hiyo ilimtokea tu siku hiyo lakini kabla ya hapo hajawahi kukutwa na hali kama hiyo.”
Kwa hisani ya Shaffih Dauda