Neema, jina lililoimbwa zaidi Tanzania

Neema, jina lililoimbwa zaidi Tanzania

Makonyeza

Member
Joined
Feb 2, 2020
Posts
72
Reaction score
261
Wapenzi wa muziki wa Dansi wengi ukiwatajia jina la Neema kumbukumbu zao hurejea kwenye sauti ya Cosmas Chidumule akiwa na DDC bendi iliyomilikiiwa na Shirika la Maendele Dar es Dalaam (Dar es Salaam Development Corporation-DDC).

"Usipate taabuuu Neemaaaa,ukiyoyafanya siyo mageni hapa Dunianieeee..."

Hapa Chidumule alilalamika dhidi ya Neema kwa kile kitendo cha Neema kumzuia yeye Chidumule asikanyage nyumbani kwake wala kazini asimfuate na hata kusalimiana naye hataki tena,kisa? Eti yule bwana aliyezaa naye yupo.

" hata habari yako nimeipokea,
kwa mikono miwilioo,tena bila ya kinyongo moyoni mwangu Neeema..
Hata shemeji zako Kitimtim na Bure,niliwatuma waje wakupe Salam zangu,....,
ingawa roho iliuma mamaaa,uliponielezea,kwamba yule bwana uliyezaa naye yuuupoooooo....,
kwa hiyo nisije nyumbani kwako,
wala kazini nisikufuate,
hata kusalimiana na mimi hutaki,japo twafahamiana..."
Lakini kwa kuwa huyo jamaa anayeogopwa hajamuoa Neema,Chidumule anaahidi na kuapia kwenda nyumbani kwa wazazi wa Neema kupeleka barua ya uchumba achukue jumla jumla.
Ni bonge moja la wimbo wa viwango hasa kwa wanaojua nyimbo za Dance,hata sasa ukisikika sehemu yoyote utaona waungwana wanavyoenda nao beti baada ya beti.
Mbali na Chidumule na Ddc yake, sass kuna baadhi hasa wale vijana walioishuhudia bendi ya DIAMOND Sound,'wanakibindankoi'. Pale kuna mwamba aliitwa Eliston Angay faraoh na Allan Mulumba Kashama walitunga kibao kinaitwa Neema, yaani ilikiwa balaa mjini.

Unakumbuka beti hizi?

"Nashangaa na maneno yako,umekuwa kigeugeu,aaah Neema Oh,
ninapopendana na weweee,umenjtamkia mweyewe,nakupenda japo huna kitu,unaponipakaziaa,eti mimi sina kituuu,nasikitika Neema...

Chini tumelaaaaooooh,njaa tumeshindaaa..

"Neema kumbuka,kupata ni Majaliwa,
Mapenzi sio Mali wala kipato,
Penzi ni dhamana ya moyo wa mtu oooh.....milima nimepanda,mabonde nimetembea
Jamaa alikuwa anamkumbusha Neema ahadi aliyompa kumpenda kama alivyo, na anamsisitizia mapenzi sio mali bali ni dhamana ya moyo wa tu.
Wakati wimbo huu unasumbua mjini mimi nilikuwa kidato cha Tatu,na radio kubwa jijini ilikuwa ni Redio One Stereo, city Redio, External Service ilikuwepo Tabata huko(sijui iliipotelea wapi) na Redio Tanzania( RTD).
Basi kila mwenye jina la Neema alihisi ni yeye ndiye anaimbwa na Mulumba[emoji1787]

Sasa kwangu hao wote wawili ,yaani Ddc na Kibindankoi hawakumtendea haki stahili Neema,Neema kama kuimbwa ameimbwa na Bima Lee, chini ya Utunzi wake 'Super Motisha',Shaaban Dede Kamchape.
Hawa jamaa walipigilia msumali,walijua hasa kumlilia Neema.
Ilikuwa timu ya watu watatu wakipishanisha sauti zao, Dede mwenyewe alikamata sauti ya kwanza,Athuman Momba( Sauti ya Chuma),yeye aliivumisha sauti ya pili na ile sauti nzito inayogugumia nyuma ya hizo mbili ni ya Jerry Nashon (Dudumizi). Hawa wote kwa sasa ni marehemu,Mungu awapumzishe pahala pema.
Kama Neema hakuwaelewa Bima Lee chini yule mtindo wa Magneto Tingisha,basi hakuna anayeweza kumuimbia Neema akamuelewa. Huu wimbo uliimbwa kati ya mwaka 1984/1985,wakati huo mimi nikiwa kinda la miaka mitano tu.
Wimbo huu kwangu unaangukia katika tatu Bora yangu ya nyimbo Bora za Dance Tz,na Mtunzi wake kwangu kadharika yungali miongoni mwa watunzi watatu(3) Bora wa muziki wa Dance Tanzania. Orodha kamili nitaijata siku nyingine.
Ebu tazama mashairi yalivyopangwa kiutundu:

" Nimesimama chini ya Mnara wa Bismin,
Barabara kubwa ya Moro iendayo bandari ya salama,

Mawazo yamenijaa,machozi yanimwagika,
Naiwaza sura ya Neema,Naiwaza sura ya Malaika wangueee,

Nawaza jinsi penzi letu lilivyoyeyuuuka ,eti sababu ya ufukara na unahili nilionaoooo,
Umenikataa sababu mimi ni bahiri,mkono wangu haunyooki,eti ninamkono wa bilika mamaaaa.

Nitoe nitoe kizimbani,Neemaeee mtoto wa Songea, nitoe nitoe kizimbani ,niwe huru oooh niwe huruuu."
Huu wimbo ulitungwa ukigawanywa mafungu mawili, Baada ya fungu la awali la beti hizo katikati zinaingia ala za upepo zikiongozwa na Mafumu Bilali Mbombenga.

Fungu la pili la beti za wimbo huo linaendelea likiwa kama kiitikio,sauti zile tatu zinaendelea kurindima.

"Usiniache peeke Neema,
Nitasema na naani mamaaa,
Usifate wayasemayo wafitini, hao wako mbelembele kuharibu mapenzi yetu,mimi na weewe."

Anaingia Dudumizi na lisauti lake lenye kitetemo kama ndege yule aina ya Dudumizi, na hii ndio sababu ya yeye kuitwa jina la utani Dudumizi akipewa na marehemu 'Gwiji Chiriku Hemed Maneti Ulaya'.

"Maneno mengi sana nilishasema,usfuate ya wambea watakuja kutuvurugia,umeyaona sasa,yamekukuta Mpenzi,tumependana,bado tunapendana,Neema mamaaaa,

Ubeti wa kiitikio unajirudia..

"Usiniache peeke Neema,nitasema na nani Mamaa...."

Kisha analizia Momba na sauti ya iliyofananishwa na chuma ,jina ambalo pia alipewa na yule Chiriku Hemed Mabeti Ulaya kipindi wakiwa pamoja Pale Vijana Jazz.

" uliponambia adios amigooo,
ulipotamka adios amigoo,
Uliniacha peke,ninateseka mpenzi,sina mwingine Neema ooooh,fanya Himmaaaaaa..."

Rufia ubeti wa kiitikio...

Huu wimbo hauchoshi kuusikiliza hata kidogo.
Wapenzi na wadau wa muziki wa enzi Enzo hizo watakubaliana na mimi kwamba usajili na kiwango cha utendaji kazi cha kikosi cha Bima Lee enzi hizo Magnet Tingisha au Magnet 84 ilikuwa ni kama huu usajili wa Yanga hii inayosumbua Afrika leo.
Achana na wale waimbaji watatu niliokutajia Yaani Momba,Dede na Dudumizi,kwenye gitaa besi alikuwepo Selemani Mwanyiro,mnamnjua kazi zake,kulikuwepo na mwamba wakimuita bwana mipango Joseph Mulenga akiwa ndio kiongozi wa bendi. Solo ilikamatwa na Kassim Mponda De la Shanse.

Wengine siwakumbuki mtanisaidia.

Chukua na hii ya nyongeza:

Sasa kwa taarifa yako,pamoja na mapenzi na mahaba yangu yote kwa Sikinde ba Msondo,Bima Lee, Magnet 84 inabaki kuwa ndio bendi yangu Bora ya wakati wote na wimbo huu wa Neema ni moja ya sababu zangu nyingi za kuizawadia bendi hii ufalme mbele ya hao mapacha wawili Sikinde na Msondo.
Nimalizie kwa kusema,kuna Sikinde na Msondo wakitajwa kama alama za Muziki wa Tanzania ,lakini kwangu kuna Bima Lee Orchestra Magnet Tingisha(1984).

Kama unaujua Muziki wa Dance lakini!

Namimi nakuaga ADIOS AMIGOOO![emoji112]

"
 
Back
Top Bottom