Neno Hili Neno Gani?

Neno Hili Neno Gani?

Filipo Lubua

JF-Expert Member
Joined
Nov 18, 2011
Posts
339
Reaction score
578
NENO GANI?
Malenga nawaamsha, asubuhi na mapema
Ndoto imenigutusha, mimi sikulala jama
Malaika wa kutisha, ndotoni kanitutuma
Kanifumba fumbo gumu, sikweza kulitanzua

Kaniambia Lubua, hima unipe jawabu
Jibule sikulijua, nikalia kwa aibu
Nambyeni kama mwajua, neno moja ndo jawabu
Neno tata neno gani, laleta tabu dunyani

Malenga nifumbueni, mwenzenu raha sipati
Neno hili neno gani, lasababisha mauti
Neno hili litajeni, msipoteze wakati
Neno hili neno gani, liletalo tafurani

Neno la herufi saba, mtaani lasulubu
Limewatesa wababa, halijaacha mababu
Ya kale yake nasaba, watu wengi lawaadhibu
Neno hili neno gani, liletalo tafurani

Nilipokuwa mdogo, mamangu alinusia
Ni kali kama mbogo, watu wengi limeua
Limekuwa ni mtego, lanasa wasojijua
Neno hili neno gani, tegueni nifahamu

Bado mnajiuliza, tegueni tendawili
Ni hatari nawajuza, ili mwende kwa akili
Laleta mauzauza, si refu kama ukili
Neno hili neno gani, nambieni nifahamu

Silabi zake ni tatu, latesa hasa vijana
Rafiki yake ni chatu, ameza baba na wana
Msiseme kwa ubutu, fafanueni bayana
Neno hili neno gani, litujazalo majonzi

Rafikiye kisirani, nisemacho si uzushi
Atakweka majonzini, akumalize ubishi
Akutupe kaburini, uwe mwisho wa kuishi
Neno hili neno gani, tegueni mnijuvye

Hili neno la zamani, tangu enzi za wahenga
Kwa wivu limeshekheni, naweleza bila chenga
Lawatia wazimuni, laleta mengi matanga
Neno hili neno gani, tegweni kitendawili

Sielezei zaidi, wa busara tegueni
Mkisubiri zaidi, mwenzenu ntakufeni
Malaika kaniradidi, jibule ni shartini
Neno hili neno gani, kitendawili tegweni


© Filipo Lubua, 24 Novemba 2013
 
Asante sana Filipo, kwa mafundisho murua.
Tuzingatie tulipo, tusije tukapotea.
Uliyoyasema yapo, ukimwi balaa sana.
Neno lenyewe ukimwi, silabi zake ni tatu.





Nimetegua mtego, swali lako nimejibu.
Mimi pia ni kiboko, kiswahili lugha yangu.
Tusikilize maonyo, tusikie ya mkuu.
Neno lenyewe ukimwi, silabi zake ni tatu.
 
Asante sana Filipo, kwa mafundisho murua.
Tuzingatie tulipo, tusije tukapotea.
Uliyoyasema yapo, ukimwi balaa sana.
Neno lenyewe ukimwi, silabi zake ni tatu.

Nimetegua mtego, swali lako nimejibu.
Mimi pia ni kiboko, kiswahili lugha yangu.
Tusikilize maonyo, tusikie ya mkuu.
Neno lenyewe ukimwi, silabi zake ni tatu.

Agosti umejaribu, japo hukulipatia
Nasema hivyo sababu, vigezo hukufikia
Ukimwi hilo si jibu, japo umekaribia
Lisome tena shairi, uone vyote vigezo
 
Naja kujibu Filipo , usiseme nakosea
Ningoje hapo ulipo , mwezako nachechemea
Mwanzo suali lako , jibu linafuatia
Neno lenyewe MAPENZI,ndio ulokusudia

Neno hilo ni la zama , enzi za wazee wetu
Nasi limetutuama , limo vifuani mwetu
Twalitupia lawama , kumbe ni makosa yetu
Neno lenyewe MAPENZI , ndio ulokusudia

Nina mengi ya kunena , ila nahofia muda
Ingelikua mchana , isingekua na shida
Ila nitarudi tena , kuengeza tafsida
Neno lenyewe MAPENZI , ndio ulokusudia

Kukosea ni wajibu , kama sepata nambia
Usikae kama bubu , mji nitakupatia
Zawadi kwako wajibu , kama nimelipatia
Neno lenyewe MAPENZI , ndii ulokusudia
 
Naja kujibu Filipo , usiseme nakosea
Ningoje hapo ulipo , mwezako nachechemea
Mwanzo suali lako , jibu linafuatia
Neno lenyewe MAPENZI,ndio ulokusudia

Neno hilo ni la zama , enzi za wazee wetu
Nasi limetutuama , limo vifuani mwetu
Twalitupia lawama , kumbe ni makosa yetu
Neno lenyewe MAPENZI , ndio ulokusudia

Nina mengi ya kunena , ila nahofia muda
Ingelikua mchana , isingekua na shida
Ila nitarudi tena , kuengeza tafsida
Neno lenyewe MAPENZI , ndio ulokusudia

Kukosea ni wajibu , kama sepata nambia
Usikae kama bubu , mji nitakupatia
Zawadi kwako wajibu , kama nimelipatia
Neno lenyewe MAPENZI , ndii ulokusudia

Mahirtwahir umepatia, fumbo umelifumbua
Zawadi takupatia, jambo moja ukyelezea
Mapenzi kama halua, vipi yawe ya kuua?
Mbona mapenzi asali, yaweje tena ajali?
 
Mh, kiukweli nimefungua nikataka kujua nini kinasemwa.........Haya tena Nimetoka kapa
 
Mahirtwahir umepatia, fumbo umelifumbua
Zawadi takupatia, jambo moja ukyelezea
Mapenzi kama halua, vipi yawe ya kuua?
Mbona mapenzi asali, yaweje tena ajali?
Neno penzi wingi mapenzi lina maana papna sana:
Mtu anaweza kuwa na mapenzi kwa nchi yake,mwanawe,mzazi wake,kazi,pesa,mwanamke n.k

Lakini linapokuja penzi la mwanamume kwa mwanamke (au kinyume chake) likiambatana na huba,ladha,matamanio n.k kama ulivyoelezea katika shairi lako basi huitwa ASHIKI ! si penzi.

Na Kiislamu ashki ni maradhi katika maradhi mabaya ya moyo bali Quran inaitaja ashiki kuwa ni ulevi.

Mtu akipandwa na ashiki huwa kama vile mlevi wa pombe na kufanya mambo ya aibu au kama ulivyoelezea kwenye beti zako husababisha mauti,tafrani n.k kwa Mswahili yoyote yule ukizungumzia hivyo tu anajua kuwa hilo si penzi bali ni ashiki/ashki.
 
Sasa kuna swali la kulijibu, je ashiki ni jambo ambalo halizuiliki? yaani mwenye ashiki asilaumiwe kwa ayafanyayo kwa vile si yeye bali ni moyo, au ni jambo la kujitakia?

Yaani mathalani mwenye ashiki anaiba au kudhulumu kwa ajili ya kupata cha kumridhisha nyonda wake, tunamsamehe kwa vile si yeye bali ni moyo?

Jawabu lake ni hapana! hatumsamehi abadan!
Kwa sababu Quran inaiita ashiki kuwa ni ulevi basi mfano wake ni kama vile mtu aliyetoka nyumbani kwake akaenda baa, akanunua kilevi, akafungua, akanywa mpaka akalewa! mtu huyu hawezi kutuambia kuwa niliiba au nilidhulumu hali nikiwa katika ulevi hivyo nisameheni! hatumsamehi!

Vilevile kwa mwenye ashiki; ni yeye mwenyewe ndiye aliyemuangalia (mwanamke), akamleta mawazoni, akaleta picha kichwani jinsi itakavyokuwa akiwa naye, akaanza kufuatilia anaitwa nani, anaishi wapi, anafanya nini mpaka huba zikamganda na kushitadi moyoni na kuwa ulevi kamili wa ashiki! baadaye mtu huyu anakuja kuiba, kudhulumu au kuvunja undugu na ndugu zake kwa ajili ya (mwanamke) na kutupatia jawabu kuwa si mimi ni moyo hivyo tumsamehe!

Hapana hatumsamehi! tunamwambia kuwa wewe mwenyewe ndiye uliyejitakia kwa kumuangalia (pamoja na kwamba Quran inakataza), kumfikiria,kumfuatilia, kuwa pamoja naye na mengineyo.

*ningeelezea tiba ya maradhi ya ashiki kufuatana na Quran na Sunnah lakini si jukwaa husika hili.
 
Filipo narudi tena , kwani imenilazimu
Narudi bila hiyana , tena kwa jambo muhimu
Nitaliweka bayana , uweze kunifahamu
Kweli mapenzi asali , alosema hakuzua

Mapenzi kweli asali , alosema hakuzua
Penzi ni kitu asili , hadi leo twatumia
Katu hatukibadili , kwani tushakizoea
Mapenzi kama halua , pindi ukiyajulia

Mapenzi ya siku hizi , tofauti na zamani
Ya sasa yanahirizi , kama kitanzi shingoni
Wapendwao si wajuzi , na wana hila moyoni
Mapenzi kweli yauwa , wala hayana utani

Ajali kwenye mapenzi , hio ndio kawaida
Wapendwao ni washenzi , na hasa akina dada
Hawayajui mapenzi , kwao hayana faida
Wanajali maslahi , wajivishe midabwada
 
Back
Top Bottom