Huu ni usanii mwingine. Wanadai hawawezi kukaa kimya wakati vurugu zimeanza wiki nzima iliyopita na walikuwa hawajui la kuzungumza mara Kikwete kenda kumuona M7 mara hivi mara vile.
Nchi nyingi duniani zimetoa kauli zao kuhusiana na machafuko ya Kenya, sisi kama majirani tulinyamaza wiki nzima halafu leo wanadai hawawezi kukaa kimya!!! 😕
CCM, ni lini mtaacha usanii wenu!? Watanzania tumechoshwa na usanii usiokwisha.
Sunday, 06 January 2008
Chama cha Mapinduzi nchini Tanzania leo kimetoa kuhusu hali ya machafuko ya kisiasa yaliyotokea nchini Kenya baada ya Uchaguzi Mkuu wa Disemba 2007.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Jijini Dar-es-Saalam Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi Bw. John Chiligati alisema kwamba Chama cha Mapinduzi kimesikitishwa sana na umwagaji damu uliotokea nchini Kenya na machafuko ambayo yamekuwa yakiendelea kwa zaidi ya wiki sasa.
Bw. Chiligati alisema kuwa CCM haiwezi "kukaa kimya" wakati majirani zake wako katika hali mbaya ya kisiasa. Bw. Chiligati alisema kuwa wakati umefika kwa viongozi wa kisiasa nchini Kenya "wakae chini na kuzungumza" ili waweze kumaliza mgogoro huo kwa amani.
Bw. Chiligati alisema kuwa jinsi ambavyo viongozi wa kisiasa walivyoshughulikia mgogoro huu kwa kweli siyo "njia sawa". Zaidi ya yote, Bw. Chiligati alisema kuwa kwa vile Kenya ni sehemu ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki basi wananchi na viongozi wa Kenya wakumbuke kuwa matukio ya umwagaji damu yanatishia kwa kiasi kikubwa ujio wa shirikisho la Afrika ya Mashariki.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Tanzania Bw. Bernard Membe amezitaka jumuiya na wadau wote wa hali ya kisiasa nchini Kenya kumsaidia Rais Kibaki katika kutafuta suluhisho la amani nchini humo. Bw. Membe alisema kuwa ipo haja ya kuchunguza kwa kina yote yaliyosababisha uchafukaji wa kisisiasa nchini humo na mwelekeo wa kulaumu "upande mmoja" haumsaidii Rais Kibaki ambaye anajaribu kutafuta usuluhishi.
Pia, Bw. Membe alisema kuwa Rais Kibaki azungumze na viongozi wengine wote ili kuweza kutafuta muafaka unaokubalika. Kwa kauli yake hiyo mapema leo, hii inakuwa ni mara ya kwanza kwa serikali ya Tanzania kumtambua Bw. Mwai Kibaki kuwa Rais wa Kenya.