SoC02 Ngazi iliyoachwa na vijana

SoC02 Ngazi iliyoachwa na vijana

Stories of Change - 2022 Competition
Joined
Aug 17, 2022
Posts
10
Reaction score
2
Ngazi ni kifaa muhimu kinacho msaidia mtu kupanda na kufikia mahali anapohitaji. Mtu anaweza kutumia kupanda kuelekea juu au kushuka chini, ngazi hutumika sana wakati wa ujenzi, kama vile nyumba, visima au kupanda kufikia kitu fulani kilicho mbali.

UTOAJI unaweza kusimama au kuwakilisha ngazi katika kufikia mafanikio iwapo mtu ataelewa namna ya kuitumia ngazi hiyo.

Watu wengi hasa kundi la vijana wameiacha ngazi hii na kuanza kupambana wenyewe bila msaada wowote. Wameshindwa kujichanganya na watu wengine wa rika zote, hali zote za kiuchumi na kujiangalia wao wenyewe, wakiamini juu ya nguvu zao wenyewe, kimawazo hata kiutendaji. Lakini pia wameacha kanuni muhimu sana inayoitwa (UTOAJI).

UTOAJI ndiyo ngazi inayoweza kujikita katika nyanja nyingi kama vile:- utoaji wa mawazo chanya kwa watu wengine, utoaji wa misaada kama vile pesa na vitu. Na mengineyo yanayohusu kusaidia. Siku zote hakuna kitu kinachoenda bure na kanuni ya kupokea ni kutoa.

Tujifunze katika asili tulizonazo kama vile MITO. Mto siku zote hulazimika kutoa maji yake ili iweze kupokea mengine mapya kutoka katika mito mingine kwa sababu ikiacha kutoa haitakuwa na sehem ya kuhifadhi maji mengine na hiyo itapelekea kuacha kupokea maji tena.

Tujifunze kutoa ili nasisi tupokee, kijana unapomsaidia mtu mwingine ipo siku utasaidiwa pia hata kama sio na mtu yule yule uliyemsaidia bali hata na mtu mwingine, watu wataona fadhila na mchango wako kwao hivyo watapata wepesi wa kukufikiria wewe pia hata katika nyakati za shida au kukosa.

Kutoa pia hujenga mahusiano baina ya mtu na mtu. Unapotoa unajiwekea hazina ambayo itakusaidia baadae.

Katika biashara wanahitajika watu(wateja) ili kununua bidhaa zako, katika maswala yote ya jamii wanahitajika watu watakao husika maana kila jambo linahitaji watu, na ili kuwapata watu yanahitajika mahusiano mazuri ili kuwafikia kwa urahisi.

Kijana unapopata fursa jitahidi kutegemeza na wengine. Kama ni biashara ukifaulu jitahidi kuwapa njia na wengine ili na wao wafikie malengo yao, maana hakuna anayejua kesho yake itakuwaje. Katika kila jambo kuna kupanda na kushuka, hivyo tengeneza fursa na mazingira ambayo yatakusaidia kuinuka tena siku utakayoanguka, inawezekana wale uliowashika mkono wakakushika nawewe siku ya kuanguka kwako au yeyote aliyeona jitihada zako wakati wa mafanikio yako kama wote hawataona basi yuko Mungu aonaye kila hatua atakutumia watu wa kukusaidia.

Mafanikio yanaweza kuletwa kwako na watu wengine waliofanikiwa mbele yako au na watu ambao hawajafanikiwa walio chini yako. Maana kila mtu humtegemea mwingine kimawazo na hata katika utendaji. Mfano biashara itahitaji wateja ambao ni watu wa vipato tofauti tofauti. Yote ni katika kupambania kutimiza malengo.

Haimaanishi kila unapotoa lazima upokee au kila unapotoa unawekeza bali unapaswa kutoa au kusaidia kwa hiari kwa moyo wa kupenda, ukiwa na shauku ya kuona mwingine akifanikiwa pia kuepuka unyonyaji wa aina yoyote ile, unapaswa kutenda haki kwa kila mtu anayejua sheria husika na asiyejua, huku ukiwa mwaminifu hata katika madogo maana hiyo ni kanuni ya kuongeza na kukuza mahusiano baina yako na watu wengine.

Kila aliyefanikiwa kuna sehemu alisaidiwa maana hata wateja wanaokuja kwenye biashara au kazi yoyote hao wanakusaidia kufikia malengo yako hivyo ni vyema kumheshimu kila mtu na kumpa nafasi yake stahiki bila upendeleo wala uvunjwaji haki wa aina yoyote ile.

Mto hupokea maji na kutoa bila upendeleo nasi tutoe kwa haki maana kila tunapotoa kupokea ni kanuni ya asili, lakini kama tutapokea pasipo kutoa basi huko ni kujilimbikizia mali na mwisho hatutakuwa na msaada kutoka nje kwasababu ya kukosa mahusiano na watu wengine.

Tengeneza mahusiano bora kwa tabia ya utoaji ili yakusaidie kukua na kufikia malengo yako. Tunaowatumikia ndio watakao tuinua. TENGENEZA NGAZI IMARA KWA KUHUSIANA VYEMA NA WATU.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom