Amani Girls Organization
Member
- Feb 17, 2024
- 8
- 2
Wasichana balehe (wenye umri kati ya miaka 10-19) wakiwa katika mafunzo juu ya madhara ya Ndoa za Utotoni
Ndoa za utotoni ni tatizo sugu nchini Tanzania na zinaathiri zaidi wasichana: asilimia 92.5 ya ndoa zote za watoto zilizoripotiwa ni za wasichana. Kwa mujibu wa kiashiria cha magoli endelevu ya dunia (SDG), mikoa minne - Mara, Morogoro, Shinyanga na Simiyu - inaripoti viwango vya ndoa za wasichana kuwa juu ya asilimia 30. Katika ngazi ya kitaifa, asilimia 19 ya watu wanaamini ni sawa kwa msichana kuolewa kabla ya kufikisha miaka 18, huku asilimia 6 tu ya watu wanaamini hivyo kwa wavulana wa umri huo huo. Katika mazingira ambapo rasilimali ni chache, mahari ya bibi harusi inaonekana kama njia ya kupunguza mzigo wa kiuchumi wa familia.
Katika kijiji cha Twa Twa Twa, kilichopo Kata ya Parakuyo, Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro, wasichana wengi wanalazimishwa kuolewa wakiwa na umri mdogo na wazazi wao. Wazazi wanaamini kuwa hii itazuia wasichana hao kuleta aibu kwa familia na ukoo wao kwa kupata mimba kabla ya ndoa. Hivyo, wasichana hawa wanalazimishwa kuolewa. Ikiwa watakataa, mara nyingi watapigwa, kuchapwa viboko na kaka zao.
Katika kijiji hiki, kuna shule chache za msingi na sekondari ambazo zinakabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa na walimu. Ingawa umuhimu wa elimu unasisitizwa, bado rasilimali zinabaki kuwa chache. Wasichana wengi wanaahidiwa kuolewa wakiwa bado shuleni, jambo ambalo linawavunja moyo kuendelea na masomo yao. Bado kuna wanaume wanapeleka mahari kwa wazazi wa hawa wasichana ambao bado wapo shuleni (katika shule za msingi na sekondari).
Wakati Amani Girls Organization (AGO) ilipotembelea makundi haya ya wasichana balehe, wasichana hawa waliomba elimu juu ya athari mbaya za ndoa za utotoni pia itolewe kwa wazazi wao. Wasichana hawa bado wanaishi chini ya uangalizi wa wazazi wao, ambao pia ndio watoa maamuzi ya mwisho. Katika jamii hizi, ni changamoto kwa watoto kuzungumza na wazazi wao na kuwashawishi kuacha desturi ya ndoa za utotoni.
"Tunataka wazazi wetu wazielewe ndoto zetu na kutusaidia kuzifikia, sio kuziharibu kwa ndoa za utotoni. Wakati wazazi wetu wanapofahamu hatari za ndoa za utotoni, wanakuwa washirika wetu wakubwa katika kupambana nazo," alisema msichana balehe kutoka katika kijiji cha Twa Twa Twa.
Jamii ya Twa Twa Twa inajishughulisha zaidi na ufugaji wa ng'ombe na kuuza maziwa ili kupata kipato. Familia hizi hupokea mahari kwa njia ya mifugo (ng'ombe) na kuthamini mifugo zaidi kuliko maendeleo binafsi ya binti zao. Wanajivunia zaidi idadi ya mifugo waliyonayo kuliko kuona binti zao wakipata elimu, kujiendeleza, na kupata ajira zitakazowapa kipato.
Upendeleo huu wa mifugo juu ya elimu unadumisha mzunguko wa umaskini na kupunguza fursa kwa wasichana wadogo, ambao mara nyingi wanaolewa wakiwa na umri mdogo. Bila elimu, wasichana hawa hawawezi kufikia ndoto zao, na kuwa na mchango katika jamii ambazo desturi za jadi zinapata nafasi kubwa kuliko umuhimu wa ukuaji binafsi na maendeleo ya kiuchumi. Ili kuvunja mzunguko huu, ni muhimu kukuza thamani ya elimu na kuwawezesha familia kuona faida za muda mrefu za kuwekeza katika mustakabali wa binti zao.
Amani Girls Organization (AGO), kwa sasa inatekeleza mradi wa Hapana Marefu Yasio na Mwisho, mradi wa miaka 3 unaolenga kutokomeza ndoa za utotoni nchini Tanzania. Ukiongozwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (ELCT), mradi huu unashirikiana na C-Sema, shirika linaloendesha huduma ya simu kwa watoto #116, likiwa na lengo la kuendeleza haki za wasichana na kupinga mila na desturi zenye madhara kwa jamii.
Reference: OECD (2022), SIGI Country Report for Tanzania, Social Institutions and Gender Index, OECD Publishing, Paris, SIGI Country Report for Tanzania.