size=3]
Kundi la watu zaidi ya 15 wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wakiwa na silaha za kivita, wamevamia basi moja la abiria kulilipua kwa mabomu na kuua watu wawili papo hapo. Tukio hilo ambalo ni la ajabu kutokea hapa kwetu Bongo, limetokea huko mkoani Kagera na kuzua hofu kubwa kwa wananchi. Akizungumza na Alasiri kwa njia ya simu leo asubuhi, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Abdallah Msika amesema tukio hilo lilitokea jana saa 8:30 mchana katika pori la Kimisi lililo kati ya wilaya ya Karagwe na Ngara.
Amesema basi hilo lenye namba za usajili T 915 ANA aina ya Hino lililokuwa likitokea wilayani Karagwe kwenda Ngara, lilikuwa na abiria kati ya 30 na 35 huku likiendeshwa na Bw. Mwesiga Joseph. Akisimulia tukio hilo, Kamanda Msika amesema basi hilo lilipofika kwenye pori la Kimisi kwenye kona iitwayo Mnyonge ndipo walipojitokeza majambazi hao na kuanza kulishambulia kwa risasi.
Akasema hata hivyo askari polisi wawili waliokuwa wakisindikiza basi hilo, waliamua kujibu mashambulizi na kusimama kidete kutetea kazi yao. Akasema mapambano ya kurushiana risasi baina ya majambazi na askari hao, yalikuwa makali na majambazi yalipoona yamezidiwa nguvu, ndipo yakabadili silaha na kurusha mabomu ya mkono.
Kamanda amesema baada ya kurushwa kwa mabomu hayo, majambazi yaliwazidi nguvu Polisi na kufanikiwa kuingia ndani ya basi hilo na kuanza kupora abiria. Amesema yalipoingia ndani ya basi, yalimuona askari mmoja aliyekuwa amevalia sare, yakampiga risasi na kumuua papo hapo. Kamanda Msika amemtaja askari huyo kuwa ni mwenye namba MG 413657 Obadia Didas aliyekuwa akitokea Karagwe kwenda Benako.
Aidha Kamanda Msika amesema katika sakata hilo, majambazi hayo pia yalimpiga risasi na kumuua papo hapo mwanamke mmoja anayekadiriwa kuwa na umri wa kari ya miaka 30 na 35. Kamanda Msika amesema mwanamke huyo aliyeuawa bado hajatambuliwa. Kamanda Msika amesema majambazi hayo pia yamewajeruhi watu kadhaa wakiwemo wafanyabiashara wawili na askari polisi mmoja. Amewataja wafanyabiashara hao kuwa ni Bw. Nahimana Herbert ambaye ni raia wa Burundi aliyepigwa risasi ubavuni na Bw. Rutaha Evarist, 37, naye mkazi wa Mhinga nchini Burundi.
Akasema Bw. Evarist ambaye alikuwa akitokea Uganda kununua viatu vya mitumba amejeruhiwa kwa risasi bega lake la kushoto na mkononi. Kamanda Msika amemtaja askari aliyejeruhiwa kwa bomu kuwa ni mwenye namba G 1339 PC Yusufu. Amesema askari huyo pamoja na majeruhi wengine wamelazwa katika Hospitali ya Mrugwanza mjini Ngara. Kwa mujibu wa Kamanda Msika tayari polisi wameanza msako mkali katika pori hilo la Kimisi, ambapo tayari bunduki moja aina ya gobore imeshakamatwa.
Amesema pia maganda 31 ya risasi za bunduki aina ya SMG na mabaki ya mabomu yameokotwa eneo la tukio. Kamanda Msika amesema vikundi mbalimbali vya askari Polisi vimetumwa kuendesha msako katika pori hilo la Kimisi ili kukomesha vitendo hivyo vya uvamizi wa magari ambavyo vilikuwa vimeanza kutoweka. Aidha Kamanda Msika amewaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa askari ili kufanikisha kuwakamata majambazi hao ambao katika uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa walikuwa wakizungumza lugha za Kirundi na Kinyarwanda.
Akasema pia uchunguzi huo wa awali umeonyesha kuwa miongoni mwa majambazi hao alikuwemo mwanamke mmoja. Vitendo vya utekaji wa magari viliibuka kwa nguvu baada ya Tanzania kupokea wakimbizi kutoka nchi za Rwanda na Burundi, lakini katika kipindi cha miaka miwili iliyopita Serikali ya Tanzania ilifanikiwa kuvipunguza kwa kiasi kikubwa. [/size]