The Sheriff
JF-Expert Member
- Oct 10, 2019
- 747
- 2,112
Kuzaliwa, utoto, ujana, utu uzima na uzee ni hatua za kawaida katika maisha ya mwanadamu. Hatua hizi zote zina raha na shida zake. Kila hatua fulani inapopita nguvu za kimwili hupungua na vilevile utulivu wa akili huzorota.
Kwa kuwa umri unasonga, masuala mbalimbali ya kiafya hutokea. Baadhi ya magonjwa yanayojulikana kwa kawaida ni shinikizo la damu, kisukari, matatizo ya moyo, saratani, maumivu ya viungo, na mengine chungu nzima.
Idadi kubwa ya wazee wanapitia changamoto za kiafya, na ni wakati huu ambapo wanahitaji matunzo na faraja ili kuishi maisha yenye furaha bila wasiwasi na huzuni. Mara nyingi ukosefu wa ufahamu kuhusu mabadiliko ya tabia kwa wazee nyumbani yanaweza kusababisha kunyanyaswa na watu wao wa karibu.
Kwa kutokuwa na uwezo wa kuelewa mahitaji na wasiwasi wa wazee, mara nyingi jamii huwatazama kama mizigo. Lakini pia, wazee wapo kwenye hatari ya kutendewa vibaya na wanafamilia kwa sababu ya mali. Baadhi yao wanalazimishwa kuuza mali zao na kuishi maisha duni hadi kufa.
Hata hivyo, jambo moja tunalopaswa kuliweka akilini ni kuwa wazee, kama watu wengine wote, pia wanatamani maisha yenye furaha, utu, uhuru na hatimaye kifo cha amani. Wanatamani kutunzwa vizuri, kujaliwa na kuoneshwa upendo. Hivyo kuelewa mahitaji na wasiwasi wao, kunaweza kuwapa amani na hatimaye maisha yenye furaha, hata kama wanakabiliwa na maradhi.
Kutoa usaidizi wa kihisia kwa wazee kunaweza kuwafanya wawe na furaha, ambayo bila shaka ndiyo njia bora ya kuishi maisha yenye afya na amani. Hata hivyo, kwa watu wengi, kutoa huduma na uangalizi kwa wazee haiwezekani kutokana na vipaumbele vya kazi, lakini ni wajibu wetu kwenye jamii kuhakikisha kuwa wazee wetu wanafurahia maisha yao ya uzee ikiwa ni pamoja na kupata mapenzi ya familia au watu wao wa karibu.
Kuwa mlezi wa mzee kunaweza kuwa jukumu gumu, kwani jukumu hilo linaweza kumgharimu mtu kihisia na kimwili, lakini tunahitaji kujitolea kwa moyo mmoja na uvumilivu.
Ni vyema kuelewa kwamba wakati mwingine wazee wanapitia wakati mgumu kihisia kama vile kushindwa kujihudumia na kuwa na uhuru wa kufanya mambo yao wenyewe. Tukumbuke kwamba kupoteza uhuru kutokana na uzee au maradhi ni mojawapo ya mabadiliko magumu zaidi kwa mtu yeyote kupitia.
Kuwa na uvumilivu ni jukumu zito na linaweza kuchosha sana, lakini kuwaonesha wazee wetu heshima na upendo ndilo chaguo bora siku zote. Ni muhimu kufanya kila liwezekanalo kuwaonesha upendo na kuwapatia faraja wakati wote. Hii ni pamoja na kuwaondoa katika majukumu yanayowahitaji kutumia nguvu nyingi za kiakili na kimwili.
Ni muhimu kukumbuka kuwa sio tu kuwa tunahitaji kuwajali, lakini pia tunapaswa kuwaonesha kuwaheshimu.
Ikiwa leo ni Oktoba 1, ambayo ni Siku ya Wazee Duniani, mimi kama mmoja wa watu ambao nimebarikiwa kuwa na wazee kadhaa katika familia, nimeona ni vyema tukumbushane mawili matatu kuhusu masuala yanayowahusu wazee wetu.
Tubarikiwe sote!