Maziwa ya kopo ni hatari kwa watoto wachanga
Fredy Azzah
WAZIRI wa Afya na Ustawi wa Jamii Profesa David Mwakyusa amewataka kinamama kuepuka kuwapa watoto wao maziwa ya kopo isipokuwa pale watakapokuwa wameshauriwa na daktari kwa sababu yana athari za ubongo, ukuaji na mengine ni sumu.
Amesema maziwa mengi ya kopo ni hatari kwa afya za watoto wao hivyo akahimiza kuzingatia zaidi utaratibu wa kunyonyesha.
Alitoa rai hiyo wiki hii Jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuwahamasisha wanawake kuwanyonyesha watoto maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya mwazo.
Katika hotuba hiyo ya Profesa Mwakyusa iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bilandina Nyoni kinamama wengi huamasishwa na matangazo ya maziwa hayo ambayo aliyaelezea yanatoa taarifa zisizo sahihi.
Usambazaji holela wa maziwa ya unga na vyakula vingine vya watoto ni changamoto. Maziwa mengi hayana ubora na baadhi ya matangazo ya biashara yanapotosha hivyo wanawake wanajikuta wakiwapa watoto wao sumu, alisema.
Hata hivyo, alisema serikali inaendelea kudhibiti uingizwaji wa maziwa hayo hapa nchini kwa kuwabana wafanyabiashara wanaoyapitisha njia za panya.
Profesa Mwakyusa alisema takwimu zinaonyesha kuwa ni asilimia 41 tu ya wanawake nchini wanaonyonyesha watoto wao kama ilivyopendekezwa kitaalamu.
Alisema baadhi ya wanawake huanza kuwachanganyia watoto wao maziwa na vitu vingine baada ya miezi miwili tangu wazaliwe.
Takwimu zinaonyesha kwamba, kwa watoto wenye umri chini ya miezi miwili kiwango cha unyonyeshaji maziwa ya mama pekee ni asilimia 70, wenye miezi miwili mpaka mitatu kiwango cha unyonyeshaji ni asilimia 42.3 huku wenye miezi mine mpaka mitano; kiwango cha unyonyeshaji kikiwa asilimia 13.5, alisema.
Alisema, athari za kuwachanganyia watoto wenye umri huo maziwa kinaathiri ukuaji wa miili na ubongo wao na pia uwezo wao wa kufikiri.
Mbali na madhara hayo, alisema baadhi ya maziwa ambayo hayana viwango yanaweza kuwa sumu kwa watoto na hata kuwasababishia magonjwa yanayoweza kusababisha kifo.
Usambazaji holela wa maziwa ya unga na vyakula vingine vya watoto ni changamoto. Maziwa mengi hayana ubora na baadhi ya matangazo ya biashara ya maziwa haya yanayotolewa yanapotosha hivyo wanawake wanajikuta wakiwapa watoto wao sumu, alisema.
Naye mtaalam kutoka taasisi ya chakula na lishe Neema Joshua alisema kinamama wanaofanya kazi sehemu ambazo hawawezi kwenda na watoto wao wanapaswa kukamua maziwa yao na kuyaacha nyumbani ili motto anyweshwe.
Source:
?Maziwa ya kopo ni hatari kwa watoto wachanga?