SoC03 Ni namna gani serikali ifanye ili kukuza wigo wa ukusanyaji mapato

SoC03 Ni namna gani serikali ifanye ili kukuza wigo wa ukusanyaji mapato

Stories of Change - 2023 Competition

Undava King

JF-Expert Member
Joined
Aug 11, 2017
Posts
3,422
Reaction score
5,659
1.KUONGEZA UKUSANYAJI MAPATO KUPITIA STENDI ZA MABASI

Utaratibu wa stendi za mabasi uboreshwe katika maeneo yafuatayo:-

A) Wenye mabasi mengi wapewe vipaumbele kwanza kwenye ugawaji wa vizimba na siyo maajenti; kumekuwa na sintofahamu katika ugawanyaji wa vizimba vya ukataji tiketi ambapo inapelekea wamiliki wa makampuni makubwa ya mabasi kukosa sehemu ndani ya stendi na badala yake wale wenye vizimba wanakuwa ni wale wasio na wateja wengi au mawakala, kitu kinachopelekea wamiliki wengi kukosa chaguo nakuamua kupangisha nje ya jengo la stendi au mbali mitaani nakuathiri mfumo wa ulipaji mapato.

B) Agenti asajiliwe na ofisi yake kwa ajili ya kuhudumia kampuni moja tu, imekuwa ni changamoto kubwa na kero kwa abiria pindi wanapotaka kukata tiketi kwa ajili ya safari, inakuwa ni vigumu kupata tiketi ya gari ambalo unatarajia kulipanda kutokana na utitiri wa mabandiko ya magari mengi katika kuta za ofisi za mawakala hao,

pili ofisi husika huwa na mashinikizo au minadi mingi yakukufanya upande gari fulani ambalo wao wanajua fika haliwezi kupata abiria wengi kutokana na mapungufu fulani fulani, ukihoji basi lingine utaambiwa limeshajaza au ongeza nauli n.k

Ilimradi wao wafanikishe adhma yao pasipo kujali maslahi ya mteja wao, hii ni kwa kuwa maajenti hawa wanarundo la makampuni ya magari mezani kwao lakini kama angekuwa anawajibika kwa ajili ya kampuni moja basi ufanisi ungekuwepo achilia mbali kila kampuni ingejitahidi kuboresha huduma hili isiachwe nyuma au kukimbiwa na mawakala kitu ambacho kingeleta ushindani zaidi.

C) Maajenti wahusike moja kwa moja kwenye kulipa kodi kulingana na kiwango wanachoingiza, kumekuwa na uonevu kwa wamiliki wa mabasi ambapo kwa wastani wa chini wa nauli ya Dar-Mwanza tuchukulie mfano ni 60000 ila cha ajabu kwa kila kichwa (abiria) ajenti ujilipa 20000 huku mmiliki ambaye ni mlipa kodi na mwenye utitiri wa malipo ya faini,mishahara,matengenezo na vibali ujilipa 40000 je, ni haki hii kwa mmiliki wa chombo? Ifikie wakati maajenti hawa nao sheria itafute namna ya kuwabana wachangie mapato maana kwa hali ilivyo sasa wananeemeka pakubwa kuliko hata wamiliki wa vyombo wenyewe.

D) Vyumba ambavyo havina wapangaji bado(not full occupied) kisa matumizi yake hayaelekezi hivyo aidha ni kwa matumizi ya supermarkets,gym,n.k yagawiwe kwa wafanyabishara wenye matumizi navyo kwa wakati husika hata kama matumizi yake yatabadilika, kikubwa ni kutengeneza mapato na pale atakapopatikana mpangaji aliyetakiwa, wale wapangaji wasio rasmi kwa mujibu wa matumizi ya eneo husika watampisha mwekezaji halisi wa eneo hilo.

E) Stendi zifate matekelezo ya plan walizokuwa nazo mwanzo wakati wa uandaaji miradi, chukulia mfano stendi kama Nyamhongolo ya jijini Mwanza ina parking kubwa kwa ajili ya malori na hosteli kwa ajili ya wageni lakini tokea stendi imeanza kazi yapata mwaka sasa hakuna kinachoendelea,

Hili linapunguza mapato kwa halmashauri husika kwani kama wangeweka utaratibu unaofaa na uwe unafatwa wa kulaza malori yote transit ndani ya stendi na siyo mitaani na kwenye sheli za mafuta, wasingekosa mwekezaji ambaye angeona fursa ya biashara katika hosteli za hapo stendi lakini pia hili lingechochea kukuza biashara zote katika eneo la kuzunguka stendi.

F) Mabasi ya masafa marefu hususani ya Dar-Mwanza na kwingineko yaruhusiwe pasipo vizuizi vya masaa na ushuru wa kujirudia-rudia magetini pale wanapoanza safari zao asubuhi katika eneo la Nyamhongolo na baadae kupitia Nyegezi au viseversa, kuwekwe utaratibu mmoja na unaoeleweka ambao utawapa ahueni wamiliki wa mabasi haya kuwa na wigo mpana na machaguo ya namna ya kuwafikia abiria wao kwa urahisi na kwa wakati kama ambavyo lengo la kujenga stendi mbili jijini mwanza lilivyokuwa kuwa nje ya kukusanya mapato lakini pia nikurahisisha usafiri kwa wakazi wa jiji lote na viunga vyake.

2. TUUTAMBUE MCHANGO WA WAGANGA/MADAKTARI WA JADI NA TUWARASIMISHE NA KUWAJENGEA UWEZO, HILI NAO WALIPE KODI KUPITIA HUDUMA WANAZOTOA.

Kuna kundi muhimu mno katika jamii la wataalamu wenye vipawa vya asili vya kutatua matatizo mbalimbali ya kijamii hususani magonjwa (sizungumzii waganga wa tiba asili/ramli)lakini huwa hawapewi kipaumbele au ni kama wamesahulika mpaka tukiwa na matatizo ndipo tunawafanya kimbilio.

Watu hawa invincible katika jamii ndiyo wanaofanya mahospitali yetu yasielemewe na wagonjwa lakini pia hutoa matibabu makubwa kwa gharama nafuu mno kwa watanzania wenzetu wasiokuwa na uwezo wa kumudu matibabu ghali ya hospitali.

Mfano mdogo miaka mitatu iliyopita rafiki yangu alipatwa na tatizo la kilimi kilichokomaa kiasi cha kurefuka na kumnyima pumzi kabisa tulipofika hospitalini, daktari hakujiangaisha hata kuandika vidonge alituambia rudini tu nyumbani mkajiandae kisaikolojia kwa kuwa huyu mtu hawezi kupona, lakini tulipokuwa tumekata tamaa wanajamii wakatufikisha kwa bingwa wa ukataji vilimi na tatizo hilo likawa historia.

Huo ni mfano mdogo tu wa umuhimu wa wataalamu hawa wa kuunga mifupa, kutibu uzazi, ukunga, vilimi, utumbuaji majipu, ukandaji, matatizo ya chemba ya moyo,n.k walivyo na mchango mkubwa kwa jamii iishiyo mbali na vituo vya afya, lakini pia kwa matatizo yale ambayo bado upeo wa sayansi haujafikia bado au hauna ufanisi mkubwa nao.

Kilichofanya niwazungumzie watu hawa ni mazingira yao duni ya ufanyaji kazi zao na vifaa vyao vya utendaji kazi ambavyo ni hatarishi kwa afya ya wagonjwa wanaopokea matibabu kwao.

Unakuta msururu wa wagonjwa wameketi mlangoni wakingojea matibabu ambayo utegemea zaidi mikasi, visu, nyembe zilezile kwa kila mgonjwa na hali ya usafi inakuwa pia hairidhishi hamna gloves, dustbin wala eneo la kujisaidia na kujisafishia wagonjwa.

Watu hawa licha ya vipawa walivyojaaliwa na Mungu, bado wanahitaji serikali iwatambue na kuwaboreshea mazingira yao ya ufanyaji kazi ikiwezekana wawe wakipatiwa baadhi ya vifaa tiba muhimu bure, waboreshewe mazingira yao ya utendaji kazi, wapewe vipaumbele katika mikopo au wawezeshwe hili nao walipe kodi, wapewe ushauri na mafunzo muhimu ya kitaalamu na namna ya kutekeleza majukumu yao pasipo kukiuka misingi ya kiafya.

Siku zote jukumu la usalama na afya za wananchi ni jukumu la serikali hivyo serikali isiwaachie mzigo mzito watu hawa ambao hujitoa kwa hali na mali kuisaidia jamii lakini mchango wao hautambuliwi licha ya kuwa tunatambua fika kuwa idadi ya wagonjwa kwa kila daktari mmoja bado ni kubwa mno na inaelemea sekta ya afya.

3. TUWATUMIE WATENDAJI WA SERIKALI ZA MITAA/VIJIJI KUONGEZA UFANISI KATIKA ZOEZI LA ULIPAJI KODI

Hili kuongeza ufanisi katika zoezi la ulipaji kodi na kuwafikia wafanyabishara wote katika ngazi ya mtaa au kijiji ambako ndiko haswaa penye mzizi wa mapato tunapaswa kumtumia vilivyo mtu reliable pekee wa serikali ambaye kwa kiasi kikubwa huwa na taarifa nyingi na sahihi za eneo husika kuhusu wafanyabiashara na wananchi wote wa eneo lake ambaye ni mtendaji.

Kutokana na upungufu au ukosefu wa vitendea kazi, idadi ndogo ya wafanyakazi katika idara ya biashara na TRA, hawawezi kutuhakikishia ufanisi katika ukusanyaji mzuri wa mapato na taarifa sahihi za walipa kodi kwa nchi nzima.

Mfano idara ya biashara katika halmashauri ya mji X ina gari moja na maafisa watano tu wanaotakiwa kuwafikia wafanyabishara 1000 na zaidi walioko mjini na bado wale walioko vijijini kuwaelimisha na kuwaelekeza mmoja mmoja namna ya kukata leseni za biashara kidigitali lakini ikiwemo pia kuwa na taarifa zote muhimu kuhusu wateja wao kila wakati, je hili linawezekana kufanyika kwa asilimia mia kwa idadi hii ya watumishi tulionao na vitendea kazi vyao? Bila shaka hatuwezi kufikia asilimia hata 10 ya ukusanyaji mapato kwa usahihi kwa staili hii.

Hivyo napendekeza serikalini iwatumie watendaji wa mitaa/vijiji kama ifuatavyo:-

A) Watendaji wapewe mamlaka kamili katika ku-identify na kukusanya taarifa za walipa kodi katika maeneo yao na kuwasilisha katika mamlaka husika hili zifanyiwe kazi na hili lifanyike kila mara ndani ya kipindi maalumu cha muda utakaokubalika kitaalamu.

B) Watendaji wapewe elimu kuhusu kodi na leseni za biashara na wasaidiane na mamlaka za biashara na za ki-kodi katika kuwafikia walengwa.

C) Watendaji wasaidiane na mamlaka husika katika kufikisha elimu ya ulipaji kodi na kutatua changamoto ndogondogo kwa wananchi wao zinazotokana na uelewa mdogo kuhusu mambo ya ki-kodi na pale jambo linapokuwa linahitaji ufafanuzi wa kitaalamu wawe ni kiunganishi muhimu kati ya mfanyabiashara na TRA au idara ya biashara katika mazingira yao.

D) Katika maeneo ambayo yana uhaba mkubwa wa wataalamu,changamoto ya miundombinu au hayafikiki kwa urahisi, watendaji wanaweza kuwa msaada mkubwa katika kuwatambua walipaji kodi wao na kukusanya mapato kwa njia ya kielektroniki kwa niaba ya mamlaka husika na hivyo kufanikisha adhma ya serikali kuwafikia walipa kodi wote kwa wakati na kwa ufanisi.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom