Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
NI SAHIHI KUWATENGA WANAFUNZI WETU KWA KIGEZO CHA WENYE VIPAJI?
JUMATANO ya Novemba, 5 2014 Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) lilitangaza matokeo ya mtihani wa darasa la saba uliofanyika mwezi Septemba, 2014 yalioonesha kuwa, zaidi ya nusu ya wanafunzi waliofanya mtihani huo wamefaulu.
Matokeo hayo yaliyotangazwa na Katibu Mkuu wake Mtendaji Dk Charles Msonde yanaonesha kuwa, wasichana wamefanya vema zaidi kuliko wavulana huku ufaulu kwa ujumla ukiwa umeongezeka kwa asilimia 6.38 ikilinganishwa na mwaka 2013.
Wakati Watanzania tukisubiri watoto wetu kupangiwa shule za kwenda kusoma kwa waliofanya vizuri, nimeona nidadisi suala hili ambalo ninaamini hakuna lisilomgusa.
Kwa muda mrefu Serikali yetu imekuwa na desturi ya kuwapanga wanafunzi wanaoingia shule za sekondari kulingana na alama za ufaulu.
Hapa nakusudia shule maalum za wenye vipaji( (Genius)ambazo idadi yake hailingani na zile za kawaida.
Kabla sijenda mbele, nikiri mapema kuwa,
sina hakika lengo la utaratibu huu lilikuwa lipi. Na kama limefikiwa ama bado, na ikiwa limefikiwa ni kwa kiasi gani.
Bali ipo dhana miongoni mwetu kwamba, mpango huu baada ya kuanzishwa kwa shule nyingi za kata umeonesha dhahiri pengo kati ya aina hizo mbili za shule.
Pengo hili, binafsi ndilo lililonisukuma kushika kalamu na kutaka kudadisi, iwapo ni sahihi kuendeleza mfumo huu wa kuwatenganisha wanafunzi kwa kigezo cha viwango vya alama za ufaulu ama la?
Najua kwamba, ukiingia darasani ni lazima ukutane na aina kuu mbili za wanafunzi ambapo kama mwalimu, ni lazima uhakikishe wote wanalielewa vema somo unalowafundisha.
Wapo wanafunzi wasiochelewa kumwelewa mwalimu. Hawa wanajulikana kitaalamu kama ‘genius', na wapo wanaochelewa kuelewa ambao nao kitaalamu wanajulikana kama ‘slowleners'.
Kwa wanaoafikiana na utaratibu huu wanasema, lengo lilikuwa ni wale wa shule za kawaida (slowleners) kufundishwa kwa bidii huku ikifahamika wazi kwamba, ni wanafunzi wa namna gani.
Hata hivyo wanasema baadhi ya walimu katika shule hizi za serikali zenye wanafunzi wa aina hii wamekuwa wazembe na wanafundisha ‘bora liende'!
Haijulikani iwapo hata walimu wanaofundisha kwenye shule za wanafunzi wenye vipaji nao wako hivyo hivyo ama la!
Aidha kundi hili pia linataja sababu nyingine ya kuunga mkono mfumo huu ni kwamba, huwezi kuwachanganya wenye vipaji watatu na kina ‘Kayumba' 160 kwenye darasa moja ukategemea vijana hao watatu watabaki salama bila ‘kukokotwa' na fikra za wanafunzi hao 160.
"Mkaa mmoja wenye moto ukiuweka kwenye rundo la majivu, ni lazima mkaa huo wa moto utazimika tu", alisema mwananchi mmoja wa kawaida mkazi wa Mbwewe wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Mkazi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Abddalllah Mpozo alisema hayo akimaanisha kwamba, ni muhari kuepuka utaratibu huu kutokana na hali halisi ya mfumo wa elimu yetu.
Hata hivyo wapo wanaoona iko haja ya serikali kuangalia upya faida na hasara za kuendeleza utaratibu huu wa kuwatenganisha wanafunzi kwenye shule maalum za vipaji.
Wamesema pamoja na mfano wa mkaa wa moto kuzimika ukiwekwa kwenye majivu, wamekumbusha kuwa, ukiwekwa kwenye mkaa usio na moto, wote utawaka.
"Haiwezekani mtu akae na muuza uturi (mafuta mazuri) halafu asinukie hata kidogo!, ni lazima atanukia tu atake asitake!", alisema mtu mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Nunu Zuber mkazi wa mji mpya, mkoani Morogoro.
Vilevile wanaongeza kusema kuwa, hakuna haja ya kuwatenganisha wanafunzi hawa kwasababu pengo baina ya shule hizi linakuwa kubwa mwaka hadi mwaka na kuleta manung'uniko miongoni mwa watanzania.
Mfano wanasema matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2013 ya shule ya wavulana Kibaha mkoani Pwani ambapo jumla ya wanafunzi 87 walifanikiwa kufanya mtihani.
Kati yao daraja la kwanza walikuwa 44, daraja la pili walikuwa 31, daraja la tatu 12 na daraja la nne walikuwa sifuri.
Wakati hiyo ni shule ya vipaji maalum, wanasema tuangalie shule za ‘mjomba rashid' na hapa tuna shule ya sekondari Kibuta iliyoko mkoani Pwani.
Ambapo matokeo ya mwaka 2013 mtihani huohuo daraja la kwanza 0, daraja la pili 0, daraja la tatu nalo 0, na daraja la nne walikuwa wanane huku waliofeli walikuwa 25.
Mbali na mfano huo, zipo shule kama ile ya wasichana ya Kifungiro mkoani Tanga ambayo daraja la kwanza -68, la pili -23, la tatu-3 na 4-0.
Mzumbe sekondari ya mkoani Morogoro mtihani huo ilifaulisha daraja la kwanza-57, la pili-27, la tatu walikuwa 15 na daraja la 4-9.
Aidha shule nyingine za vipaji ambazo baadhi ya wananchi wanaopinga utaratibu huu wamezitolea mfano kuwa ni pamoja na Kilakala shule ya wasichana iliyoko mkoani Morogoro.
Katika shule hii daraja la kwanza walikuwa-34, la pili walikuwa-32, daraja la tatu walikuwa-7,na daraja la nne walikuwa-10 na hakukuwa na waliofeli!
Lakini ukitazama matokeo katika shule nyingine za sekondari kama vile Mafiga sekondari ya mkoani Morogoro, utaona iko haja ya serikali kufanya marekebisho juu ya mpango huu.
Kwenye shule hiyo ambayo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) Hawa Abdulrahman Ghasia alikataa kupiga picha ya pamoja na walimu wake, matokeo yanasomeka kama ifuatavyo:
Daraja la kwanza-0, daraja la pili-0, daraja la tatu-2, daraja la nne-40 na waliofeli walikuwa 128!
Na shule ya sekondari Kitonga iliyoko mkoani Dar es salaam matokeo yalikuwa daraja la kwanza-0, la pili-0, la tatu-0, la nne-5, na waliofeli walikuwa-38.
Kwa mifano hii michache niliyoitanguliza hapo juu ambayo nimepewa na baadhi ya wananchi wenzangu wa kawaida, kwa kiasi fulani imeanza nami kunishawishi nikubaliane nao, ingawa UDADISI wangu bado upo palepale.
Aidha ukiyachungulia kwa makini matokeo ya shule hizo utabaini kwamba, wakati shule za ‘genius' kuanzia daraja la kwanza wanakuwa wengi na kupungua wanapofikia daraja la tatu na hatimaye kukosekana kabisa ‘ziro'.
Kina ‘Kayumba' wao wanakosa daraja la kwanza mpaka la tatu, lakini kuanzia daraja la nne wanaanza kuongezeka na idadi yao inazidi inapofikia daraja ‘ziro'.
Je, bado kuna ulazima wa kuendelea na mfumo huu wa kuwatenganisha wenye vipaji na wasionavyo?
Tukutane juma lijalo hapahapa kwa udadisi mwingine wa kukata na shoka.
Toa maoni yako.