Ni uwekezaji au ukoloni mamboleo?

tenende

JF-Expert Member
Joined
Jan 10, 2012
Posts
6,511
Reaction score
505
[h=2] MWANDISHI wa Kitabu cha 'False Starts in Africa,' Rene Dumont, ambacho tafsiri yake kwa lugha ya Kiswahili ni
'Afrika inakwenda kombo,’
alielezea kuwa Afrika imeshindwa kutekeleza hatua zake za maendeleo baada ya kupata uhuru kutokana na athari zilizotokana na tawala za kikoloni.[/h]
Alisema kuenea kwa 'wimbi la mabadiliko' kulisababisha Afrika kugeuzwa kutoka bara lililokuwa koloni kuwa mchanganyiko wa mataifa huru bila kukidhi mahitaji ya umoja wa kijiografia au kijamii.

Kuvunjika huko kwa umoja miongoni mwa jamii hizo kulisababishwa na kuingia kwa nguvu kubwa za ushindani wa kikoloni mwishoni mwa karne ya 19.

Dumont alimaanisha kuwa hali ya Afrika jinsi ilivyo sasa mifumo yake imeundwa na wakoloni na baada ya uhuru, nchi nyingi za Afrika hazikuchukua hatua sahihi za kujisimamia wala kuwa tayari kusahihisha makosa yaliyojitokeza au kuendelea kujitokeza.

Kilichojitokeza baadaye miongoni mwa nchi nyingi ni suala la utaifa na ambao haujatambuliwa na kuchukuliwa kwa upana wake baada ya uhuru.

Baada ya uhuru wa nchi nyingi za Afrika kilichofuatia ni kugubikwa na masuala muhimu ya maendeleo na hata hivyo mwangwi wa utawala wa kikoloni umeendelea kuwepo.

Hata baada ya uhuru, serikali na jamii kwenye mipango yake ya maendeleo na kujenga taifa ikiwa ni pamoja na utaifishaji wa baadhi ya rasilimali, utendaji wa masuala muhimu na mambo mengine mengi ulifanyika kwa utashi wa wanasiasa au watu binafsi waliokuwa wanajituma.

Ukweli unabakia kuwa mataifa mengi baada ya kupata uhuru yameendelea kuegemea katika mataifa yaliyopata kuzitawala kwa majina au lugha tamu kama wahisani au wafadhili na hivyo kukosa uhuru wa kiuchumi. Zimejikuta zikining'inia kwenye mabega ya nchi hizo.

Nchi zinazozungumza Kiingereza zimejibanza Uingereza, zinazozungumza Kifaransa, Ufaransa na zinazozungumza Kireno.

Uhuru wa kiuchumi unamaanisha uhuru wa kuchagua mawakala wa kiuchumi, wawe ni wazalishaji, walaji, waajiriwa au waajiri.

Kuwa tegemezi kiuchumi ambako Afrika inazitegemea Nchi za Magharibi, kunaonekana kuzifanya zishindwe kuendelea na hivyo hali yake ya kiuchumi kuwa na vidokezo kadhaa ambavyo vinaonyesha kuathirika kwa muundo wake wa uzalishaji na hata uendeshaji wa biashara.

Aidha, uchumi unaonyesha kuwa misaada ya nje na mitiririko ya mitaji binafsi imekuwa inaunda sehemu kubwa ya uwekezaji kwenye sekta za umma na uwekezaji wa jumla ndani ya nchi.

Hali kadhalika, mgawo wa watu kutoka nje kwenye akiba ya mitaji ndani ya sekta za sasa na nguvu kazi yenye stadi ni kubwa na matokeo yake mgawo wa nje kwenye pato la jumla la ndani kuwa kubwa.

Hali hiyo inaogopesha kuona kuwa miaka michache baada ya kupata uhuru kutoka kwa Ufaransa, sera za kiuchumi za nchi za Afrika zinazozungumza Kifaransa kubakia kuwa nakala za sera zilizopokelewa kwa ajili ya kukidhi maslahi ya Ufaransa.

Vivyo hivyo, kwa zinazoitwa nchi za Jumuiya ya Madola zinaning’inia mabegani mwa Uingereza. Ukweli unabakia kuwa nchi zinazozungumza Kifaransa, Umoja wa Ulaya, Jumuiya ya Madola na taasisi nyingine za Magharibi zinakuwa na ushawishi barani Afrika kwa kutoa huduma rahisi ili ziweze kuvuna rasilimali zake.

Kwa upande mwingine, nchi za Afrika zinaweza kunufaika au kupata hasara. Mtazamo unaokuwepo ni kwamba nchi za Afrika zinatakiwa zijiondoe kwenye ulaghai wa kuamini kwamba nchi za magharibi zinavutiwa na ustawi wake kiuchumi.

Kuamini hivyo ni kujidanganya. Waafrika wanatakiwa waache kuamini kuwa misaada ya fedha ni suluhisho la matatizo ya maendeleo ya Afrika.

Afrika inachohitaji si misaada, bali ushirikiano wa kibiashara ulio na uwiano sawa. Serikali za Afrika zinatakiwa kufanya zaidi ya ndoto za mchana na kuondokana na ahadi tupu.

Ni wakati wa kuondokana na utegemezi wenye utata kwa nchi zilizokuwa zinazitawala. Ipo haja ya kufanya mambo tofauti na kuondokana na kile kinachoweza kuelezwa kuwa ni bara lililofungwa minyororo.

Mwelekeo wa kusonga mbele kwa Afrika na kustawi kijamii na kiuchumi kumedokezwa kwenye mpango mpya wa ushirikiano wa maendeleo wa Afrika ambao ulibuniwa na Umoja wa Afrika.

Mpango huo unaonekana kama jukwaa la Afrika katika kuunganisha sera muhimu za kiuchumi kwa Afrika. Itakuwa ni huzuni kama jukwaa hilo litageuzwa kuwa sehemu ya mazungumzo kama ilivyokuwa imezoeleka kwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU).

Pindi hilo likifanyika, Afrika itakuwa imepata uzoefu mpya wa maisha na pia itaweza kuweka madai yake sahihi ya uhuru wa kiuchumi.

Lakini hilo litawezekana kwa kuendesha ujasiriamali kwa kutumia rasilimali za ndani badala ya kutegemea ujasiriamali kutoka nje. Aidha ufanisi wake utakuwa ni kuwezesha wazalendo kuchukua au kutumia fursa za uzalishaji badala ya kutegemea wawekezaji wa nje wakati walio wengi wapo ndani ya nchi.

Yanaweza kuwepo mambo mengi ya kijamii, kisiasa na kiuchumi katika kufanikisha hali hiyo, lakini jambo la kukumbuka ni kwamba wawekezaji wamekuwa wanawekeza kwenye siasa na kwenye tabaka linalotawala kwa nguvu mpya, ari mpya na kasi mpya, waweze kudhibiti na kupata rasilimali zinazokuwepo.

Hali ngumu ya uchumi wa Afrika inatokana na sababu za nje na ndani, ukiwemo ukoloni mamboleo, migongano ya ubepari uchwara na mabepari wa nchi zilizoendelea, mikakati ya kutafuta suluhisho la kudumu la matatizo, kukiwa na migongano ya nguvu za Magharibi inayoingilia masuala ya mambo ya ndani ya mataifa mengi ya Afrika.

Katika dhana rahisi tu ni kwamba Umoja wa Afrika umekosa nguvu ya kukemea au kulaani uvamizi wa majeshi ya kigeni kwa hofu ya kuwaudhi wahisani wa fedha za maendeleo na hususani bajeti zake.

Pamoja na utegemezi unaokuwepo, kinachojidhihirisha sasa ni kasi ya uporaji wa ardhi na rasilimali nyingine kwa jina la uwekezaji, hivyo kufanya wazalishaji wadogo kutupwa pembezoni.

Lililo wazi ni kwamba wawekezaji wanawezeshwa na wazawa kufanikisha uwekezaji wao kwenye rasilimali hizo bila kujali maslahi ya wazalendo, hivyo kujenga taswira inayotolewa na kitabu hicho ya kuwepo kwa wateule wachache wanaoishi kifalme.

"Haiwezekani kuendeleza nchi kwa kuongeza maradufu wafanyakazi wa ofisini au kwa kugawia marafiki vyeo vinavyowapatia mishahara bila kufanya kazi, ila tu kwa kuunganisha watu wenye utashi wa kazi ili kutekeleza matakwa yanayomfaidisha kila mmoja. Iwapo mambo hayatarekebishwa, uendeshaji wa serikali ndiyo utakaoteketeza nchi za Kiafrika."

Taswira hiyo inaonyesha kuwa 'uwekezaji' ni lugha au neno laini kwa maneno 'ukoloni mamboleo', hali ambayo inaweza kuhitimishwa kwamba bila kupitiwa upya dhana nzima ya uwekezaji basi itakuwa ni kweli Afrika inakwenda kombo.

Source: Mtanzania

Mytake: Hata mikataba hii ya wachina itakapolipuka na siri yake kubumburuka viongozi watatafuta mahali pa kuficha nyuso Zao - wakati wananchi wanaanza kudai CHAO!!!!
 
Huu ni mtihani mkubwa saana katika bara la AFRIKA!!!
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…