Katika wiki za hivi karibuni suala la kutafuta asili ya virusi vya Corona limekuwa likizungumzwa sana katika nchi mbalimbali duniani. Kwa bahati mbaya baadhi ya wanaolizungumzia suala hilo, kuna wale wanaoelekeza hoja zao kwenye mambo ya siasa, na wengine, hasa wanasayansi wameweka mkazo kwenye sayansi, yaani kutafuta chanzo cha virusi.
Hata hivyo kumekuwa na hoja mbalimbali kuhusu suala hili. Kuna wale wanaona kuwa dunia inatakiwa kukusanya nguvu zake kuleta kutatua tatizo, yaani kuhakikisha chanjo inapatikana, ikiwezekana na dawa ipatikane na hatimaye ugonjwa huu utokomezwe na dunia irudi katika hali yake ya kawaida.
Kuna wengine wanasema licha ya hilo kutakiwa kuwa lengo kuu, kuna hoja ya kuwa virusi vya Corona vilitoka maabara haitakiwi kupuuzwa. Na hata kama kuna uwezekano kidogo kuwa virusi hivi vilitoka maabara kutokana na dosari za kiusalama kwenye maabara, sio jambo baya kuchunguza. Ni kutokana na ukweli huu, China iliridhia wataalam kutoka Shirika la Afya Duniani, kwenda kufanya uchunguzi kwenye maabara ya utafiti wa virusi mjini Wuhan. Lakini tangu virusi vya Corona vilipogunduliwa mjini Wuhan mwanzoni mwa mwaka jana, kuna hali ya ajabu ambayo imekuwa inatokea na kuleta maswali mengi kuhusu virusi hivi vilitoka wapi.
Kwanza, si mara moja wala mara mbili tumesikia wataalam wa maabara za damu waliohifadhi sampuli za damu kutoka vipindi mbalimbali kabla ya kuibuka kwa virusi vya Corona. Wataalam hao wamesema kuna ushahidi kuwa kwenye baadhi ya sampuli kulikuwa na virusi vya Corona. Hii imegunduliwa nchini Italia, nchini Marekani na hata nchini Brazil.
Pili, ni baada ya kutokea kwa wimbi la maambukizi mjini Wuhan ndio dunia ikaanza kujua kuwa kumekuwa na ajali kadhaa za kuvuja kwa virusi kutoka kwenye maabara mbalimbali duniani. Mwaka 1972 virusi vya ugonjwa wa ndui vilivuja kutoka kwenye maabara moja mjini London, na mwaka 1978 virusi hivyo vilivuja tena kutoka kwenye maabara mjini Birmingham. Na mwaka 2007 ugonjwa wa Kwato na midomo ya ng’ombe pia ulitajwa kuwa ulisafirishwa kwa matairi ya gari yaliyokanyaga virusi hivyo kwenye maabara moja ya kushughulikia maji taka. Na virusi vya H1N1 vilivyoonekana kwa mara ya kwanza mwaka 1918, vimetajwa kuwa vilitokana na kuvuja kwa virusi kwenye maabara moja nchini Marekani wakati wa majaribio ya kutengeneza chanjo. Kwa hiyo sauti za kutaka kuwepo kwa uchunguzi kwenye maabara una msingi.
Hata hivyo kumekuwa na mambo ya kusikitisha kidogo, pale ambapo inaonekana kuna vigezo tofauti linapokuja suala la uchunguzi kuhusu uwezekano wa kuvunja wa virusi kutoka maabara. Hivi karibuni imefahamika kuwa theluthi mbili ya wanyama katika eneo moja wamekuwa kiwango cha juu cha kinga mwili ya COVID-19. Kwa mujibu wa maelezo ya kisayansi, kinga mwili huwa inaonekana kwa wanyama walioambukizwa ugonjwa fulani. Lakini ajabu ni kuwa sauti za kutaka uchunguzi kuhusu hali hiyo ufanyike zimekuwa zikipinga au kupuuzwa kwa makusudi.
Lakini pia kumekuwa na taarifa nyingi kuhusu kuumwa magonjwa yasiyojulikana kwa watu waliohusiana na maabara za Marekani. Swali kuwa watu hao walipata matatizo hayo kutokana na nini linaonekana kupuuzwa au kuonekana halina umuhimu.
Inawezekana kuwa hoja ya kufanya utafiti kuhusu uwezekano wa virusi kuvuja kutoka maabara ina mashiko. Na kama ni kweli kwa sasa utafiti huo unatakiwa kufanyika, isiwe na eneo moja tu linalotakiwa kufanyiwa uchunguzi, maeneo yote yanayotia mashaka yanatakiwa kufanyiwa uchunguzi huru.