SoC04 Nimeota ndoto: Mfumo wa Tehama utakaothibiti urasimu

SoC04 Nimeota ndoto: Mfumo wa Tehama utakaothibiti urasimu

Tanzania Tuitakayo competition threads

i_denyc

New Member
Joined
Jun 6, 2023
Posts
4
Reaction score
8
MFUMO WA TEHAMA UTAKAODHIBITI URASIMU KWENYE SEKTA YA HAKI

UTANGULIZI

Mimi ni kijana ninaesomea sheria hapa Tanzania. Mwezi uliopita nilijitolea kwenye kliniki ya msaada wa sheria kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo. Huko nilipata kuona changamoto za watu wasiojiweza na wenye kipato cha chini katika kuifikia haki kwa wakati. Kwa mfano, kuna siku nilisikiliza malalamiko ya Mama Mbede (68) ambae mwanae alihukumiwa kifungo kwa kosa ambalo hakulifanya hivyo mama huyu alikusudia kuikatia rufaa hukumu hio. Kila alipofuatilia jalada la kesi hio kwenye ofisi za taasisi za haki jalada lilipopita kabla ya kuifikia hukumu, alichokipata ni danadana tuu, ataambiwa njoo kesho, mara jalada lipo ofisi flani na ukienda huko wanamwambia jalada lime "fowadiwa" ofisi nyingine. Siku zinapita, kutokana na hali ya afya na uchumi wa huyu mama jitihada zake za kukata rufaa ziligonga mwamba. Hapa ndipo wazo la kuunganisha mifumo ya TEHAMA ya taasisi za haki liliponijia.

NDOTO
Jioni kabla ya kulala nilitafiti: Ni kwa namna gani mifumo ya TEHAMA inaweza kuunganishwa na kusomana ili kuwanufaisha watu wenye hali kama ya Mama Mbede waliokosa haki kutokana na urasimu wa mfumo wa upatikanaji haki uliopo?. Na baada ya kumaliza kutafiti nililala kwa uchungu kwa kujua nimepata suluhu ila sina pa kuiwasilisha. Usiku ule niliota ndoto nimealikwa kuhudhuria mkutano wa wavumbuzi katika sekta ya haki ulioandaliwa na Jaji mkuu ambapo wataalamu kutoka nyanja mbalimbali waliwasilisha mawazo yao ya kuboresha upatikanaji haki. Ilipofika zamu yangu niliwasilisha yafuatayo;-
WASILISHO
Awali ya yote nikushukuru Mh. Jaji mkuu kwa kunipa fursa hii. Mapendekezo yangu yanalenga kutumia fursa za mapinduzi ya nne ya viwanda zilizopo zinazomfaa mtumiaji ambazo zitasaidia kuziba pengo la ufikivu wa haki kwa watu wenye hadhi zote na kwa wakati fasaha.

Mh Jaji, Machi 2024 Tanzania ilikua mwenyeji wa mkutano wa Mawaziri wa sheria wa Jumuiya ya Madola ambapo nchi ya Rwanda ilipewa tuzo iliotokana na mipango ya kipekee ya uvumbuzi wa mfumo jumuishi wa TEHAMA unaowezesha upatikanaji haki kwa watu wote na kwa wakati (Intergrated Electronic Case Management System) ulioanzishwa 2016. Huu ni mfumo unaoziunganisha taasisi zote za upatikanaji haki, maridhiano, sheria na uratibu. Vile vile mfumo huendesha michakato ya mahakama kiotomatiki na hutoa kila taasisi kiolesura kilichoboreshwa kwa ajili ya kufanya kazi zake. Inatumika kama sehemu moja ya kuingilia kwa kurekodi na kupata habari za kesi na kushiriki habari kwa ufanisi kati ya taasisi za sekta. Mbali na hii tuzo, mfumo huu pia umeshinda tuzo mbili nyingine, tuzo ya ubunifu kutoka kwa Chama cha Kiafrika cha Usimamizi wa Utawala wa Umma 2016 pamoja na tuzo kumi bora za suluhisho la teknolojia ya kimahakama kutoka kwa Jumuiya ya kimataifa ya utawala wa mahakama.

Mh Jaji, ninahimiza sana upitishwaji wa mfumo huu wa jukwaa la pamoja litakalotumiwa na taasisi zote za haki hapa Tanzania kwani kumekuwepo na changamoto za kimifumo zinazotokana na taasisi ya sekta ya haki kutosomana hivyo kusababisha urasimu kwa watumiaji. Mfumo huu utajumuisha taasisi za haki kama jeshi la polisi, ofisi ya mwendesha mashtaka, TAKUKURU, DCEA, Jeshi la Magereza na Mahakama. Hii itasaidia kubadilishana kwa taarifa baina ya hizi taasisi kwa manufaa ya ufikivu wa haki kwa wakati. Utekelezaji wa mfumo jumuishi wa kusimamia kesi za kielektroniki (IECMS) nchini Tanzania utahitaji mbinu iliyoratibiwa vyema na ya awamu nyingi. Ifuatayo ni ramani ya kina ya jinsi mfumo unavyoweza kuletwa kwenye matumizi hapa nchini;-​
  • Tathmini na kushirikisha wadau,​
    mahakama inatakiwa kufanya tathmini kamili ya mahitaji ya watumiaji wa huduma zake kujua ni wapi kuna changamoto na kipi cha kubadilisha kwenye miundombinu ya mfumo mpya wa IECMS. Ushirikishi wa washikadau wote wa mahakama wakiwemo mawakili, jeshi la polisi,tume ya kurekebisha sheria, ofisi ya waendesha mashtaka na asasi za kiraia. Kuunda kikosi kazi chenye wawakilishi kutoka kila kikundi cha washikadau ili kusimamia utekelezaji.​
  • Mpango kazi, baada ya kujifanyia tathmini ya changamoto mahakama inatakiwa kujiwekea malengo yanayopimika inayoyatarajia baada ya mfumo kuanza kutumika. Malengo kama vile kumaliza mlundikano wa kesi zinazokwamishwa na urasimu wa taasisi za haki na kuboresha uwazi wa mwenendo wa mashauri. Mahakama ianzishe utekelezaji wa awamu ambao utachagua eneo au baadhi ya mahakama za majaribio na kisha baadae kuongeza wigo wa eneo au mahakama hatua kwa hatua.​
  • Maboresho ya miundombinu ya teknolojia, muunganisho wa intaneti katika ofisi za mahakama na ofisi nyingine za taasisi za haki unatakiwa uwe imara. Viunzi muhimu kama kompyuta, seva na printa vyenye uwezo mkubwa wa kupokea na kukusanya taarifa ni muhimu kwenye maboresho ya miundombinu. Mfano wa tovuti ya mfumo ambayo itajumuisha vipengele muhimu kama vile uhifadhi wa jalada mtandaoni, ufuatiliaji wa kesi hatua kwa hatua kwenye ofisi za taasisi za haki mbali mbali kwa njia ya kiotomatiki.​
  • Mafunzo kwa watumishi na watumiaji, programu za mafunzo ya kina kwa majaji, watumishi wa mahakama, wanasheria na washikadau wengine juu ya matumizi ya mfumo mpya. Mahakama itaanzisha kampeni za uhamasishaji umma kuhusu matumizi ya IECMS bila kusahau kutoa nyenzo zitakazosaidia watu wasiojiweza kwenye vituo vya haki.​
FAIDA ZA MFUMO
  • Ni kituo jumuishi cha ofisi zote za taasisi ya haki​
  • Kupungua kwa mlundikano wa kesi​
  • Ongezeko la watumiaji wa huduma​
  • Ongezeko la imani ya wadau wa haki​
Mh Jaji, namalizia kwa kusema mbali na faida nyingi tutakazozipata kwa kutumia mfumo huu, usalama wa mtandao ni swala la msingi ili kulinda taarifa nyeti. Kuingia makubaliano na wakandarasi wenye viwango vya kimataifa kama Synergy pamoja na kuongeza maslahi ya watumishi wa TEHAMA mahakamani kutasaidia kudumisha usiri unaohitajika kwenye mfumo huu. Asanteni.

Nilimaliza kuhitimisha. Mkutano ulivyoisha nilipata wasaa wa kuongea na Mh Jaji mkuu ambapo alisema “Wasilisho lako linaweza kuwa hatua muhimu mbele katika kufanya haki ipatikane zaidi na kwa usawa miaka ya mbeleni”. Na mara baada nilishtuka usingizini.​
 
Upvote 5
Back
Top Bottom