Nimevua pendo langu

Nimevua pendo langu

tamu 3

Member
Joined
Dec 11, 2024
Posts
63
Reaction score
122
NIMEVUA PENDO LANGU

Sitokuja penda tena, katika maisha yangu,
Nilimpenda Amina, kipenzi cha moyo wangu,
Tukaja tukaoana, kutimiza lengo langu,
Nimevua pendo langu, sitokuja oa tena.

Binti kutoka Singida, aliniteka moyoni,
Alikuwa hana shida, kumpokea rohoni,
Kwao wa pekee dada, walobaki kiumeni,
Nimevua pendo langu, sitokuja oa tena.

Likuja kwetu nyumbani, kazi kutusaidia,
Dada wa kazi za ndani, vizuri litufanyia,
Sote tukampendeni, wazazi na mimi pia,
Nimevua pendo langu, sitokuja oa tena.

Amina cheupe dawa, hakika alivutia,
Sio siri lipagawa, sera zangu nikatoa,
Mwanzoni hakuelewa, kila nilipomwambia,
Nimevua pendo langu, sitokuja oa tena.

Nikanza tabia mbaya, usiku kikaribia,
Naanza kuchunguliya, Amina mejilalia,
Nguo zote metupiya, hata ile hajavaa,
Nimevua pendo langu, sitokuja oa tena.

Siku alipogunduwa, kuwa namchunguliya,
Naye akanielewa, mchezo tukazoeya,
Wazazi waligunduwa, lionywa hii tabiya,
Nimevua pendo langu, sitokuja oa tena.

Nikawa mimi mbishi, sijui la kuambiwa,
Nilipenda lake pishi, kwangu anapoligawa,
Pamoja lianza ishi, tayari nimeshaowa,
Nimevua pendo langu, sitokuja oa tena.

Maisha kiwa ndoani, mwanzoni lifurahia,
Watoto liwazaeni, ni wawili idadia,
Siku ziliposogeni, akabadili tabia,
Nimevua pendo langu, sitokuja oa tena.

Akabadili tabiya, akienda kupombeka,
Kila ninalomwambiya, yeye anakasirika,
Kazidisha umalaya, kabisa mebadilika,
Nimevua pendo langu, sitokuja oa tena.

Ugonjwa akaukwaa, tena usio tibika,
Ni ugonjwa wa zinaa, tabibu alitamka,
Akaanza kuugua, mwilini atetemeka,
Nimevua pendo langu, sitokuja oa tena.

Tarehe kama ya leo, mwaka ulotangulia,
Nyumbani kuna kilio, Amina amejifia,
Hakuwa na masikio, kipindi namuusia,
Nimevua pendo langu, sitokuja oa tena.

Nami nimeathirika, sina budi kulisema,
Moyoni nina mashaka, watoto nitawahama,
Kuoa tena mechoka, siwatamani wamama,
Nimevua pendo langu, sitokuja oa tena.

Denny Jeremias kitumbika
Mtunzi wa mashairi na ngano za Kiafrika
Mufindi Tanzania 10/11/2024
 

Attachments

  • 1734198449051.jpg
    1734198449051.jpg
    272.6 KB · Views: 2
Back
Top Bottom