Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
Maelezo kuhusu taarifa
Simu ya Mahmoud Shaheen iliita alfajiri. Ilikuwa Alhamisi tarehe 19 Oktoba karibu saa 12:30, wakati Israel ikiendelea kuishambulia Gaza kwa siku 12 mfululizo.
Akiwa katika ghorofa ya tatu, kwenye nyumba ya vyumba vitatu vya kulala huko al-Zahra. Ghafla alisikia kelele kutoka nje, "mnatakiwa kuondoka, watashambulia," mtu alipiga kelele kutoka barabarani.
Alipoteremka ghorofa na kuvuka barabara, akitafuta sehemu salama, simu yake ikaita. Ilikuwa nambari ngeni.
"Ninazungumza na wewe kutoka intelejensia ya Israel," mwanaume huyo alisema baada ya Mahmoud kupokea. Alizungumza kiarabu safi kabisa na kumtaja Mahmoud kwa majina yake kamili.
"Aliniambia watalipua majengo matatu ya ghorofa na kuniamuru niondoke eneo hilo."
Ghorofa ya Mahmoud haiukuwa katika tishio la kushambuliwa, lakini aliwajibika kuwahimiza mamia ya watu kuondoka.
Akamsikiliza na kumwambia yule mtu aliyejitambulisha kwa jina la Abu Khaled, asikate simu.
Mahmoud ni daktari wa meno mwenye umri wa miaka 40, alipiga kelele hadi koo lake likamuuma akitaka watu wakimbie. Alihamisha kwa kiasi kikubwa majirani zake.
Wakati wa mzozo huu, jeshi la Israel limewapigia simu wananchi wa Gaza baadhi ya nyakati kuwaonya kabla ya mashambulizi ya anga, Mahmoud anaelezea moja ya simu hizo.
BBC iliwasiliana na Mahmoud baada ya wakazi wa al-Zahra kumtambua kuwa ndiye mtu aliyepokea simu ya onyo.
Siku hiyo mamia ya watu waliachwa bila makazi wakati jeshi la Israel liliposhambulia kwa mabomu takribani makazi 25 na kuharibu mtaa mzima. Watu walilazimika kukimbia na vitu vichache na hatimaye wakatawanyika kote Gaza.
IDF inasema inalenga maeneo ya kijeshi ya Hamas na hufanya hivyo kwa kufuata "vifungu vya sheria za kimataifa."
Mlipuko wa Onyo
Baadhi ya watu walijihifadhi katika chuo kikuu cha Palestine
Watu walio karibu na Mahmoud walionya kuwa simu hiyo inaweza kuwa ya uwongo. Tangu vita vimeanza kumekuwa na simu za uongo za maonyo.
Mahmoud alimuomba mtu kwenye simu kufyatua mlipuko wa onyo ili kuthibitisha onyo ni la kweli. Ikiwa wale ambao bado wamelala hawakusikia mayowe kutoka mitaani basi mlipuko huo watausikia.
Mlipuko wa onyo huenda ulitoka kwenye ndege isiyo na rubani, uligonga moja ya jengo.
"Nilimuomba afyatue mlipuko mwingine wa onyo kabla ya kulipua," Mahmoud anasema. Kisha alimuomba mtu huyo awe na subira. "Nilimwambia: 'Usitusaliti na kupiga bomu wakati watu bado wanahama.''
Mtu huyo alisema atawapa muda wa kutosha, alisema hataki mtu yeyote auawe. Aliendelea kuzungumza katika simu huku akizunguka katika kitongoji hicho akiwataka watu wahame. Kisha watu wengine wakajiunga naye kupiga mayowe.
Mamia ya watu walimiminika mitaani asubuhi hiyo. Wakazi wa jiji hili ambalo kwa kawaida lilikuwa na amani walikuwa wakipiga kelele na kukimbia, baadhi yao wakiwa wamevalia nguo zao za kulalia au nguo za maombi.
Mahmoud hakuweza kuelewa ni kwanini mtaa wake umekuwa shabaha. "Nilijaribu niwezavyo kumzuia. Niliuliza, 'kwanini unataka kupiga bomu?'
"Akasema, 'Kuna baadhi ya mambo ambayo tunayaona wewe huyaoni."
Kwa mujibu wa Mahmoud, mwanaume huyo alisema, "ni amri kutoka kwa watu wakubwa kuliko mimi na wewe, na tumepewa amri ya kulipua," mwanaume huyo alisema.
Maeneo hayo yalipoonekana hayana tena mtu, alimtaarifu Mahmoud kuwa mlipuko wa mabomu utaanza.
Baada ya mlipuko, Mahmoud anakumbuka sauti ikimwambia: "Tumemaliza, unaweza kurudi."
Simu nyingine
Jioni ya siku hiyo, baada ya Mahmoud kumaliza swala Isha, au sala ya usiku. Aliona simu ambayo hakuwa ameipokea kutoka namba ngeni. Muda si muda simu yake ikaita tena.
Mahmoud wa upande mwingine kwenye simu alimwambia majengo zaidi yatapigwa mabomu usiku huo, na daktari huyo atahitajika kuamuru majirani zake kuhama kwa mara nyingine tena.
Mwanzoni, aliambiwa shabaha ni majengo mawili karibu na yale matatu ambayo yalikuwa yameharibiwa asubuhi hiyo.
"Aliniambia, 'Tunataka uwajulishe watu wahame eneo hilo,' nami nikasema, Nipe muda.'
Mahmoud aliendelea kujitahidi kuomba muda kadiri ya uwezo wake, huku akiongea na mtu aliyejiita Daoud, hadi watu wote wakawa wameondoka eneo lile.
Majengo matatu yaliharibiwa. Huku Mahmoud akitazama uharibifu huo. Ghafla mabadiliko ya amri yalikuja ghafla. Watapiga bomu safu nzima ya nyumba za upande wa mashariki mwa barabara, Mahmoud anakumbuka kuambiwa.
"Kuna watu ambao tulikuwa hatujawahamisha bado kwa sababu hakukuwa na onyo kuhusu majengo hayo. Nilimwambia. Angalau tupe hadi asubuhi, wakati wa usiku, watu watakwenda wapi?'
"Jibu lilikuwa, 'tutapiga mabomu ndani ya saa mbili."
Mahmoud alipiga kelele watu waondoke eneo hilo. Wakazi wanaelezea matukio ya fujo watu wakipiga kelele na watoto wakilia. Baadhi ya wazazi na watoto walipotezana.
Pamoja na hofu hiyo, Mahmoud alibaki kwenye simu muda wote akijitahidi kuchelewesha shambulio hilo la bomu.
Sauti ya upande wa pili ilisema, ‘una muda wa kutosha. Sitapiga bomu isipokuwa unipe ruhusa.'
“Nikasema kwa ruhusa yangu sitaki upige bomu, ukitaka nihame nitahamisha kwa usalama wa wananchi, lakini ukitaka kupiga bomu usiniambie unahitaji ruhusa yangu.'
Yeye na wengine pia walikuwa na wasiwasi kuhusu nyumba ya kulea wazee. Lakini mtu aliyepiga simu alisema "atapiga tu majengo ya makazi.
Uharibifu mkubwa
CHANZO CHA PICHA,QUTAIBA KOLTHOUM
Maelezo ya picha, Watu wakisubiri nje
Mahmoud anasema kile alichoshuhudia yeye na majirani zake usiku huo "halikuwa shambulio dogo" bali "uharibifu mkubwa wa majengo."
Mkazi mmoja akiongea na BBC kupitia ujumbe wa WhatsApp. "Hatukujua tunapaswa kwenda wapi, wengine walisema lazima twende shule, wengine walisema tunapaswa kwenda Al Nuseirat [kambi ya wakimbizi kusini mwa kitongoji hicho."
Mahmoud alimuuliza yule mtu kwenye simu apeleke wapi majirani zake.
"Akasema, ' waende Mashariki au Magharibi.' Nikasema, 'Kuwapeleka Mashariki itakuwa ngumu, kwa sababu upande wa mashariki wa al-Zahra ni Al Mughraqa, eneo ambalo tayari si salama. Watu walikuwa tayari wanaogopa kwenda huko. '
"Aliniambia, 'Wapeleke Magharibi hadi Mtaa wa Palestina'. Nilipendekeza Chuo Kikuu cha Palestina na akasema, ndio."
Mahmoud aliongoza umati huo, ambao ulijumuisha sio tu wakaazi wa majengo hayo, lakini pia watu wengine waliokimbia makazi yao nawalikuwa wametafuta makazi huko al-Zahra baada ya kukimbia makazi yao mahali pengine.
Wakazi wengine wamethibitisha kwamba walienda chuo kikuu, na video iliyowekwa Facebook inaonyesha watu wakitembea na kuendesha gari kuelekea huko.
Mahmoud anasema watu walisubiri chuo kikuu kwa hofu, wakisikiliza mshindo wa milipuko. Mbwa waliokuwa na hofu mitaani walijaribu kutafuta mahali pa kulala kati ya wanawake na watoto.
Wakati fulani, Mahmoud anasema sauti kwenye simu ilimuuliza amebakisha chaji kiasi gani. Ilikuwa na 15%. Walimwambia akate simu ili kuihifadhi chaji na watampigia tena.
Simu za mara kwa mara
CHANZO CHA PICHA,QUTAIBA KOLTHOUM/GETTY IMAGES
"Walinipigia simu kuniambia, 'Sasa tutalipua jengo jingine,' 'Sasa tutalipua jingine.' Walisema, 'Tutaendelea kupiga simu hadi tutakapomaliza,'" Mahmoud anasema.
Umati ulimtazama Mahmoud kwa majibu. "[Walikuwa] wakisema 'daktari, walikupigia simu ili turudi? Je, walikuambia watapiga wapi?'
Mahmoud na yule mtu aliyejiita Daoud waliendelea kuzungumza hadi mitaa ikatulia. Kisha simu ikakatwa bila ya maelekezo.
"Hawakutuambia turudi majumbani mwetu, au tuhame au tuondoke eneo hilo. Kwa hiyo watu walisubiri hadi saa sita mchana, na ndipo wakaanza kurudi," Mahmoud anasema.
Katika saa na siku zilizofuata, watu WA al-Zahra, kama wengi wa Gaza, walisambaratika.
"Hata kwa watu ambao nyumba zao bado zimesimama, hakuna huduma zilizobaki, mifumo ya maji taka imeharibika, hakuna duka la mikate, hakuna maji, hakuna umeme," Mahmoud anasema.
Ameipeleka familia yake katika eneo jingine la Gaza, anakaa katika nyumba ya rafiki yake ambayo ina watu wengi. “Sifikirii zahanati yangu wala nyumba yangu, naomba tu niishi na niendelee kuwa hai,” anasema.
Israel huwaonya raia wa Gaza kwa kuwapigia simu, kuwatumia ujumbe mfupi wa simu na kuwaangushia vipeperushi kabla ya kushambulia kwa mabomu. Lakini katika baadhi ya matukio, raia wanasema hawaonywi.
chanzo. 'Ninapiga simu kutoka intelijensia ya Israel. Tutapiga bomu, una saa mbili za kuondoka’ - BBC News Swahili