Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
NINAVYOMKUMBUKA BABA WA TAIFA MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE
MWALIMU MTU WA WATU 2
MWALIMU MTU WA WATU 2
Mwalimu alikuwa mtu kutoka bara, Mkristo Mkatoliki.
Alianza siasa hasa za kudai uhuru wa Tanganyika katika mazingira ya Dar es Salaam akiwa kazungukwa na Uislam na Waislam.
Kulikuwa na tofauti kubwa katika ya kiongozi huyu na wale aliokuwa akiwaongoza.
Siku hizo Mwalimu kijana mdogo wa miaka 30.
Kivazi chake kilikuwa kaptula na siksi ndefu, stokingi.
Mavazi rasmi ya wasomi.
Katika TAA, Mwalimu aliwakuta vijana wengine kama Abdul na Ally Sykes, Hamza Mwapachu, Steven Mhando na Zuberi Mtemvu.
TANU ilipoundwa mwaka wa 1954 kukawa na baraza la wazee chini ya Sheikh Suleiman Takadir.
Baraza hili lilijumuisha wazee wengi maarufu wa mjini na masheikh. Katika hali kama hii ungejihisi kuwa Mwalimu yupo ugenini.
La hasha, Mwalimu alienea vyema katika kundi hili la Waswahili na masheikh.
Mwalimu aliwanyenyekea na kuzungumzanao katika lugha waliyoielewa. Mwalimu akizungumza Kiswahili safi na fasaha bila ya lafidhi ya kwao Musoma.
Kwa aliyekuwa hamfahamu Mwalimu ilikuwa vigumu kuweza kujua kama alikuwa Mzanaki wa Musoma, tena vijijini.
Mwalimu aliwavutia zaidi wazee wale kwa ustadi wake wa kucheza bao.
Sehemu za pwani mchezo wa bao kwa kawaida ni mchezo wa wazee.
Aghlabu vijana kuucheza mchezo huu.
Wazee wa tano wengi wao walikuwa wapenzi wa bao.
Mchezo wa bao ni mchezo wa kupanga mikakati na kupiga hesabu namna ya kumpiku mpinzani wako.
Mwalimu alilimudu sana bao.
Wazee wa TANU walimuheshimu sana Mwalimu walipokuja kugundua kuwa alikuwa bingwa wa kete.
Kati ya marafiki zake katika enzi zile walikuwa wapinzani wake wakubwa katika bao,
Mzee Mshume Kiyate, Mwinjuma Mwinyikambi, Boi Singizi, Jumbe Tambaza na wengine wengi.
Picha inamuonyesha Mwalimu Nyerere akiwa na Mshume Kiyate kulia Max Mbwana na Mwinjuma Mwinyikambi na hiyo nyingine ni Ally Sykes na Julius Nyerere.