Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
NINAVYOMKUMBUKA BABA WA TAIFA MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE
MWALIMU MTU WA WATU 3
MWALIMU MTU WA WATU 3
Mwalimu kama vile alivyokuwa bingwa wa kupanga mikakati katika mchezo wa siasa dhidi ya mbinu za Gavana Edward Twining, vilevile alikuwa hodari wa kupanga kete zake dhidi ya rafiki yake Kiyate Mshume.
Wenzake hawakuwa na kipaji wala subra kama hii aliyokuwanayo Mwalimu.
Vijana wenzake katika harakati hawakuweza kufanya aliyokuwa akifanya Mwalimu.
Hawakuwa na muda wa kukaa na kucheza bao na wazee. Walihisi kuwa huo haukuwa uwanja wao.
Si Hamza Mwapachu, Abdulwahid Sykes na Ali Mwinyi Tambwe waliowaza kupumzisha akili zao kati ya wazee wa TANU kwa kucheza bao.
Kwao wao harakati ilikuwa kuhangaisha bongo zao kwa kuandika fikra zao na kubadilishana mawazo na wasomi wenzi wao wengine ikiwa pamoja na Wazungu kama akina John Hatch na Kathleen Stahl wa Chama cha Labour cha Uingereza.
Hawa walikuwa siasa kali wasomi wa Kiingereza na wanaharakati wa mrengo wa kushoto wa Fabian Society ndani ya Labour Party.
Ingawa Mwalimu aliyafanya haya yote na kwa ufanisi mkubwa sana, lakini hakuona tabu kukaa chini kwenye jamvi ama akila chakula na hawa wazee au akicheza bao au wakibarizi tu.
Mwalimu alikuwa nyumbani aidha akimwaga umombo na Abdul Sykes, Hamza Mwapachu, Steven Mhando, Dr. Vedasto Kyaruzi, Dr. Luciano Tsere au Dr. Wilbard Mwanjisi katika moja ya migahawa mikubwa ya Dar Salaam kama Cosy Cafe au akiwa mitaa ya Uswahilini akizungumza na rafiki yake Shaban Gonga au Juma Mlevi, vijana wa TANU Youth League, au akiwa ndani ya madras ya Mufti wa Tanganyika Sheikh Hassan bin Ameir,
Ukimkuta Mwalimu pale New Street nyumba na. 25 katika nyumba zile za zamani za TANU akipiga soga na wananchi, huwezi kutambua kuwa alikuwa msomi wa Makerere na Chuo Kikuu Cha Edinburgh, Uskochi na Mwafrika wa kwanza kupata shahada ya pili.
Sanasa unaweza kudhani kuwa alikuwa kijana wa mtaa wa jirani pale amekuja ofisi ya TANU kuzungumza.
Picha ya kwanza Julius Nyerere na Kiyate Mshume na ya pili ni Cosy Cafe kama ilivyokuwa katika miaka ya 1950.