Ninavyomkumbuka Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwalimu mtu wa watu 4

Ninavyomkumbuka Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwalimu mtu wa watu 4

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
NINAVYOMKUMBUKA BABA WA TAIFA MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE
MWALIMU MTU WA WATU 4​

Mwalimu ameingia kaburini kama mtu aliyekuwa hana majivuno si kwa cheo chake au elimu yake.
Huyu ndiye Mwalimu wakati alikuwa mtu wa watu.

Mwalimu hakuthamini mali kwa hiyo alikuwa aghali sana.
Hakuna mnada ulioweza kumwekea bei.

Katika miaka ya 1970 Benki ya Kiswisi maarufu kwa kuhifadhi fedha za viongozi wa Afrika walimletea Mwalimu barua wakimtahadharisha kuhusu matatizo ya serikali za Kiafrika na mikosi ya kupinduliwa viongozi.

Walimuomba Mwalimu aweke fedha zake huko kwao ili zije kumfaa siku za baadae.
Benki hii ilimpelekea Amir Jamal barua kama hii pia.

Mwalimu aliiadhiri benki hiyo.

Barua yao hiyo aliichapa ukurasa wa mbele wa Daily News gazeti la serikali.
Jambo kama hili lilikuwa halijapata kutokea kwa viongozi wa Afrika.

Wengi wao waliuthamini ushauri ule na kupenyeza fedha ili zihifadhiwe huko.
Mwalimu alikuwa mtu maridhia na mwepesi sana katika maisha yake.

Kuna wakati mwandishi mmoja alistaajabu na akaandika kuwa alipofika nyumbani kwa Mwalimu kufanya mahojiano alishangazwa na jinsi nyumba yake ilivyokuwa tofauti na jinsi alivyofikiria.

Ilikuwa nyumba ya kawaida na yenye samani za kawaida tu.

Kubwa zaidi ni pale Mwalimu katika kumkirimu, watumishi wa Mwalimu waliokuwa katika mavazi ya kawaida sana walipompa maji ya matunda yaliyokuwa si baridi.

Alishindwa kutambua kama jiko la Mwalimu lilikuwa halina jokofu.

Mwalimu akisoma makala hizi katika magazeti ya nje na akaruhusu makala hizo zichapwe katika Daily News, chini ya anuani, ''What They Say About Us.''

Vitu hivi havikuwa vikimuhangaisha Mwalimu.
Utu wake hakuwa ameupa thamani ya vitu.

Wanaomfahamu Mwalimu na waliokuwa karibu nae wanasema Mwalimu hakuwahi kutia hata shilingi moja ndani ya mfuko wake kwa matumizi, si yake binafsi wala ya familia yake.

Si akiwa nyumbani au nje ya nchi.
Fedha ikifika kwa Mwalimu ilikosa thamani.

Vitu vilikuwa na umuhimu tu kwa ile kazi ya lazima iliyokusudiwa ndani ya vitu hivyo.
Hakutumia vitu kwa kupata starehe ya kutumia.

Kwa ajili hii hata nguo alizokuwa anavaa zilikuwa kwa kuwa zinasitiri maungo.
Hakuvaa kwa kuiridhisha nafsi.

Kuna kisa cha viongozi wenzake waliokuwa wakishonewa nguo zao uniform tena za kijeshi na kampuni mashuhuri ya Kifaransa ya mitindo - Pierre Cardin.

Mwalimu alikuwa akicheka hadi machozi yanamtoka alipokuwa akisoma visa kama hivi.

Akiwa Ulaya Mwalimu hakuwahangaisha wasaidizi wake kwa kuwaelekeza wamnunulie suti nzuri za mitindo au nguo kwa mkewe na wanae.

Hakuwa na muda huo.
Hakuwa anapokea zawadi ya aina yoyote na hili wengi walilitambua.

Zawadi aliyokuwa akipokea ilikuwa vitabu.
Mwalimu alirudi nyumbani kutoka safarini kama alivyokwenda.

Kitakachozidi kwake kitakuwa ni makaratasi ya mikutano.

Wengi watashangaa, inasemekana Mwalimu katika maisha yake hakupata kujifunza kuendesha gari hata pale TANU ilipokuwa inao uwezo wa kumnunulia usafiri wake mwenyewe.

1570994319690.png

Nyerere na Amir Jamal
 
Back
Top Bottom