Ninavyoukumbuka Ubunge wa Profesa Mwandosya, Busokelo

Ninavyoukumbuka Ubunge wa Profesa Mwandosya, Busokelo

Peter Stephano 809

Senior Member
Joined
Feb 29, 2020
Posts
120
Reaction score
162
"Kila jambo lina wakati wake" ni maneno ya wahenga na vitabu vya dini.

Ingawaje Kuna wakati jambo huanza kwa uzuri na kuisha kwa ubaya kulingana na Vikwazo vikivyopo ukingoni.

Yote hayo ni matokeo tu lakini inabaki kuwa kila jambo lililo jema hubaki kwenye kumbukumbu vizazi hata vizazi.

Unamkumbuka msomi Prof. Mark Mwandosya aliewahi kuogoza wizara mbalimbali Kama waziri kisha kugombea kiti kuwania urais uchaguzi mkuu wa 2015 kabla ya jina lake kukatwa ndani ya CCM? Huyu Mwandosya aliyewahi kuwa mkuu wa chuo Cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) na msomi wa kiwango cha juu nchini.

Huyu ndiye aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Rungwe mashariki Sasa jimbo la Busokelo mkoani Mbeya. Huyu ndiye anaezungumzwa hapa.

Iko hivi kabla ya kustaafu shughuli za kisiasa baada ya uchaguzi mkuu wa 2015, Mwandosya alikuwa mbunge wa Busokelo Wakati wa Uongozi wake aliweka historia ya kuwa mbunge aliyekaa muda mrefu zaidi kuliko watangulizi wake 2000-2015.

Katika kipindi chote hicho Mwandosya hakuwahi kukutana na upinzani ndani ya chama chake Cha CCM wala nje ya chama.
Mwandosya alilitumikia jimbo lake kwa hali na mali kila alipohitajika. Aliweka utaratibu wa kutembea kila kata kila Kijiji mara tu alipopata muda baada ya bunge ili kujua mahitaji ya watu wake.

Kipindi cha Uongozi wake msafara wake ukipita wananchi walijitokeza kwa wingi kumpingia mkono barabarani pasipo kushinikizwa.
Alipotakiwa kusimama ili awasikilize alisimama na kuwasalimia pamoja na kusikiliza kero zao.

Mwendo wa magari ya Msafara wake ulikuwa wa kawaida Sana kwani alitambua kuwa anatembea ndani ya jimbo lake Wala hapiti ugenini.

Uongozi wa Mwandosya ndio ulionipa hamasa ya kufikiria kuwa wasomi ni watu muhimu kwenye jamii iliyochanga.

Nakumbuka mara kwa mara alipopita kijijini Kwetu alipoona Msiba alisimama kuwafariji, alipoalikwa kwenye harambee ya kuchangia maendeleo hakusita kuja yeye mwenyewe na sio kutuma wapambe wake. Alipofanya ziara nje ya nchi alirudi na Zawadi kwa wananchi wa jimbo lake Wala hakuenda huko kwa manufaa yake binafsi.

Nakumbuka Kuna mwaka alisafiri nje ya nchi alivyorudi nikaliona gari limebeba vifaa vya huduma za afya baadae nikasikia ilikua Ni matunda ya ziara yake nje ya nchi. Mwandosya alithubutu kutoa hela yake binafsi pale alipoona wananchi wanahitaji msaada kwenye jambo fulani.

Hii leo unasikia "Madarasa ya Mama Samia" unashangaa? Mimi Nilisikia na kuona "Madarasa ya Mwandosya" mengi Sana katika shule nilizosoma na mpaka leo imara yamebaki kumbukumbu. Nani anakumbuka ujenzi wa shule Kama Bujesi, Kisegese na Mbigili Sekondari aniambie hamkumbuki Mwandosya?

Mimi nakumbuka mengi Sana nakumbuka ujenzi wa madaraja Kama Daraja la Kandete-Luteba na daraja la Tapio hizo zote ni juhudi za Mwandosya.

Mwandosya hakutaka utamaduni wa jamii yake upotee akajenga kituo cha makumbusho ya Kabila la wanyakyusa pale Lukasi kwakua ndio maeneo ulipo uchifu wa Wanyakyusa wa Busokelo. Mwandosya alihakikisha Uvunaji wa maji ya mito kwa kutandaza mabomba kila kata maji yakatiririka.

Haikua rahisi eneo lisilo na Watu wengi wala viwanda vingi kupata umeme lakini Mwandosya alihakikisha baadhi ya vijiji vya Busokelo vinapata umeme.

Ndio maana hata Mwakaleli umeme ulifika kabla ya karne ya 21. Mwandosya hakugawa rushwa wala kupiga bao la mkono alifanya kazi iliyo bora iwe kibali cha yeye kukubalika.

Hakuanza kazi akiwa màarufu Kama ilivyo kwa watangulizi wake Kama Eli Anangisye bali umahiri wake ukampa umaarufu.
Aliposikia mawasiliano ya Simu ni hitaji kubwa miaka ya 2000 alipambana na kuhakikisha minara ya Simu inajengwa Busokelo nilishuhudia mnara wa Celtel ukisimama Kijiji cha Mbigili na kufungua Mawasiliano ya simu kwa watu wa Mwakaleli.

Hakusubiri ifike muda wa kampeni ndio aje kufanya mikutano bali aliweka utaratibu wa mwaka kwa mwaka mpaka kieleweke na alisikiliza hoja kwa hoja kutoka kwa kila alietaka kuzungumza kuhusu jimbo lake.

Baada ya kufanya mengi ambayo sijayataja hapa Mwandosya aliona Busokelo inapaswa kuwa halmashauri ya wilaya na sio tarafa akapeleka ombi serikalini. Jitihada zake zikafanikiwa kiasi kwani Busokelo ikatambulika rasmi kuwa halmashauri Bali sio wilaya Kama alivyopendekeza.

Kwakua ilikosa vigezo Muhimu ikiwemo idadi ya watu, idadi ya tarafa 3 pamoja na vyanzo vya mapato ili iweze kuwa Wilaya.
Baada ya kufanikisha kupata halmashauri Busokelo ikapata chuo chake cha Ufundi stadi VETA, Ikapata makao makuu yake ya Halmashauri, Lwangwa.

Na ombi la kuunganisha Busokelo na Tukuyu Mjini kwa miundombinu ya barabara ya lami likakubalika na kwa mara ya kwanza ujenzi wa barabara kuu Tukuyu-Busokelo-Katumba ukaanza. Ramani ya ujenzi wa jengo kuu la utawala la halmashauri ya Busokelo ikachorwa ikatangazwa tenda ujenzi ukaanza.

Hakuna marefu yasiyokuwa na ncha hatimae siasa za uchaguzi mkuu wa 2015 zikapamba moto na Vijana wasaka ugali wakavamia jimbo, Mwandosya akapigania kiti cha urais.

Si mnajua kilichotokea baada ya hapo au niendelee lakini napo Siwezi kumaliza yote. Nikimpigia simu mbunge wangu ananipa dakika 2 za Kueleza shida yangu Kisha anakata simu kabla sijamaliza.

Naukumbuka Ubunge wa Mwandosya Busokelo.

Peter Mwaihola kitaaluma ni mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya kijamii.
 
Baada ya kichaa kushika madaraka Mzee akakaa kimyaa kulinda heshima yake.

Namkumbuka asingekuwa yeye songwe international airport isingejengwa ijapokuwa Bado haujaisha. Awamu ya tano ilihamisha pesa za songwe zikaenda chato.
 
Umenkumbusha Busokelo, mwaka 2015 ndo nilipata bahati ya kuitembelea kwa mara ya kwanza. Niliizunguka kata zake zote. Kipindi hicho kampeni za uchaguzi zinatengwa maeneo ya vilabu vya pombe maana watu wanapatikana huko zaidi. Ngoma za asili ilikuwa ndio burudani yake. Maji ya mito yanatirieika kila kona. Noah za Lwangwa kwenda Tukuyu watu mnajazana kwelikweli [emoji1787][emoji1787][emoji1787][emoji1787],barabara vumbi kweli. Nilikuwa na rafiki yangu mkubwa sana pale Lwangwa mashineni akifanya shughuli za kushona viatu,Joel Mwakitwangi,nmemkumbuka sana. Hapohapo Lwanga stand kulikuwa na mgahawa wa mke wa mwalimu maana vijijini walimu ndio watu maarufu,unapata mchemsho wa kuku na ndizi au viazi kwa 2500/= za Kitanzania.
Bucha za kitimoto ni nyingi kuliko za nyama ya ng'ombe,kila jumamosi gurio hapo Lwangwa hahaha
 
Umenkumbusha Busokelo, mwaka 2015 ndo nilipata bahati ya kuitembelea kwa mara ya kwanza. Niliizunguka kata zake zote. Kipindi hicho kampeni za uchaguzi zinatengwa maeneo ya vilabu vya pombe maana watu wanapatikana huko zaidi. Ngoma za asili ilikuwa ndio burudani yake. Maji ya mito yanatirieika kila kona. Noah za Lwangwa kwenda Tukuyu watu mnajazana kwelikweli [emoji1787][emoji1787][emoji1787][emoji1787],barabara vumbi kweli. Nilikuwa na rafiki yangu mkubwa sana pale Lwangwa mashineni akifanya shughuli za kushona viatu,Joel Mwakitwangi,nmemkumbuka sana. Hapohapo Lwanga stand kulikuwa na mgahawa wa mke wa mwalimu maana vijijini walimu ndio watu maarufu,unapata mchemsho wa kuku na ndizi au viazi kwa 2500/= za Kitanzania.
Bucha za kitimoto ni nyingi kuliko za nyama ya ng'ombe,kila jumamosi gurio hapo Lwangwa hahaha
Sasa Busokelo imechangamka Sana.
Karibu Tena mkuu wangu

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom