NINI KHASA TATIZO LA ZANZIBAR?

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
NINI KHASA TATIZO LA ZANZIBAR?

Na Harith Ghassany

Maridhiano ndio “Magna Carta”* ya Zanzibar. Maridhiano bado yamo ndani ya Katiba ya Zanzibar. Kinachokosekana ni viongozi WAPYA watakaoweza kulitatua tatizo la Zanzibar.

Lakini nini khasa tatizo (real diagnosis) la Zanzibar kwa sentensi moja? Ifikirie vizuri jawabu yako: ni ya kupakapaka (finyu) au yenye undani na mtazamo mpya?

Natamani Zanzibar ingelikuwa na viongozi wabunifu. Viongozi wabunifu ni wale ambao wana uwezo wa kuanzisha mchakato endelevu katika kuituliza Zanzibar na kuipa maendeleo ya haraka sana ya kielimu na kiuchumi. Wenye kuililia na kuitamania Zanzibar iwe Singapore au Dubai ya Afrika Mashariki na Kati ni wengi. Lakini wangapi wanaotwambia ukweli iwe pembeni au hadharani nini khasa tatizo la Zanzibar? Maana kulijua tatizo ni nusu ya utatuzi.

Rwanda wameweka kando roho mbaya na siasa za mivutano ili wajenge nchi yao. Zanzibar bado tunachechemea kwa kutoaminiana na kudanganyana.

Wananchi wa Zanzibar kwa asilimia kubwa wameshaliona hili, tuombe tupate viongozi wakweli ambao wataweza kulifanyia upasuaji wa kina na dawa ya kudumu gonjwa hili sugu lenye sifa ya donda ndugu, siasa mbovu na chafu zilizowazoelesha Wazanzibari kushindwa kutia nguvu zao zote katika kuijenga Zanzibar badala ya kutupiana maneno na kubaguana kusikokwisha.

Lakini kwanza: nini khasa tatizo la Zanzibar? Kweli ni visingiziyo vya Utumwa, Mapinduzi, Muungano (Tanganyika), vyama vingi, chaguzi, Katiba, vyama va siasa lazima kuwa vya Kitaifa, kutoaminiana kwa viongozi wa vyama vya kisiasa, suala la vyama kujiona wao wana haki na Zanzibar zaidi ya wengine, suala la vyama kutosikiliza sauti za wafuasi, hoja za dini, mivutano baina ya Wazanzibari walioko Zanzibar, au baina ya Zanzibar na Tanganyika, au baina ya CCM Zanzibar na wahajirina, kukosekana kwa umoja wa kijamii au umoja wa kitaifa, au kushindwa katika yote kwa kushindwa kuifahamu, kujifunza, halafu kuisahau historia na kuzielekeza nguvu zote za kijamii na kuziweka kwenye kulijenga Taifa la Zanzibar na la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?

Au tatizo la Zanzibar lina mizizi mirefu zaidi na kuongezewa kasi Zama za Siasa (kabla ya 1964), mizizi ambayo bado haijatambuliwa na kung'olewa na wasomi, vijana, na watawala wa 2018?

Fikiria vizuri kabla hujajibu kwa kuyarudia majibu ambayo tayari yanajulikana na ambayo yamekuwa wakielezwa Wazanzibari na wanasiasa wa pande ZOTE.

Tanzania Bara, Rwanda, Kenya, Eritrea, Ethiopia, wote wanabadilika na wanategemea kupata maendeleo makubwa ya kiuchumi. Wazanzibari hawakunasa. Viongozi ni wale wenye kufata uongozi na uongozi wa Zanzibar ni Maridhiano ambayo yametikiswa lakini hayajaanguka.

Nini khasa tatizo la Zanzibar? Usikurupuke na usikubali kukurupushwa. Na zaidi kama kweli tuna uchungu na tunaipenda Zanzibar basi tusikubali kudanganyana.

*Magna Carta (Great Charter) ni mkataba/ msingi wa ustaarabu wa nchi za Magharibi ambao ulitiwa saini Uiengereza na Mfalme John mwaka 1215. Ni Mkataba ambao ulisimamisha uwajibikaji mbele ya sheria akiwemo Mfalme...

July 9, 2018
 
Tatizo kuu la Zanzibar ni dhambi ya ubaguzi wa Ubwana na Utwana!.

Wenyeji asili wa Zanzibar ni Wahadimu wakiongozwa na Mwinyi Mkuu. Wareno wakaivamia Zanzibar kutaka kuitawala, Mwinyi Mkuu akaomba usaidizi wa Sultan Seyyid Said wa Oman kuja kuisaidia ili isitwaliwe na Mreno. Sultan akaitika wito akaja Zanzibar kumsaidia Mwinyi Mkuu, baada ya kukamilisha kazi aliyotumwa, Sultan Seyyid Said akahamia jumla Zanzibar na kuyahamisha makao yake makuu kutoka Oman hadi Zanzibar.

Only God knows kilichomkuta Mwinyi Mkuu, ila Sultan alipohamia Zanzibar jumla, alivitwaa visiwa hivyo na kuvigeuza ni mali yake as if havikuwa na wenyewe!. Alijimilikisha Ardhi yote na kushamirisha biashara ya utumwa, na huo sasa ndio ukawa mwanzo wa ubwana na utwana.

Wazalia wote wa Sultan waliofuatia, wakajisikia wao ndio mabwana na wakajiona wao pekee ndio wenye haki zote, na watwana kujisikia dhalili mbele ya mabwana!.

Wakati wa mikutano wa Berlin wa 1884 ulioitishwa na mtawala Otto Von Bismark wa Ujerumani, na kuigawanya Afrika kama mali yao, Zanzibar haikugawanya bali ilitambulika kama himaya ya Sultan wa Zanzibar. Baada ya ujerumani kushindwa vita kuu ya kwanza ya dunia, ikanyangwantwa makoloni yake yote, lakini Sultan wa Zanzibar akapewa hadhi ya ulinzi wa Waingereza, A British Protectorate.

Kipindi chote cha ulinzi, ndipo harakati za kisiasa zikaanza Zanzibar katika misingi ile ile ya ubaguzi, kukawa na vyama vya Kiarabu, Arab Associations, Vyama vya Washirazi, Shirazi Associations, na vyama vya Waafrika, Afro Associations. Waarabu waliendelea kujiuona bora, wakifuatiwa na Washirazi, huku Waafrika wenyewe wenye visiwa vyao, wakiwa ndio watu wa mwisho. Chaguzi zote zilionyesha matokeo ya mgawanyiko huo.

Ndipo chama chama cha Waafrika, African Association wakaungana na Shirazi Association kuunda Afro-Shirazi Party, hivyo hiki ndicho kikawa chama chenye nguvu kubwa sana, lakini sote tunajua kilichotokea kwenye matokeo ya uchaguzi wa December 1963, Zanzibar ikapewa Uhuru aliyepewa sote tunamjua, na kilichofuatia sote tunakijua, wenye nchi yao, wakaamua kufanya yao kuchukua kilicho chao.

Hali hii ndio iliyopo hadi sasa, kuna watu bado wanaamini Zanzibar ni mali yao na wamepokwa, na kuna watu wanajua for sure kuwa Zanzibar ni mali yao, bali walipokwa tuu, ndio maana wakapoka, na kila uchaguzi ukifanyika aliyeshinda tangu ile 1963, kila siku anashinda tena na kila siku anapokwa tena kwa sababu mzoea vya kunyonga, vya kuchinja haviwezi, ukiishazowea kupoka, utapoka tuu!, na wewe ambaye mwanzo ulipoka kwa wenyeji, na kujiona ni mali yako, mwenye mali alipokupoka, unaumia kwa kujiona umepokwa!.

Mzizi wa yote haya ni dhambi ya ubaguzi!, haya mengine yote ya Utumwa, Mapinduzi, Muungano (Tanganyika), vyama vingi, chaguzi, Katiba, vyama va siasa lazima kuwa vya Kitaifa, kutoaminiana kwa viongozi wa vyama vya kisiasa, suala la vyama kujiona wao wana haki na Zanzibar zaidi ya wengine, suala la vyama kutosikiliza sauti za wafuasi, hoja za dini, mivutano baina ya Wazanzibari walioko Zanzibar, au baina ya Zanzibar na Tanganyika, au baina ya CCM Zanzibar na wahajirina, kukosekana kwa umoja wa kijamii au umoja wa kitaifa, au kushindwa katika yote kwa kushindwa kuifahamu, kujifunza, halafu kuisahau historia na kuzielekeza nguvu zote za kijamii na kuziweka kwenye kulijenga Taifa la Zanzibar na la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yote ni matokeo tuu na sii msingi!.

A Way Forward ya Zanzibar.
Kunahitajika Zanzibar ni ku deal na chanzo, mzizi!, kuundwe tume ya maridhiano, mzizi wa fitna ukatwe !, wa kwanza kupoka, aombe radhi kwa wenye Zanzibar yao kwa madhila aliyowatenda miaka yote hiyo, na mpokaji mwenye Zanzibar yake aombe radhi kwa aliyoyafanya ile 1964. Watu washikane mikono na kuamua lazima watawale wote wawili kwa zamu na sio kutegemea uchaguzi wa mpoka na mpokwa!.

P.
 

Ndugu zangu,
Nakuwekeeni hapo chini baada ya ya makala ya Dr. Harith Ghassany fikra za Othman Masoud:

WAZANZIBARI WANATAKA KUTOKA HAPA TULIPO, WANATAKA ZANZIBAR MPYA, WANATAKA ZANZIBAR TUNAYOSTAHIKI

Na Othman Masoud

Nimeutafakari Waraka wa Dk. Harith Ghassany na naamini tutakubaliana kuna ya msingi ya kutafakari.

Moja na kubwa ametaja Mkataba wa Magna Carta (Mkataba wa Uhuru au wa Haki za Binadamu). Mkataba huu ulikuja baada ya figisu figisu nyingi baina ya Bunge na Mfalme wa Uingereza. Bunge lilijinasibu na watu wa kawaida na Mfalme alijinasibu na utawala. Kanisa nalo likijinasibu na kulinda sheria na maadili. Magna Carta ikaja kama maridhiano.

Suala muhimu ni kuwa je, Magna Carta ndio iliyoikomboa na kuijenga Uingereza katika ustaarabu mpya wa utawala, demokrasia na maridhiano? Jibu la wazi ni kuwa HAPANA. Sababu kubwa ni kukosekana kwa nia ya dhati ya kuheshimu sheria na utaifa. Aidha kukosekana taasisi madhubuti za utawala.

Mapambano baina ya Ufalme na Bunge yalishamiri tena hasa alipoingia Mfame Charles I. Alituhumiwa kutawala kibabe na kutoheshimu Bunge na haki za raia. Mapambano hayo yalipelekea Mapinduzi ya Oliver Cromwell ya 1649 lakini akaanza kutawala rasmi kama Lord Protector katika mfumo wa Republic (Jamhuri) na sio Monarchy (Ufalme). Lakini na yeye akaja na Umagu wake. Akawa mbabe kuliko huyo Mfalme. Na ndio mana alipofariki mwaka 1658 wabunge na raia wakaona bora Mfalme arudi lakini ule Mkataba wa Magna Carta utekelezwe kwa vitendo. Ndio maana Charles II akafuatwa Ufaransa alikokuwa uhamishoni akaja kutawala kwa masharti ya kutekeleza kwa vitendo Mkataba wa Magna Carta. Jambo hilo ndio lililokuwa msingi wa Maridhiano ya Uingereza na hata Uingereza na Scotland. Ndio mana pia hata Muungano rasmi wa Scotland na Uingereza ukawa rahisi kufanyika rasmi mwaka 1707.

Tunachojifunza hapa nahisi kipo wazi, kwamba Maridhiano yanajengwa na pande mbili zenye kukinzana na yanajengwa juu ya msingi wa kuweka mbele maslahi ya taifa. Si mfumo, mkataba wala mrengu unaojenga maridhiano. Moja lipo wazi, kuondokana na kasumba za yaliyopita ni muhimu sana. Hakuna lilipopita zuri zaidi ya kuzaliwa. Hata uzuri basi unaporomoka kutokana na wakati... kisura mrembo akawa chapwa hata wabaya wakamcheka!!!

Mimi nahisi hapa tulipofika kwa asimia 99 kizazi cha Zanzibar cha leo hakiguswi wala hakiabudu na pengine hakijui yaliyopita. Wanachokijua ni ule uzuri wa milele, uzuri wa kuzaliwa. Kwamba Zanzibar ilizaliwa na ipo na inastahiki kuendelea mbele kama Zanzibar. Hilo lipo wazi.

Wakati ninasomesha darasa za Redet kuhusu Demokrasia Zanzibar, washiriki kila msimu walikuwa ni vijana wa CCM na CUF kwa idadi sawa. Lakini wakati wa kujadili mustakbali wa Zanzibar ndani ya Muungano ilikuwa huwezi kumjua yupi kijana wa CCM na yupi wa CUF. Kusema kweli wakati mwengine wale vijana waliojinasibu kuwa wa CCM walikuwa wakali zaidi na hoja nzito zaidi kuliko za Mhe. Mansoor Yussuf Himid, utadhani aliwawekea darsa akawafunda. Niwe mkweli nilipata insipiration (kutiwa nguvu) kubwa sana kutokana na hoja na mwelekeo wa vijana wale. Darsa zaidi ya 20 za Redet zilinipa na mimi darsa kubwa sana na hazina ya imani kwa nchi yangu.

Miongo miwili ya siasa za vyama vingi vya siasa za Zanzibar zimedhihirisha jambo moja kubwa sana. Kwamba Wazanzibari wengi wanataka kutoka hapa tulipo. Wanataka Zanzibar mpya; wanataka Zanzibar tunayostahiki.


Mimi sioni kama kuna tatizo la uongozi katika mageuzi. Tatizo liliopo ni kama la nchi nyingi zilizopata bahati mbaya kuwa katika hali kama ya kwetu. Hali ambayo mna wenzenu wamejisahau, wamelewa ubinafsi, wamelewa maslahi yao. Hao walikuwepo wakati wa kupigania uhuru katika nchi zote. Walikuwepo Afrika Kusini wakati Wazungu walikuwa na sera ya wazi ya kuwabagua Waafrika na bado walikuwepo Waafrika waliokuwa wakitumiwa na Wazungu kuhujumu ukombozi. Watu kama hao leo wapo Palestina wakiwachongea wanaopambana na udhalimu uliokithiri wa Wazayuni dhidi ya Wafalastin.

Udhaifu unaoonekana kama udhaifu kwa uongozi wa siasa wa upinzani unahitaji tafakuri kubwa. Tafakuri hiyo nahisi si rahisi kuifanya kwa kigezo cha ushindi na kupewa Serikali. Wengi wanaona hilo limeshindikana labda kwa ubwege (samahani kwa lugha isiyopendeza) wa upinzani. Wanasahau kwamba mwizi haibi kwa sababu anayeibiwa ni bwege bali anaiba kwa sababu ni mwizi na mazingira yanamruhusu aibe bila kukamatwa. Ndio mana wapo wezi wanamuibia hata Mungu; misikiti, zaka na mali za yatima ambazo zote hizo ni mali za Mungu. Haziibiwi kwa sababu Mungu ni dhaifu bali Mungu mwenyewe anayawacha yatokee ili iwe funzo kwa binaadamu juu ya kiwango cha udhalimu wa binadamu.

Mimi nahisi tukubali kwamba upande mmoja katika ‘’equation,’’ ya mustakbali wa Zanzibar ipo wazi kwamba inataka Maridhiano na Zanzibar mpya na upande wa pili bado hawajaleuka katika pombe ya maslahi yao.

Tatizo si Wazanzibari. Tatizo ni Wazanzibari waliolala na waliolewa. Dawa si kulaumu chombo cha kutupeleka katika safari ya kuwaamsha bali dawa ni kutovunjika moyo katika safari hiyo. Tukianza kulaumiana manahodha, sarahange na abiria, tutachelewa. La mwanzo lifanywe mwanzo.

Tukishafika tutajua nani anafaa kuendelea na hatua ya pili ya safari. Kwa sasa ni vyema kushauri kuliko kutia shaka. Wachina wana msemo "IN TIME OF WAR EVEN A GRAIN CAN TILT THE SCALE" yaani wakati wa vita hata punje ya nafaka inaweza kuifanya mizani iinamie upande mwengine. We need everybody not somebody. Tunahitaji kila mtu na siyo baadhi ya watu.

JUST THINKING ALOUD!

9 Julai, 2018
 
Huwezi kiwa na maendeleo katika nchi inayoamini sana mambo kwenda kwa kudra za Mungu.

Hapo ndipo mzizi wa matatizo si ya Zanzibar tu, bali nchi masikini nyingi.

Ukiamini hizi habari hata mambo kama inclusivity na meritocracy tu yatakushinda.

Watakuja watu wenye talent kutaka kuendeleza mambo, utawaita makafir, machogo.

Huwezi kuendelea.
 
Ni wazo zuri na limekuja kwa wakati muafaka. Ni vyema pande zinazohasimiana kifikra, kiutamaduni na kidini kutafuta majawabu mujarabu kwa manufaa ya Wazanzibar. Haipendezi waungwana kuendeleza malumbano ambayo hayana tija wala suluhu ya wananchi wa Zanzibar.
Wengi wamekuwa wakiutumia huu mfarakano kujinufaisha kisiasa na kiuchumi bila kufikiri mambo ya msingi yanayotakiwa yafanyike ili kutengeneza mazingira bora ya kuukuza uchumi wa Zanzibar.
 

Ndugu zangu,
Dk. Harith Ghassany amerusi tena...:

KAMA SI TATIZO LA ZANZIBAR KABLA NA BAADA YA 1964, BASI NI KITU GANI?

Na Harith Ghassany
July 11, 2018

Au, limo kwenye mgongano baina ya “national sovereignty” (mamlaka ya kitaifa) na “ethnic sovereignty” (mamlaka ya uasili wa Wazanzibari)?

Suala la kubakisha au kubadilisha muelekeo na uongozi linatokana na “diagnosis” ya maradhi ya Zanzibar, na naamini bado hatujalishughulikia na kulijibu ipasavyo suala la nini khasa tatizo la Zanzibar.

Kwanza niweke wazi kiasi gani namuhishimu na kumkubali ndugu yangu Mheshimiwa Othman Masoud. Namuhishimu kwa mengi na naamini ni Mzanzibari ambae ni mkweli, msomi bobea, si mwanasiasa, na anaifahamu vizuri sana Zanzibar na hajakumbwa na maradhi ya tatizo la Zanzibar na ni mwanga wa mustkabal mwema wa Zanzibar ambao uko juu ya siasa za vyama vya siasa na mitafaruku yake.

Kimafumbo Mh. Othman Masoud amelizungumzia tatizo la Zanzibar ni tatizo la watu ambao wamelewa ubinafsi na maslahi yao. Watu hao wamo kwenye uongozi na viongozi wa vilivokuwa ZNP na ASP, au pia ndani ya uongozi na viongozi wa CCM na CUF?

Si kweli kuwa kizazi cha leo hakiguswi na yaliopita. Tatizo la Zanzibar ni la kihistoria na linawagusa Wazanzibari wa marika YOTE. Tusiikimbie historia wakati historia si ile ya muda wa zamani sana tu. Historia ni muda wowote ule uliopita hata kama ni jana. Umuhimu wa historia ni kusoma na kujifunza.

Uongozi, viongozi, na asilimia kubwa sana ya vijana, wamejifunza nini kutoka historia ili tuiweke KANDO, na tuweze kuyaweka mbele maslahi ya Taifa la Zanzibar BILA ya mgongano na mvutano baina ya Mamlaka ya Utaifa wa Zanzibar na Mamlaka ya Utaifa wa asili ya makundi mawili makubwa ya Zanzibar: ya Bara la Afrika na Mabara mengineyo?

Tatizo la Zanzibar halikuwahi kutatulia katika phase ya kwanza ya Maridhiano kwa sababu kulikuwa na vikwazo ambavyo havitokani na CCM au CUF peke yake. CCM iliyaunga mkono Maridhiano na yasingeliwezekana bila ya mchango mkubwa wa Mh. Mansour na Mh. Eddy Riyami, na kukuridhiwa na Rais Mstaafu Mh. Dkt. Amani Karume. Pia Maridhiano yasingelifanikiwa bila ya mchango wa Mh. Ismail Jussa na kuridhiwa na Maalim Seif Sharif Hamad. Na yaliendelezwa na Dkt Shein mpaka yalipotokea yaliotokea. Yaliotokea na kuyaharibu Maridhiano ni kukosekena kwa misingi madhubuti ya Maridhiano kutokea uundaji wake, na kushindwa kwa Kamati ya Maridhiano kuyalinda Maridhiano kwa kukosa kuwa na Plan B...

Sasa kama alivotupa darasa mwanana Mh. Othman Masoud namna vipi “Magna Carta” ilipitia kwenye vipindi tafauti, na Maridhiano ya Zanzibar yanahitajia kuendelezwa kwa kuingizwa kunako “phase” nyengine.

Lakini kwanza tatizo la Zanzibar lipitiwe upya kwa dhamira mpya na kwa kuzishirikisha pande zote ambazo hazikulewa ubinafsi na maslahi binafsi.

Maridhiano ya kudumu Zanzibar yatapatikana pale Mamlaka ya Utaifa wa Zanzibar na Mamlaka ya Uasili wa Wazanzibari utakapokuwa kitu kimoja.

Maridhiano ya Zanzibar ni kilio cha kila Mzanzibari mwenye kuitakia kheri Zanzibar - CCM na CUF.

Lakini BADO “Magna Carta” ya Zanzibar ina nafasi ya kupiga hatua kubwa na ya haraka, na Mh. Othman Masoud ameshaonyesha njia ambayo ikisubiriwa na Wazanzibari walio wengi tena kutoka pande ZOTE.
 


Labda kwanza ungelitufahamisha wahadimu ni watu waina gani? au je nikabila ?

NA je unaweza tupa ushahidi wowote kama mwinyi mkuu alikua ni muhadimu?
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…