Hebu msome huyu mshairi hapa chini, upate kuburudika...!
Riziki ni maksumu, kila mja fungu lake
Humshukia sehemu, Kinyume na wazo lake
Huo ndio ukarimu, Wamola kwa mja wake
Kila shina zao lake riziki anayo Mungu.
Riziki ni mahakumu, Wenzangu lifahamike
Aweza kosa hakimu, Topasi atajirike
Kuna walisha kaumu, Namshindwa tumbo lake
Kila shina zao lake riziki anayo Mungu.
Mola wetu ni karimu, Hakuna mfano wake
Kutowa kwamlazimu, Kila kiyumbe na chake
Ni wa nini ukhasamu, Nahuku msononeke
Kila shina zao lake riziki anayo Mungu.
Kaditamati tamamu, Shairi na lifupike
Tajiri sitabasamu, Fakiri msimcheke
Lenye mwanzo ufahamu, Halikosi mwisho wake
Kila shina zao lake riziki anayo Mungu.