Nisikilize Nyerere

Idd Ninga

JF-Expert Member
Joined
Nov 18, 2012
Posts
5,497
Reaction score
4,775
NISIKILIZE NYERERE.



1.Huku tunadanganyana,ya kwamba tunakuenzi
Na mbali wameikana,wajali kiti cha enzi
Tasema tena na tena,Hata kama kwa utenzi
Nisikilize Nyerere,kwa hili hauenziwi.

2.Ulipenda Ushairi,kwa upendo na vitendo
Ukapenda washairi,na kufata zao nyendo
Hata ukayakariri,wala hukukaa kando
Nisikilize Nyerere,kwa hili hauenziwi.

3.Fani tena si jalili,hakuna wakuijali
Imetupwa kidhalili,kwa vyama na serikali
Haina tena jamali,kisiri waikejili
Nisikilize Nyerere,kwa hili hauenziwi.

4.Umebaki mshangao,fani kufichwa kapuni
Ni kama magangao,yaso na tena thamani
Shairi ya kale nguo,labda ndivyo wavyodhani
Nisikilize Nyerere,kwa hili hauenziwi.

5.Na sanaa za usumbi,zapewa kipaumbele
Hii yawashwa utambi,ifie mbele kwa mbele
Wanachofanya vitimbi,wakti tungo zipo tele
Nisikilize Nyerere,kwa hili hauenziwi.

6.Ushairi ni fukara,wapeleka mavuoni
Nani afanye jabara,na ipate afueni
Imegeuzwa tambara,lisopendwa maskani
Nisikilize Nyerere,kwa hili hauenziwi.

7.Leo washairi wengi, tatizo ni serikali
Zimetungwa tungo nyingi,maridadi zilo tuli
Hata kwa wetu uwingi,serikali hitujali
Nisikilize Nyerere,kwa hili hauenziwi.

8.Labda cha kwetu utumwa,cha Mgeni ndo dhahabu
Sitakia kuja sakamwa,sana nikapata tabu
Vibaya nikaja semwa,nimekashifu mababu
Ushairi ulopenda,Nyerere hauenziwi.

SHAIRI-NISIKILIZE NYERERE.
MTUNZI-Idd Ninga,Tengeru Arusha
+255623010160
iddyallyninga@gmail.com
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…