*ANAANDIKA ALBERT MSANDO KUHUSU UNAFIKI NA USALITI WA ZITTO*
Ndugu Kabwe Z. Ruyagwa Zitto,
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo,
Bangwe, Kigoma Mjini.
Kwanza, nichukue nafasi hii kukupa pole kwa ajali na kumshukuru Mungu kwa kukuponya na ajali hiyo.
Pili, nimeona kwa haraka kabisa nibebe jukumu la kukujibu wewe binafsi kuhusu Tamko lako lenye kichwa cha habari, “Nitampigia Kura Tundu Lissu ili awe Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”.
Nilitegemea sana kwamba baada ya kufungwa kengele ya unafiki na usaliti na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo miaka yote ile leo ungesimama na kuwaeleza ukweli watanzania badala ya hiki ulichokifanya.
Mimi nilikuwa mtu wa mwisho kabisa kuamini kwamba wewe ni mnafiki na msaliti. Tulisimama wote muda wote ulipopewa jina baya ili ufe kisiasa (“wazungu wanasema “give a dog a bad name and hang it”).
Ila leo umethibitisha yaliyosemwa na hao ulioamua kushikana nao mikono. Hii yote ni kwa sababu tu ya uchu wa madaraka na imani kwamba kuna uwezekano wa kupata nafasi endapo TL atashinda. Umediriki KUTAMKA hadharani UONGO na UPOTOSHAJI ili kukidhi matamanio ya nafsi yako.
Umesaliti na kutupa chini ya basi misimamo yako binafsi na ya wale ambao wameendelea kukuamini hata baada ya sisi wengine kukaa pembeni na kukuacha ili ujenge Chama chako. Najua hawatakwambia ila mioyoni mwao watakuwa wanaumia sana na sasa wameelewa wewe ni mtu wa aina gani. Ila ndio basi tena!
Nikukumbushe mambo mawili tu ambayo umeyasemea UONGO na kujivika joho na UNAFIKI kwenye tamko lako.
1. Umetamka kwamba kutokana na uwepo wa sheria kandamizi ya Vyama vya Siasa, ushirikiano wa kisheria tumeona hauna maana kwetu kama Chama kwani Msajili wa Vyama hawezi kuidhinisha jambo linalokwenda kuiondoa CCM madarakani. Zitto, wewe ni muongo sana. Sana. Kifungu cha 11A cha Sheria ya Vyama vya Siasa inaruhusu USHIRIKIANO wa vyama vya siasa MIEZI MITATU kabla ya uchaguzi. Mikutano Mikuu ya Vyama husika lazima vipitishe maamuzi ya ushirikiano huo (coalition). Nikuulize, mngekaa lini? Miezi mitatu mazungumzo yenu na CHADEMA kuhusu ushirikiano yalikwamishwa na nini? Na nani? PIA Msajili wa Vyama hana mamlaka wala hapaswi KUIDHINISHA AU KURIDHIA ushirikiano wa vyama. Mkishasaini na kukabidhi BASI. Hata hili umeamua kuongopa.
2. Umetamka, “zaidi NINAMUAMINI LISSU kutokana na historia yake ya kupigania Haki za Watu”. Umesahau nani alikuwa kinara wa sisi kufukuzwa CHADEMA kwa aibu? Umesahau? Ni nani alikunyima HAKI ya kusikilizwa? Ni nani alisema Kamati Kuu isikusikilize wewe ni msaliti? Nani alisema hupaswi kuaminiwa kwa chochote? Unaongopa. Unakana hata kile nafsi yako inachokijua na ilichopitia kwa uchungu mkubwa. Umemsahau Tundu Lissu tuliekimbizana nae Mahakamani kusimamia haki zako za kutaka uenyekiti, kusikilizwa na heshima kwa jamii?
Nimalizie kwa kukukumbusha, umeshindwa kutamka nani achaguliwe kwenye Kata na Majimbo. Sio kwa bahati mbaya. Nafsi yako imekusuta. Umesema wapigiwe wagombea wenye ushawishi. Mbona mliweka wagombea ambao hawana ushawishi? Hutaki umma ujue kwamba Chadema walikugomea kukuachia baadhi ya majimbo na kata? Na sababu ni ile ile kwamba hawakuamini? Na sehemu ambazo hamjaweka wagombea ni kutokana na ukosefu wa fedha? Si ukiri tu?
Bernard Membe. Umemuacha kwenye mataa. Huyu wala simuhurumii. Alitaka mwenyewe. Angetumia akili kidogo tu angejua kona ambayo ungemuachia. Tatizo lake (na lako) ni uongo. Alikudanganya ana FEDHA nyingi za uchaguzi kumbe hata hela ya fomu ilikuwa ni mtihani kuitoa. Madeni aliyokuachia yatalipika kwa kudra za Mwenyezi Mungu. ILA hujataka hata kumzungumzia kwenye tamko lako. Wala hatma yake hujagusia. Kichaka kwamba WEWE BINAFSI utampigia kura Tundu Lissu ni cha kitoto sana. Wenye akili wataelewa. Imefika mwisho.
#JPMMitanoTena #CCM
Albert Gasper Msando,
MwanaCCM, Ndugu yako.
16/10/2020.