Wahisani watoa onyo
na Irene Mark
Tanzania Daima
KWA mara ya kwanza katika miaka ya hivi karibuni, nchi wafadhili zimetangaza rasmi kwamba imani waliyokuwa nayo kwa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kwa mwaka huu wa fedha imepungua kuliko ilivyokuwa mwaka jana.
Kutokana na hali hiyo basi, wahisani wanaotokana na kundi la nchi 14 zinazotoa misaada katika bajeti, wameitaka serikali kuchukua hatua za haraka kurejesha imani hiyo ambayo kuporomoka kwake kunachangiwa pamoja na mambo mengine, wasiwasi walionao katika matumizi ya fedha za misaada na mikopo wanayotoa kwa Tanzania.
Tamko hilo la kwanza na la aina yake, lilitolewa jana Dar es Salaam na Balozi wa Uingereza nchini, Philip Parham, wakati akitoa taarifa ya wafadhili walipokuwa wakijadili utekelezaji wa bajeti ya serikali ya mwaka 2006/07, katika mkutano ulioshirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo.
Akizungumza mbele ya Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, balozi huyo ambaye nchi yake imepewa heshima ya kuwa mwenyekiti wa mataifa hayo 14 wahisani, alibainisha kuwa serikali inapaswa kuhakikisha kuwa misaada inayotolewa na wao inasaidia kuimarisha maisha duni ya watu maskini.
Kwa kuonyesha uzito wa kauli hiyo nzito dhidi ya serikali ambayo kwa miaka mingi sasa imekuwa kipenzi cha nchi wahisani, balozi huyo kabla ya kusema maneno hayo alianza kwanza kumwomba radhi Waziri Meghji kwa atakayoyasema, akisema ameamua kuwa muwazi kwa kueleza kile wafadhili wanachokiona.
"Mafanikio bado yapo mbali. Ninaamini Mheshimiwa Waziri (Meghji) atanisamehe iwapo ninataka kuwa mkweli kuhusu mtazamo wa wahisani…Mazingira ya leo yanatoa changamoto zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka uliopita. Leo imani waliyokuwa nayo wahisani wa maendeleo imepungua kuliko ilivyokuwa mwaka 2006," alisema balozi huyo.
Kutokana na hali hiyo, Balozi Parham akionekana kuwasemea wahisani wenzake wengine ambao katika bajeti ya mwaka huu walichangia kiasi cha dola za Marekani milioni 673, sawa na asilimia 15 ya bajeti nzima, aliitaka serikali kuimarisha uwajibikaji kwa wadau wake, kikubwa akikitaja kuwa ni kukabiliana na ufisadi.
Alisema washirika wa maendeleo wanataka kuongeza misaada kwa Tanzania hasa katika kipindi hiki kigumu ambacho misaada zaidi inahitajika.
Hata hivyo, alibainisha kuwa viwango vya juu vya ufadhili kwa upande mmoja, kwa upande mwingine vinahitaji utendaji makini kutoka serikalini.
Kuhusu washirika wa maendeleo, balozi huyo alibainisha kuwa wanapokea mwangwi wa hali halisi ya Tanzania kutoka kwa maofisa wa serikali, asasi za kiraia, wasomi na wananchi kwa ujumla katika mambo mawili makubwa.
Balozi Parham aliyataja mambo hayo kuwa ni uhitaji wa serikali kutafsiri bajeti na kuifanya ionyeshe maendeleo halisi na kuinua hali ya wananchi maskini.
"Lakini ni jambo la wazi kwamba kisiasa, viwango vya juu vya ufadhili kutoka washirika wa maendeleo vinahitaji viwango vya juu vya uwajibikaji serikalini.
"Hofu kubwa ya washirika wa maendeleo, kama ambavyo inaonyeshwa pia na maofisa wa serikali, vikundi vya kijamii, wasomi na wananchi kwa ujumla inahusu masuala hayo mawili," alisema.
Alisema hali inajionyesha kuwa ili kushinda vita dhidi ya rushwa, serikali ya Rais Kikwete imelifanya hilo kuwa kipaumbele, jambo lililogeuka kuwa mjadala wa kitaifa ambao waathirika wakuu ni wananchi maskini.
Aidha, Balozi Parham alimtaka Waziri Meghji kusema ukweli kuhusu tuhuma nyingi za rushwa kwa washirika wa maendeleo, wawekezaji muhimu na Watanzania wote kwa ajili ya kurudisha imani ya serikali.
Akizungumzia haja ya matokeo kuonekana, balozi huyo alisema serikali inapofanikiwa kutimiza matarajio yake, imani ndivyo inavyoongezeka na akasema hali hiyo ndiyo huifanya serikali kukabili changamoto kutoka kwa wapinzani wake wa kisiasa, vyombo vya habari na asasi nyingine za kijamii.
Katika hilo alisema kama kuna eneo ambalo Tanzania imeshindwa basi ni lile la kuwa na mifumo inayoweza kuonyesha bayana kwamba fedha zinazotolewa na wahisani katika bajeti zinazaa matunda ya wazi kwenye maeneo kama yale ya kuimarika kwa miundombinu, huduma za kijamii na kuongezeka kwa fursa za kimaisha kwa watu maskini.
Akitoa mfano, alisema ingawa katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko kubwa la maendeleo ya elimu ya sekondari kwa shule, nyingi zaidi kujengwa, madarasa kuongezeka na kuimarika kwa hosteli, bado kumekuwa na ufinyu wa taarifa zinazoeleza uwiano uliopo kati ya idadi ya wanafunzi na ya walimu wanaowafundisha.
Hali hii alisema imesababisha kutokuwapo kwa taarifa za kutosha kuhusu idadi ya walimu waliohitimu sawasawa, mahitaji halisi ya walimu hao na vifaa vingine vya kufundishia.
Kama hiyo haitoshi, alisema kwa upande wa elimu ya msingi, hali ni hiyo hiyo kwamba, wakati takwimu zikionyesha kuwa idadi ya watu wanaojiunga na elimu hiyo imefikia asilimia 97, kiwango ambacho ni cha juu kabisa, takwimu za idadi ya watu na zile za kiafya zinaonyesha kupungua kwa idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa kuanza elimu ya msingi.
Kutokana na ukinzani huo wa takwimu, balozi huyo aliitaka serikali kuchukua hatua ya kuchunguza kasoro hizo, ikiwa ni pamoja na kuainisha mikakati ya kulinda mafanikio yaliyofikiwa na kubainisha kwa uhakika kabisa kiwango cha mafanikio katika elimu ya msingi.
Akizungumzia rushwa, Balozi Parham alisema ni muhimu kwa serikali kuonyesha kuwa ipo hai kwa kuchunguza tuhuma zinazoelekezwa kwake na kupeleleza vilipo vielelezo vya tuhuma hizo.
"Tunasubiri kwa shauku taarifa ya mkaguzi wa Benki Kuu (BoT), madeni ya nje na majibu ya serikali kuhusu suala hili. Pia tunangoja matokeo ya uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)," alisema balozi huyo.
Akihitimisha kusoma risala yake, balozi huyo alisema wamepata taarifa ya Wizara ya Fedha kwa mwezi uliopita inayoeleza masharti ya wafadhili.
Hata hivyo, katika kile kilichoonekana kama kujibu mapigo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Peniel Lyimo, alisema kuwa masharti ya wafadhili yanakwamisha maendeleo ya serikali, hali inayosababisha wafadhili kuiendesha nchi.
"Hawa mabwana wana masharti magumu sana, ndiyo maana tunashindwa kuyafikia maendeleo… hii inasababisha nchi yetu kuendeshwa na wafadhili badala ya kujiendesha wenyewe," alisema Lyimo ambaye ana uzoefu na shughuli za wafadhili, kwani amewahi kuwa Katibu Mkuu katika Wizara ya Fedha kwa muda mrefu.
Baadhi ya wadau waliohudhuria mkutano huo ni mabalozi, maofisa na watendaji wa serikali, watu mashuhuri, wanasiasa na wasomi mbalimbali.