mkulu senkondo
JF-Expert Member
- Feb 19, 2017
- 1,862
- 3,574
Tanzania inakabiliwa na tatizo la upungufu wa wafanyakazi (watumishi wa umma) katika mashirika na taasisi mbalimbali za serikali.
Kwa kutumia kada ya elimu peke yake, hadi kufikia Februari 2023, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ilieleza kuwa, mahitaji ya walimu katika shule za msingi yalikuwa ni 362,189 kwa kutumia uwiano wa 1:45 yaani (Mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45).
Hata hivyo, walimu waliokuwepo kwa wakati huo ni 175,864 ambao walikuwa na jukumu la kufundisha wanafunzi milioni 12.36 waliopo nchi nzima katika ngazi hiyo ya elimu. Hiyo ni sawa na kusema kwa wastani, mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 70. Uwiano huo uko juu kuliko mapendekezo ya Serikali ya mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi wasiozidi 45 katika darasa moja.
Idadi ya upungufu wa walimu iliyopo hadi kufikia Februari 2023.
Hadi kufikia Februari 2023, Tanzania ilikuwa na upungufu wa walimu wa shule za msingi 186,325 sawa na asimilia 51.44 ya walimu waliopo sasa kufikia uwiano wa Mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45 (1:45). Upungufu huo wa walimu uliopo ni mbali na shule za sekondari, vyuo vya ufundi, vyuo vya kati na vyuo vikuu sambamba na walimu wa wanafunzi wenye mahitaji maalum! Hata hivyo, uhaba wa watumishi katika kada mbalimbali nchini Tanzania ni mkubwa zaidi ya mfano wa data za hapo juu kwa maeneo ya vijijini. Takwimu hizo zinaonesha na kudhihirisha uwepo wa uhaba wa watumishi katika sekta mbalimbali za umma na hivyo kuzorotesha utoaji huduma na kutengeneza jamii isiyostawi na kupiga hatua kimaendeleo.
Vijana wahitimu wenye sifa za kuhudumia Watanzania wapo mtaani!
Licha ya uwepo wa upungufu mkubwa wa watumishi wa sekta za umma hususan maeneo ya vijijini, kuna maelfu ya vijana wa kitanzania waliopo mitaani ambao wangeweza kuhudumu katika utumishi wa umma! Kibaya zaidi, hata hao watumishi wachache waliopo maeneo ya vijijini hawataki kuishi na kufanya kazi huko na badala yake na wao wanataka kuhama. Hali hii inadhihirisha kuendelea kwa uwepo wa uhaba wa watumishi wa sekta za umma katika maeneo ya vijijini nchini Tanzania.
Mtazamo mpya wa kuleta mabadiliko katika sekta ya umma.
Ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa watumishi wa umma hususan maeneo ya vijijini nchini, makala hii inatoa rai kwa serikali kupitia wizara husika kuwajibika ili kuleta mabadiliko yatakayoleta uwiano sawa wa utoaji huduma kwa Watanzania bila ya kujali wanaishi mijini au vijijini kama ifuatavyo;
1. Serikali iweke posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu.
Hapana shaka yoyote kwamba, kwa mazingira ya nchi yetu, maeneo ya vijijini sio mazingira rafiki kwa watumishi wengi kulingana na malengo na matarajio yao. Hivyo, ili kuwabakiza huko bila ya kuwashurutisha, serikali iwalipe posho ya mazingira magumu ya kazi watumishi wa sekta za umma wanaofanya kazi maeneo ya vijijini mbali na mishahara yao. Hii itawavutia watumishi kufanya kazi vijijini mbali na kufikiria kuacha kazi na kusababisha upungufu.
2. Kuwaajiri vijana waliohitimu fani mbalimbali kufanya kazi kwenye maeneo yao kwa kuwalipa kiwango fulani cha mshahara.
Vijana wenye sifa ya kuajiriwa na wamekosa fursa hiyo ya kuwa watumishi wa umma waajiriwe kwa kulipwa kiwango fulani cha ujira. Mpango huu unaweza kupata upinzani mkali kutoka kwa wanaharakati wa haki za wafanyakazi na wanasiasa! lakini kipi bora? waendelee kukaa bila kazi au wafanye kazi kwa kulipwa kiwango pungufu na mshahara wa elimu zao? Mpango wa hiari wa kuwaajiri vijana kwa kuwalipa ujira pungufu utakuwa na faida zifuatazo; kwanza, utaipunguzia serikali mzigo wa gharama za matumizi (wage bill). Pili, ni suluhu ya muda mfupi ya tatizo la ukosefu wa ajira. Tatu, utasaidia kupunguza tatizo la upungufu wa watumishi wa sekta za umma maeneo ya vijijini. Nne, Utasaidia kuikuza thamani ya elimu iliyokwisha aanza kupotea. Tano, kuongeza pesa kwenye mzunguuko na mwisho kufungua fursa mpya za kiuchumi.
3. Kuboresha huduma muhimu za kijamii maeneo ya vijijini.
Moja ya sababu inayowafanya watumishi kutopendelea kuishi na kufanya kazi maeneo ya vijijini ni ubovu na ukosefu wa huduma muhimu za kijamii kuanzia; maji, umeme, miundombinu ya mawasiliano, makazi duni na huduma za afya. Hivyo, ili kuwavutia watumishi wa sekta za umma kufanya kazi maeneo ya vijijini ni vema serikali ikawajibika kwa kuboresha miundombinu ya kijamii na ile ya kimawasiliano ili kuwavutia watumishi wa sekta za umma kufanya kazi maeneo ya vijijini.
Hitimisho.
Kwa kuwa sio kila kijiji kina mazingira magumu kwa watumishi kufanya kazi, ni vema serikali kuanza mpango huu kwa kuanisha Halmashauri zenye mazingira magumu zaidi ya kazi. Serikali kwa kutumia wataalamu na maofisa wake wanaweza wakaweka viwango na vigezo anuwai vitakavyotumika kuzitambua Halmashauri za vijijini zenye mazingira magumu ya kazi kwa watumishi wa sekta za umma.

Upvote
1