SoC01 Njia ya mafanikio ina changamoto nyingi, usikate tamaa

SoC01 Njia ya mafanikio ina changamoto nyingi, usikate tamaa

Stories of Change - 2021 Competition

DustBin

JF-Expert Member
Joined
Jun 3, 2021
Posts
609
Reaction score
604
Njia ya mafanikio ina changamoto nyingi sana. Changamoto ambazo anahitajika mpambanaji ajizatiti kwa ngao ya kutokata tamaa na ajikinge kwa silaha ya uvumilivu. Vikatisha tamaa katika maisha ni vingi pia, ukiwa na moyo mwepesi huwezi kufikia malengo yako. Na kama ilivyo sifa ya mafanikio kwamba hayaji isipokua baada ya muda mrefu wa kuhangaika na kujibidiisha. Watu wengi wanashindwa kufikia malengo yao kutokana na hulka na tamaa ya kutaka kufanikiwa ndani ya muda mfupi. Na ndio maana utawakuta wakijiingiza katika shuguli zisizo halali. Hawa hukosa uvumilivu na pale wanapoona mafanikio hayaji ndani ya muda huo mfupi waliotarajia matokeo yake hukata tamaa.

Katika maisha mwanadamu hatakiwi kukata tamaa. Ni juu yetu kujituma, kuhangaika na kupambana katika kujishugulisha na shuguli mbalimbali zilizo halali mpaka pumzi ya mwisho wa maisha yetu.

Hata katika vitabu vitakatifu vilivyoshushwa kutoka mbinguni tumehimizwa na kulazimishwa kutokata tamaa. Kwa mfano katika Qur-ani 12:87 Mwenyezimungu anasema “….Wala msikate tamaa na rahama ya Mwenyezimungu, hakika hawakati tamaa na rahama za Mwenyezimungu isipokuwa watu makafiri.” Pia katika Bibilia, Luka 18:1 inasema “Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu siku zote wala msikate tamaa.” Na kukata tamaa ni ishara ya kukosa imani; na asiye na imani hata chembe Mungu hapendezwi naye.
Hivyo kukata tamaa ni tabia inayotakiwa kupigwa vita na wote wenye kupenda mafanikio.

Tujifunze kupitia hawa wafuatao huenda tukapata funzo la kutokata tamaa, kwani katika mifano mambo huwa wazi zaidi.

Mwaka 1977 Mama Samia Suluhu Hassan alikua akihudumu katika ofisi ya serikali akiwa ni karani (mchapaji au katibu muhtasi), na baada ya miaka 44 mbele, mwaka 2021 ameapishwa kuwa Raisi wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania. Laiti kama angekata tamaa na kubweteka na kazi yake ya ukarani asingeweza kufikia hapo alipofikia.

Huwezi amini katika miaka ya mwanzoni mwa 2000 Abdul Nasibu (Diamond) alikua anaomba kusindikiza kupanda jukwaani kwa ajili ya ufunguzi kwenye matamasha (shows) ya Abubakar Katwila (Q Chief). Leo hii Nasibu ni msanii wa kimataifa na ndiye msanii wa kwanza kuingiza Tanzania gari lenye thamani ya bilioni 1.5

Kwa mara ya kwanza nimeanza kumjua Ally Saleh Kiba (King Kiba) na kumuona kwenye luninga ilikua ni miaka ya 2004/2005 kwenye nyimbo ya Maria ya msanii Abby Skillz akiwashirikisha Heri Sameer Rajabu (Mr. Blue) na Ally Kiba. Ni kama vile Heri Sameer ndiye aliyemtoa Ally Kiba kwenye tasnia kwani yeye alishakua maarufu kipindi hicho. Leo hii Ali Kiba anatajwa kuwa katika wasanii wenye mafanikio makubwa.

Kutokata tamaa kumemsaidia msanii Rajabu Abdul Kahali (Harmonize) kupata mafanikio katika sanaa kwani alishawahi kushiriki mashindano ya Bongo Star Search (BSS) na hakuweza kufika hata robo fainali.

Mifano ni mingi sana katika hili, leo tutosheke na hii michache. Kama hawa niliowataja wangekata tamaa na kubweteka wasingeweza kufikia hapo walipofikia. Mafanikio yao iwe chachu kwetu katika kujituma,kujibidiisha, kuwa wavumilivu na tunayokutana nayo katika shuguli zetu, na kubwa zaidi kutokata tamaa katika maisha.

Ewe unayepambana katika shuguli zako za uzalishaji mali, usikate tamaa endelea kujibidiisha kwani ipo siku utafikia malengo yako na ndoto yako itatimia.

Ewe mwenye ndoto ya kuteuliwa katika ngazi mbali mbali za uongozi kama Mimi, tusikate tamaa ndugu yangu. Kwani ipo siku tutateuliwa tu, kama sio awamu hii hata awamu ijayo tuendelee kujituma katika kazi.

Ewe unaeandika mabandiko kwenye jukwaa hili la “Stories of Change” usikate tamaa kwa kuona haupigiwi kura, na uzi wako hakuna anechangia, endelea kuandika zaidi na zaidi. Ipo siku utakuja kupata tuzo hata kama sio tuzo za Jamii Forum.

Ewe mjasiriamali mdogo, endelea kupambana na kujituma kwa bidii na usikate tamaa. Siku moja tu itakuja kubadili maisha yako ya kibiashara na kuwa mfanyabiashara mkubwa wa kupigiwa mifano. Changamoto haziepukiki katika maisha ya kutafuta.

Ewe mwanafunzi unaesoma kwa bidii lakini bado unafanya vibaya katika masomo yako, usikate tamaa zidisha kusoma zaidi tena kwa bidii kwani waswahili husema ‘mwenye kugonga mlango kwa nguvu mwisho hufunguliwa’. Kwa hiyo enedelea kusoma kwa bidii na juhudi zote utakuja kufanikiwa tu, hakuna kisichowezekana chini ya jua.

HITIMISHO

Mafanikio hayaji yenyewe na wala hayaji ndani ya muda mfupi. Mafanikio ya kweli yanagharimu muda na jitihada kwa kujitoa katika jambo husika huku mhusika akijipamba kwa kusubiri na kutokata tamaa. Tusibweteke, na tusivunjike moyo kwa yanayotusibu hivi sasa tutambue ya kuwa mafanikio makubwa hukumbwa na changamoto kubwa.

Naomba kila mtu iandikwe katika nafsi yake “MARUFUKU KUKATA TAMAA”


DustBin
 
Upvote 6
kweli kabisa umenena hata kama ulikua juu sn ukaanguka chini kimafanikio usikate tamaa kwan unaweza kurudi tena ulipokuepo au zaidi

pia ukiwa kijana safari bado ndefu usijali kwa utakayo yapitia leo kwan iko siku yatakusaidia au yatakufikisha unapo taka kufika
maisha yakuiga sio mazur kwan kila mtu anamalengo yake jaribu kujipambanua ww mweny kufikia ndoto zako huku ukiweka uwaminifu na uvumilivu katika kila jambo.
 
kweli kabisa umenena hata kama ulikua juu sn ukaanguka chini kimafanikio usikate tamaa kwan unaweza kurudi tena ulipokuepo au zaidi

pia ukiwa kijana safari bado ndefu usijali kwa utakayo yapitia leo kwan iko siku yatakusaidia au yatakufikisha unapo taka kufika
maisha yakuiga sio mazur kwan kila mtu anamalengo yake jaribu kujipambanua ww mweny kufikia ndoto zako huku ukiweka uwaminifu na uvumilivu katika kila jambo.
Umeongeza madini ya maana sana..!! Mafanikio yapo mbali sana wengi huishia njiani kwa kukata tamaa
 
Back
Top Bottom