SoC04 Njia za kutatua tatizo la afya ya akili katika taifa letu

SoC04 Njia za kutatua tatizo la afya ya akili katika taifa letu

Tanzania Tuitakayo competition threads

Quartz360

Senior Member
Joined
Mar 27, 2023
Posts
133
Reaction score
317
UTANGULIZI
Katika nchi ya Tanzania tatizo la afya ya akili, limekuwa ni moja la tatizo linalogonga vichwa vya habari kila kukicha. Kumekuwa na taarifa nyingi sana za watu kujiua kutokana na sababu mbalimbali, matumizi ya madawa ya kulevya pia imekuwa ni tatizo. Takwimu zilizotolewa na shirika la afya duniani zinaonyesha kuwa mnamo mwaka 2020 zaidi ya watu 2,474 walijiua huku sababu kuu ikiwa ni tatizo la afya ya akili. Hii dhahiri inaonyesha ni kwa kiasi gani tatizo hili ni kubwa katika nchi yetu, na kama afya ya akili haitapewa kipaumbele ni ukweli usiopingika kuwa taifa litapoteza nguvu kazi kwa kiasi kikubwa, fedha nyingi zitatumika katika kuwapa matibabu baadhi ya waathirika na hivyo kuwa na mzigo mkubwa kwa jamii na taifa lote kwa ujumla. Afya njema ya akili ni chachu tosha ya kupata mawazo yenye ubunifu ambayo yatakuwa chachu ya maendeleo ya taifa letu kwa kuongeza chachu ya maendeleo katika nyanja zote za maisha.

KIINI
MIKAKATI YA KUTATUA TATIZO LA AFYA YA AKILI KATIKA TAIFA LETU
1. Katika vituo vya afya hasa hospitali za wilaya kuwepo na wataalamu wa masuala yanayohusu afya ya akili. Katika hospitali nyingi za wilaya nchini Tanzania wataalamu wa magonjwa ya akili hawapo kabisa, wataalamu hao huweza kupatikana katika hospitali za rufaa tuu na teule mfano hospitali ya MILEMBE iliyoko Didoma, hivyo kuwafanya wananchi walioko mbali na hospitali hizo kukosa huduma stahiki kutokana na gharama inayohitrajika ili kuweza kufikia huduma. Hivyo, kushusha huduma hii hadi ngazi ya wilaya katika hospitali zote za wilaya kutaleta mafanikio katika jamii, kwani huduma itakuwa karibu na wanajamii na hivyo kupata msaada wa kitaalamu kila inapo hitajika.

2. Kuwepo na programu maalumu ya utoaji elimu katika jamii kwa mfululizo wa vipindi vitatu kwa kwa mwaka, yaani kila baada ya miezi minne, kuandaliwe na makongamano ya utoaji wa elimu juu ya afya ya akili katika jamii, programu hizo ziendane sambamba na kuwakutanisha wataalamu wa saikolojia pamoja na wanajamii, hii itasaidia kuwapa wanajamii taarifa sahihi za namna ya kuepukana na matatizo ya afya ya akili kama vile msongo wa mawazo unaoplekea watu wengi kuchukua maamuzi ya kujiua, vilevile programu hizi zitasaidia kupunguza matumizi ya madawa ya kulevya miongoni mwa wanajamii ambapo wengi wao huishia kuwa na matatizo ya afya ya akili.

3. Serikali kupitia wizara ya afya ianzishe huduma ya kielektroniki kupitia simu za mkononi itakayowasaidia wananchi kutoa taarifa juu ya viashiria ya matatizo ya afya ya akili kwa kuwasiliana moja kwa moja na dawati na ushauri nasaha kuhusu afya ya akili kupitia simu zao, pia hii itasaidia kutoa taarifa juu ya washukiwa wa matatizo ya afya ya akili kabla hawajafikia maamuzi ya kuhatarisha maisha yao au maisha ya watu wengine. Hivyo huduma hii itasaidia sana kuokoa watu wengi kutoka kwenye dimbwi la matatizo ya akili na kuifanya jamii iweze kuwa na ustawi ulio bora.

4. Wizara ya afya kwa kushiriana na vyombo vya habari kama vile televisheni, redio na magazeti waandae vipindi maalumu vya kitaifa vitakavyolenga kuifikishia ujumbe jamii juu ya elumi ya afya ya akili, kuwepo na wataalamu wa afya ya akili kwenye kila kipindi watakaoelimisha jamii juu ya namna ya kuepukana na matatizo ya afya ya akili, vipindi hivi mfano vipindi vya redio na televisheni vitatoa wasaa wa kuuliza maswali, ambapo wafualiliaji wa vipindi hivyo watapata ufafanuzi wa maswali yao kutoka kwa wataalumu.

5. Serikali iruhusu sekta binafsi, asasi za kiraia na wadau mbalimbali kuunda taasisi maalumu katika jamii zitakazo toa msaada wa karibu na wa moja kwa moja kwa wananchi, taasisi hizi zitawasaidia wananchi kupata suruhisho la matatizo yao kila inapohitajika, italeta ustawi bora wa afya ya akili miongoni mwa watu, pia itaipunguzia serikali mzigo wa kushughukika na wagonjwa wa afya ya akili.

6. Serikali ije na mipango madhubuti ya kupunguza ugumu wa maisha katika jamii. Matukio mengi yanayotokana na matatizo ya afya ya akili chanzo chake mara nyingi ni ugumu wa maisha miongoni mwa watu katika familia na jamii zao, hii ni kutokana na takwimu za shirika la afya duniani juu ya afya ya akili ya mwaka 2020. Hivyo, serikali ipunguze ugumu wa maisha kwa kuboresha miundombinu wezeshi itakayowapa unafuu wanachi wa kufanya shughuli za uzalishaji mali, kwa kuondoa kodi zisizo na ulazima, kuondoa masharti hatarishi ya uanzishwaji wa biashara mpya, kuimarisha upatikanaji wa mikopo nafuu kwa wananchi, kuwainua wakulima kwa kuwapa elimu stahiki juu ya kilimo, kuboresha upatikanaji wa huduma za kisheria, kupinga vitendo viovu katika jamii, na kuanzisha makongamano ya kijasiliamali katika jamii yenye lengo la kutoa elimu ya kifedha kwa wananchi, hii itapunguza ugumu wa maisha kwa kiasi kikubwa na kupunguza tatizo la afya ya akili katika jamii.

HITIMISHO
Maendeleo katika nchi yetu yako mikononi mwa watanzania wenyewe, na watanzania hawawezi kuleta maendeleo ya namna yeyote ile kama afya zao za akili haziko imara, kwani kupitia afya ya akili ndiko chemichemi za fikra yanikifu huanzia. Hivyo, kila mmoja wetu ana jukumu la kushiriki kikamilifu katika kuimarisha afya ya akili katika taifa letu, ili kuweza kuleta chachu ya maendeleo katika nyanja zote za uzalishaji mali, na mwisho tuwe na taifa la watu bora, wabunifu na imara wenye mtazamo chanya katika kuleta mabadiliko.

Asante kwa kusoma andiko hili, kwa pamoja tujenge taifa letu.
 
Upvote 0
Back
Top Bottom