Serikali yatangaza miradi mikubwa minne ya umeme.
Na Freddy Azzah, Mwananchi
WAKATI taifa linakabiliwa na upungufu mkubwa wa nishati ya umeme, serikali imetangaza mpango mkakati wa kutekeleza miradi mikubwa minne inayotarajia kugharimu zaidi ya Sh324.6 bilioni.
Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake jana kuwa Mikoa ya Tanga, Dodoma, Morogoro, Iringa, Mbeya na Mwanza, iko kwenye mradi unaofadhiliwa na Millenium Challenge Corporation kwa gharama ya dola za Marekani milioni 89.666.
Kwa mujibu wa Ngeleja katika mradi huo shughuli zitakazofanyika ni pamoja na uimarishaji na upanuzi wa mifumo ya kusafirishia na kusambaza umeme katika mikoa hiyo.
Pia alisema mradi huo utahusu ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme wa megawati nane katika Mto Malagarasi na kuusambaza katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji, Uvinza na Kasulu.
Ngeleja alisema ujenzi wa kituo hicho, utagharimu jumla ya Dola za Kimarekani milioni 53.68.
Alisema ujenzi wa mfumo wa umeme wa baharini kutoka rasi ya Kilimoni Dar es Salaam hadi ya rasi Fumba Unguja, unaofadhiliwa pia na MCC, utagharimu Dola za Marekani 63.125.
"Zabuni kwa ajili ya Sub-marine cable kwenda Zanzibar, ilifunguliwa Machi 5 mwaka 2010, tathimini ya zabuni hiyo imeshakamilika, mshindi atatangazwa wakati wowote kuanzia sasa," alisema Ngeleja.
Ngeleja alisema zabuni kwa ajili ya kuwapata makandarasi watakaojenga miundombinu katika mikoa hiyo sita, imeshatangazwa na itafunguliwa Juni mosi mwaka huu.
Kwa mujibu wa wazairi miradi yote hiyo ambayo itafadhiliwa na MCC kwa gharama ya Dola milioni 206.47 za Kimarekani, itakamilika 2012.
Waziri Ngeleja alisema mradi mwingine ni ule unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) unaohusu ujenzi wa kilomita 932 za njia za usambazaji umeme wa msongo wa kilovoti 33 na 11 katika Mikoa ya Mwanza, Shinyanga ikiwemo Bukombe, Dar es Salaam na Arusha.
Alisema mradi huo utahusika na ukarabati wa miundombinu ya usambazaji umeme kwenye Mikoa ya Arusha na Dar es Salaam na kuwamba mradi wote utagharimu Dola milioni 40 za Kimarekani.
"Serikali na Tanesco zimekamilisha masharti yote ya mkopo huu wa AFDB, na mkataba uliosainiwa Machi 2008, baada ya pasaka watakuwa wameshapitia yote tuliyo ya peleka na mwishoni mwa mwezi huu mradi utaanza," alisema Ngeleja.
.