Nyerere Day: Baba wa Taifa na Wanawake - Mama Muni na Julius Nyerere 1954

Nyerere Day: Baba wa Taifa na Wanawake - Mama Muni na Julius Nyerere 1954

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
NYERERE DAY: NYERERE NA WANAWAKE - MAMA MUNI: BI ZAINAB SYKES

Mama Muni, Bi Zainab Sykes ni mmoja wa akina mama waliomfahamu Julius Nyerere siku za mwanzo alipofika Dar es Salaam 1952.

Mama Sykes amenihadithia visa viwili muhimu sana katika historia ya Julius Nyerere na harakati za kudai uhuru.

Kisa cha kwanza ni siku nyumba yake pale Mtaa wa Kipata ilipovamiwa na askari wa Special Branch wakitafuta mashine iliyokuwa ikitumika katika kudurufu makaratasi ya ‘’uchochezi,’’ ambayo makachero wa Special Branch walikuwa na taarifa kuwa kazi ile akifanya Ally Sykes na hiyo mashine iko nyumbani kwake Mtaa wa Kipata.

Mama Muni akiwa ndani mlango ulibishwa hodi na alipokwenda kuchugulia nje (kwani milango yote ilikuwa ikifungwa wakati Ally Sykes akichapa yale makaratasi), Mama Muni akamuona Amri Kweyamba kachero wa Special Branch amesimama na askari anasubiri kufunguliwa mlango.

Haraka alirudi ndani kumpa taarifa mumewe kuwa kuna askari nje.

Ilimchukua Bwana Ally muda mfupi sana kukusanya yale makaratasi na wino kutumbukiza chooni uani na mashine kurushwa ua kwa ua na ikapotelea kusikojulikana.

Alipofunguliwa mlango Amri Kweyamba hakukuta kitu ndani ila Ally Sykes na mkewe wanamtazama.

Kisa cha pili alichonihadithia ni siku Nyerere alipokwenda nyumbani kwake Bi. Zainab Sykes Kipata Street (Sasa Kleist Sykes Street )kutoa taarifa ya kuisajili TANU.

Hii ilikuwa baada ya TANU kuasisiwa katika mkutano wa mwaka wa TAA tarehe 7 Julai 1954.

Hii ndiyo siku ilipoundwa TANU.

Abdul na Ally Sykes na Julius Nyerere walikuwa wamekubaliana kuwa Nyerere akitoka kwa Msajili kuisajili TANU wakutane nyumbani kwa Mama Muni hapo Mtaa wa Kipata.

Bi. Zainab anasema Nyerere alipofika alikuwa kalowa sana akaeleza kuwa Msajili amekataa kuisajili TANU kwa kuwa haina kitabu cha rejesta kinachoonyesha majina ya wanachama.

Abdul Sykes palepale aliagiza Mzee Said Chamwenyewe atafutwe ili ampe maelekezo ya kwenda Rufiji ampe rejesta na kadi za TANU kutafuta wanachama wa mwanzo wa TANU.

Katika orodha ya mama zangu niliowadiriki hadi Bi Zainab Sykes naamini alikuwa mmoja katika kundi la mwisho la huu uzawa wa akina mama walioshuhudia harakati za uhuru na kumjua Nyerere vyema kabisa.

Waliobakia wengine kwa wakati ule kwa ufahamu wangu walikuwa akina mama wanne – Mama Ali aliyekuwa mke wa Aziz Ali wa Mtoni baba yake Dossa Aziz, Bi. Maunda Plantan, Bi. Flora Mgone na Mama Maria Nyerere.

Akina mama hawa wameona kila kitu katika historia ya uhuru kwa macho yao.

Laiti akina mama mama hawa wangelinyanyua kalamu na kuandika yale waliyoshuhudia miaka ya 1950 wakati baba zetu hapa Dar es Salaam wanaanza harakati za TANU kudai uhuru wangetuachia hazina kubwa ya historia ya kupigania uhuru wa Tanganyika isiyo na kifani.

Hata hivyo mama zetu hawa wamezungumza kwa kiasi chao na tumeyajua mengi kutoka kwenye vinywa vyao.

Mama Sykes ndiye aliyehifadhi nyaraka za familia ambazo mimi nashukuru kuwa nyingi nimezisoma wakati natafiti kitabu cha maisha ya Abdul Sykes.

Nyaraka hizi naamini ndiyo nyaraka pekee zilizobakia mikononi mwa watu binafsi zinazoeleza historia ya kudai uhuru wa nchi yetu na kwa njia ya pekee nyaraka hizi zinaeleza pia historia ya Julius Nyerere na uhusiano wake na ukoo huu katika kupigania uhuru wa Tanganyika.

Itapendeza sana sasa kwa familia hii kufikiria kwa heshima ya mama yetu huyu angalau kuwa na maktaba ndogo itakayohifadhi kumbukumbu hii na ile hazina kubwa ya picha iliyopo inayofungamana na historia ya Tanganyika na historia ya Julius Nyerere.

1728153245567.png

Bi. Zainab Sykes​
 
Back
Top Bottom