Wanamajlis,
Baada ya kumsikiliza Baba wa Taifa itapendeza kusoma nini viongozi wenzake na wao
wamesema kuhusu udini katika nchi yetu;
Prof. Kighoma Malima na
Aboud Jumbe walionya kuhusu udini katika serikali ya Tanzania:
Hebu someni hapo chini:
''Tarehe 5 Novemba, 1985 kabla hajastaafu urais, Nyerere aliwahutubia wazee wa Dar es Salaam. Hotuba hii ilijaa simanzi, Nyerere akikumbuka jinsi Waislam walivyompokea Dar es Salaam kwa mapenzi makubwa ingawa yeye alikuwa Mkristo. Wazee hawa wengi wao walikuwa wanachama wa zamani wa TANU waliomuunga mkono Nyerere wakati wa kudai uhuru. Nyerere aliusifia mchango wa Waislam katika kipindi kile kigumu cha kudai uhuru. Nyerere alisema kuwa upogo katika elimu uliorithiwa na serikali yake kutoka kwa Waingereza baina ya Waislam na Wakristo yeye ameuondosha katika kipindi cha utawala wake:
''Waislam wametupa nafasi kupitia sera yetu ya elimu, kurekebisha upogo. Sasa nipo katika hali ya kufarahisha kwa kuwa wakati mwingine sielewi kama Mbunge mpya, Waziri, au Katibu Mkuu katika wizara zetu za serikali, ni Muislam au Mkristo au hana dini labda pale jina lake la kwanza linapotoa utambulisho. Na hata hivyo hiyo siyo njia ya kuaminika kutoa utambulisho wa dini kwa kuwa tuna Wakristo wenye majina ya Kiislam, na Waislam wenye majina ya Kikristo. Kuvumiliana huku nyie ndiyo sababu; nilichofanya mimi ni kuzungumzia maadili haya kwa niaba yenu.''
[79]
Hotuba hii ilikuwa ya ulaghai. Ukweli ni kuwa miongo mitatu baada ya uhuru Waislam hawajanufaika chochote wako katika hali ile ile aliyowaacha wakoloni au mbaya zaidi. Sivalon amefichua kuwa Kanisa limeweza kujenga himaya yake ambayo inahodhi asilimia sabini na tano za viti katika Bunge la Tanzania. Kati ya viti hivyo asilimia sabini vipo mikononi mwa Wakatoliki na vilivyobaki vimegawika kati ya Waislam na Wakristo wa madhehebu nyingine.
[80] Baada ya kupatikana uhuru, Kanisa lilipohisi wasiwasi, limeweza kwa urahisi kabisa kuwazuia na kuwadhibiti Waislam. Serikali imeweza kutumia nguvu iliyokuwanayo katika kudhibiti siasa kuzuia harakati za Waislam kudai fursa sawa na Wakristo katika kugawana madaraka katika serikali. Kanisa limehakikisha kuwa kupinduliwa kwa ukoloni si kizingiti kwa Ukristo, ingawa ingetegemewa kuwa Kanisa lingedhirika kwa kuanguka kwa ukoloni. Katika miaka yake zaidi ya mia moja, Kanisa lilikuwa limestarehe kama muokozi wa nafsi na watu wenyewe. Kanisa lilikuwa salama na halikupambana na msukosuko wowote kutoka kwa serikali kwa kuwa lilikuwa Kanisa ndilo lilishika hatamu ya serikali.
Baada ya kueleza hayo yote ni muhimu sasa kuangalia jinsi ukereketwa wa Kikristo unavyofanya kazi katika serikali na jinsi kazi hiyo inavyoathiri Uislam. Wizara ya Elimu inachukuliwa kama mfano kwa sababu ya umuhimu wake katika jamii. Katika wizara hii, inaweza kuonekana kwa uwazi kabisa jinsi Ukristo unavyofanya kazi na jinsi udini ulivyoshamiri katika kugawa nafasi muhimu kati ya Waislam na Wakristo. Ilikuwa katika wizara hii katika historia ya Tanzania ndipo kwa mara ya kwanza waziri Muislam alipochaguliwa kuongoza wizara, Kanisa likaingilia kati waziwazi kumpiga waziri vita na kuhoji nafasi nyingine za juu ambazo zilipewa Waislam. Serikali haikuweza kupingana na Kanisa na waziri huyo, marehemu Profesa Kighoma Ali Malima aliondoshwa katika wizara hiyo.
Mwaka 1987 Profesa Malima aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu akiwa Muislam wa kwanza kushika nafasi hiyo. Mawaziri wanane waliopita walikuwa Wakristo. Kulikuwa na malalamiko kutoka kwa Waislam kuwa wizara hiyo imegeuzwa jimbo la Wakristo, hasa pale padri alipoteuliwa na Julius Nyerere kuongoza wizara hiyo. Profesa Malima aliposhika wizara hiyo aliona upo umuhimu wa kufanya marekebisho kadhaa ili kurejesha imani ya Waislam katika wizara hiyo. Kulikuwa na tuhuma kuwa Wizara ya Elimu ilikuwa ikiwabagua vijana wa Kiislam kupata nafasi katika vyuo vya elimu ya juu na ilikuwa ikizuia kupanda vyeo kwa Waislam.
Profesa Malima alipoona dhulma ile iliyokuwapo katika wizara ile dhidi ya Waislam, Profesa Malima aliwateua Waislam wanne kushika nafasi katika kurugenzi mbalimbali na akaandika taarifa ya siri kwa Rais Ali Hassan Mwinyi
[81]kumtaarifu udini
[82] alioukuta katika wizara ile. Katika taarifa ile kwa rais,
[83] Profesa Malima alieleza kuhusu kudumazwa kwa Waislam katika mgao wa elimu. Taarifa hii ilivuja kwa vyombo vya habari
[84] na kwa Wakristo wengine. Katika watu walioipata taarifa hii ni Rais Mstaafu Julius Nyerere wakati ule akiwa Mwenyekiti wa chama tawala CCM.
Kuwekwa kando kwa Waislam kupo wazi kiasi ya kuwa mtafiti haihitaji hata kufanya utafiti wa kina unaopewa nguvu na takwimu. Mtafiti yeyote wa sayansi ya jamii hatoweza kushindwa kuona ukweli huu kwa macho tu. Hali hii inaonekana katika kila nyanja ya maisha. Utafiti wa kwanza katika tatizo hili la Waislam kudhulumiwa katika ugawaji wa madaraka ulifanywa na vijana wa Kiislam katika jumuiya yao iliyokuwa ikijulikana kama Warsha ya Waandishi wa Kiislam, kwa ufupi ikijulikana kama Warsha.
Kanisa kwa mara ya pili tokea mwaka 1963 ilipata wasiwasi kuhusu mabadiliko ambayo yalikuwa yanafanyika katika Wizara ya Elimu. Lakini katika miaka ya 1980, hali ya mambo yalikuwa yamebadilika sana. Waislam walikuwa wamejizatiti nje ya mfumo wa siasa kiasi ya kuwa hapakuweza kupatika kibaraka katika Waislam ambae angekuwa tayari kutumika kulihami Kanisa. Hali ya uhasama wa wazi kati ya Waislam na serikali ilikuwa imejitokeza wazi kabisa. Hata hivyo mawakala wa kanisa katika serikali walimshutumu Profesa Malima kwa kuwa Muislam mwenye ‘siasa kali’. Profesa Malima akatakiwa ahojiwe mbele ya Kamati Kuu ya CCM kwa kuingiza hisia za kidini ambazo zimesababisha uadui baina ya waumini wa dini hizi mbili. Suala hili likajadiliwa Dodoma chini ya uenyekiti wa Julius Nyerere. Lakini badala ya kujadili suala la dhulma kwa Waislam na kulitafutia ufumbuzi, yule anaedhulumiwa ndiye aliyewekwa kizimbani badala ya dhalim anaedhulumu; msukumo wa mjadala ukawa katika uteuzi wa wakurugenzi wanne Waislam aliofanya Profesa Malima katika Wizara ya Elimu. Profesa Malima alionekana amekiuka mwenendo na taratibu zulizodumu katika wizara ile kwa kipindi kirefu ya kuwa ni Wakristo pekee wenye haki ya kushika nafasi za juu katika wizara za serikali. Kwa ajili hii profesa Malima akavuliwa madaraka kama Waziri wa Elimu. Rais Mwinyi alikuwa hana uwezo wa kuhimili nguvu ya Kanisa. Nchi inayodai kuwa ni ya kisekula ilikuwa imeshindwa kwa mara nyingine kuwapa Waislam haki yao waliyohakikishiwa na katiba ya Tanzania.
Kwa nchi ambayo inajigamba kuwa inajali usawa kwa wananchi wake inashangaza kuona kuwa Waislam wanabaki nyuma na juhudi zozote ambazo Waislam watafanya ili kuondoa upogo kati yao na Wakristo na kujiletea maendeleo zinapata upinzani na uadui kutoka na mfumo ule ule unajidai kuwa unasimamisha usawa na haki. Kitu cha kusikitisha ni kuwa hakusimama hata Muislam mmoja katika wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM kumuunga mkono Profesa Malima kwa dhulma ambayo wote walikuwa wanafahamu kuwa imedumu kwa kipindi kirefu. Hata ndani ya Bunge hakuna Muislam aliyekuwa na ujasiri wa kumtetea Profesa Malima.
[85] Muislam mmoja, Mwenyekiti wa Mkoa wa Pwani, Masudi Mtandika, aliungana na kambi ya Wakristo katka Kamati Kuu ya CCM kumshambulia Profesa Malima. Msimamo wa Mtandika ulikuwa sawa na ule wa Rajab Diwani na Selemani Kitundu walipomshambulia Bibi Titi Mohamed wakati Kamati Kuu ya TANU ilipokuwa ikijadili EAMWS mwaka wa 1963. Kampeni ya chuki na propaganda dhidi ya Profesa Malima ikaanzishwa na vyombo vya habari ambavyo vyote vilikuwa chini ya miliki ya Wakristo na hivyo chini ya Kanisa.
Aboud Jumbe,
[86] rais wa zamani wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Tanzania, amefanya utafiti kuhusu nafasi ambazo wameshika Waislam katika serikali, Bunge na vyuo vya elimu ya juu. Takwimu alizoonyesha Aboud Jumbe zinatisha. Katika baadhi ya taasisi Waislam wanaonekana kwa kutokuwepo katika taasisi hizo. Utafiti wa Jumbe ulikuwa wa pili katika kueleza tatizo hili la Waislam na kuliweka wazi kwa matumaini ya kuwa labda serikali ingeweza kuhisi kuwajibika na kujaribu kusahihisha makosa hayo.
Majaribio mengine yamewahi kufanyika huko nyuma na watu kama Sheikh Abubakar Mwilima, wakati huo akiwa Mwenyekiti wa JUWATA na katika Kamati Kuu ya chama tawala CCM, alijaribu kuieleza serikali tatizo hili la Waislam. Kitu kimoja mashuhuri kwa wote waliojaribu kuliweka tatizo hili mbele ya serikali wote hao walimalizwa kisiasa. Maisha yao katika siasa yalikatizwa – Chifu Abdallah Said Fundikira, Tewa Said Tewa, Bibi Titi Mohamed, Mufti Sheikh Hassan bin Amir, Mussa Kwikima, Sheikh Abubakr Mwilima, Profesa Kighoma Malima na wengine wengi. Ilikuwa kuanzia hapa ndipo Waislam walianza kunong’ona kuhusu njama dhidi yao. Kuwepo kwa njama dhidi ya Waislam kulikuja kudhihirishwa pale watafiti wa Kikristo walipoanza kufanya utafiti kuhusu athari za Ukristo katika utawala wa dola; na bila kujali matokeo ya utafiti kwa hisia za Waislam wakawa wanaeleza jinsi Waislam kwa hila na msaada wa serikali walivyowekwa pembeni katika kugawana madaraka na Wakristo.''
Kutoka, ''Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes...''
[79] Daily News, 6th November 1985.
[80] Sivalon, op.cit. uk.49.
[81] Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Jamuhuri ya Tanzania mwaka 1985-1995.
[82] Warsha ndiyo jumuiya ya kwanza katika historia ya Tanzania baada ya uhuru kuanza kuwaanda Waislam na kupambana na dhulma zilizokuwa zikifanyiwa Waislam. Kwa kipindi chote cha uhai wake serikali ilikataa kukipa usajili. Hii ilikuwa heri kwao kwa kuwa kiliendesha kampeni zake chini kwa chini, kampeni ambazo zilileta mafanikio makubwa hasa katika kuwaelimisha Waislam kuhusu mbinu za adui. Warsha iliweza kufikia hatua ikachukua uongozi wa BAKWATA. Warsha haikudumu katika uongozi kwa muda mrefu. Serikali ikimtumia Adam Nasibu kwa mara ya pili iliweza kuwapiga marufuku vijana hawa wasishugulike na uongozi wowote katika jumuiya yoyote ya Kiislam. Hata hivyo athaari za Warsha zingalipo hadi sasa. Vongozi wengi wa jumuiya za Kiislam hivi sasa wamepata uamsho na mafunzo yao ya awali ya uongozi katika Warsha. Mwaka wa 1981 Warsha walifanya utafiti ambao ulikuwa haujawahi kufanyika kabla, Warsha walifanya utafiti katika elimu ya Waislam Tanzania. Utafiti ulionyesha Waislam walikuwa wana nafasi chache katika vyuo vya elimu ya juu. Taarifa ya utafiti huu ilisambazwa kwa Waislam wote wa Tanzania.
[83] Angalia
Kiongozi, Julai 15-31, 1993.
[84] Hali ya Waislam katika Tanzania ni ya kusikitisha inapokuja suala la kueneza habari au propaganda. Vyombo vyote vya habari, vya serikali na vilivyo chini ya wamiliki binafsi vyote vipo katika mikono ya Wakristo. Vyombo hivi vinatumika vyema katika kupiga vita Waislam.
[85] Nje ya vyombo hivyo vya serikali, Profesa Malima alikuwa na jeshi kubwa ka Waislam waliokuwa nyuma yake, wengi wao wakiwa vijana. Wakiwa hawana vyombo vya habari wanavyovimiliki, Waislam walichapa makaratasi na kuyatawanya nchi nzima yakimuunga mkono Profesa Malima huku yakieleza udhalimu wa serikali, mengine yamkitaja Julius Nyerere na Kanisa Katoliki kama washiriki katika kuwadhulumu Waislam. Kwa ajili hii Profesa Malima alipendeza machoni mwa Waislam. Profesa Malima akawa anaalikwa katika kila hafla muhimu ya Waislam. Katika hafla zile Profesa Malima aliwahutubia Waislam kuhusu madhila wanayoyapata.
[86] Aboud Jumbe,
The Partner-Ship, Amana Publishers, Dar es Salaam, 1995, uk. 125-138.