Kuna Imani kuwa nyoka huuma na kuacha meno yake kwa muhanga wake. ...ifahamike meno ndo silaha kuu ya nyoka,katika kujitafutia chakula na kujilindA...Asilimia kubwa ya watanzania wanaamini hivyo kuwa nyoka akikuuma anakuachia meno ambapo inakubidi uyatoe haraka kabla madhara hayajawa makubwa.... jamiichek hili Lina ukweli au ni uwongo wa kiwango Cha lami?
- Tunachokijua
- Nyoka ni moja kati ya viumbe jamii ya reptilia wasio na miguu ambaye uwezo wake wa kutoka sehemu moja kwenda nyingine ni kwa kutambaa. Kwa mujibu wa National Geographical World Kuna zaidi ya aina 3,000 za nyoka duniani na wanapatikana kila mahali isipokuwa Antarctica, Iceland, Ireland, Greenland, na New Zealand. Takribani aina 600 wana sumu, na ni takribani aina 200 tu asilimia saba wanaoweza kuua au kumjeruhi binadamu kwa kiwango kikubwa.
Nyoka hutumia ndimi zilizogawanyika hatikati, ambazo huzitikisa kuelekea pande mbalimbali ili kunusa hali ya mazingira yao. Hii huwasaidia kujua hatari au chakula kiko karibu.
Kung'atwa na nyoka kunaweza kusababisha michubuko au alama ndogo za meno kwenye eneo lililong'atwa. Sehemu za kawaida za kung'atwa na nyoka ni mikononi na kwenye mikono, au kwenye vifundo vya miguu na miguu. Hili linaweza kutokea mtu anapong'atwa na nyoka akiwa anatembea. Pia linaweza kutokea mtu anapojaribu kumshika au kumkamata nyoka.
Kumekuwapo na madai kuwa nyoka anapong’ata huacha meno yake kwa mtu aliyeng’atwa na hawezi kung’ata tena.
Je uhalisia wa madai hayo ni upi?
Ufuatiliaji uliofanywa na JamiiCheck umebaini kuwa madai ya nyoka kung’ata na kuacha meno hadi kusababisha kushindwa kung’ata tena si ya kweli
Mkufunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka, Tito Lanoy anasema Kuhusu hoja kuwa Nyoka anang’ata mara moja tu kisha meno yake yanabaki sehemu husika na hawezi kung’ata tena, dhana hiyo sio ya kweli.
Aidha Tito anaendelea kwa kutoa ufafanuzi wa meno ya Jamii ya Nyoka kama ifuatavyo
Nyoka ambao hawana sumu
Meno ya nyoka hayafanani, Jamii ya Nyoka ambayo haina sumu meno yao yanakuwa ni mengi madogomadogo yanayolingana.Nyoka wa aina hiyo Waking’ata sehemu ya meno yao huwa yana tabia ya kukatika kutokana na udogo wake. Hawa hawana madhara makubwa zaidi utakuta amekuachia alama tu kama atakung’ata.
Nyoka wenye sumu
Jamii ya Nyoka hawa nao pia wametofautiana, meno mawili ndio yanakuwa yamebeba sumu, mengine yanakuwa yanasaidia wakati wa kumeza chakula. Nyoka wenye meno mawili, nao kuna nyoka wenye meno marefu ambao wakikung’ata unaweza kukuta matundu mawili ya sehemu alipong’ata. Nyoka wa aina hiyo akimng’ata mtu akashtuka kabla ya nyoka kutoa jino, meno yanaweza kukatika.
Nyoka wenye meno mafupi
Nyoka wenye meno mafupi mbele kama vile Koboko na Cobra, meno hayo yanatumika kupitisha sumu, hao sio rahisi kukata meno wakati wa kung’ata kama ilivyokuwa wale wenye meno marefu. Hawa ni aina ya nyoka ambao wanaweza kung’ata zaidi ya mara moja na ndio nyoka wenye sumu kali.
Nyoka wenye meno yaliyojificha
Jamii nyingine ya nyoka, hawa ni wale ambao wana meno ambayo yamekaa sehemu ya mwisho mdomoni kwa binadamu tunaweza kusema ni magego. Pamoja na kukaa mwisho, yameelekea ndani kwenye koromeo, hao sio rahisi kung’ata binadamu, ili afanye hivyo anatakiwa kuzuia anachotaka kuking’ata kwa meno ya mbele kisha ndio ang’ate kwa meno yake ya ndani.
Nyoka hawa sumu yao ni kali, kwani wakikung’ata hata matibabu yake ni gharama kwa kuwa dawa yao haitengenezwi sana kwa sababu ni ngumu kung’ata binadamu.