Nyota wa5 wanaomkubali Ronaldo dhidi ya Messi

BAK

JF-Expert Member
Joined
Feb 11, 2007
Posts
124,790
Reaction score
288,165
14Sep 2020
Na Mwandishi Wetu

Dar es Salaam

Makala
Nipashe


Nyota wa5 wanaomkubali Ronaldo dhidi ya Messi
MWEKAJI rekodi wa timu ya Taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo alilipamba jina lake kwenye vitabu vya historia baada ya kufunga bao lake la 100 na 101 kwenye mechi za kimataifa, Jumanne iliyopita.

Ronaldo kwa sasa akiwa anacheza kule Juventus bila shaka yoyote ni mmoja wa wachezaji bora zaidi kuwahi kushuhudiwa kwenye mchezo wa soka duniani.

Jumanne usiku, Ronaldo aliweka historia hiyo kwa mara nyingine tena kwa rekodi ambayo inaweza kukaa kwa miaka mingi. Mchezaji huyo wa zamani wa Real Madrid alifunga bao la 100 na 101 kwa timu ya Taifa ya Ureno wakati ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Sweden kwenye Ligi ya Mataifa ya UEFA.

Na hilo likamfanya kuwa mchezaji wa kwanza barani Ulaya kufikisha idadi hiyo ya mabao kwa timu yake ya taifa. Ronaldo alihitaji mechi 165 tu kufikisha rekodi hiyo.

Amepitwa mabao nane tu ili kufikia rekodi ya kufunga mabao mengi ya kimataifa, ambapo kwa sasa rekodi hiyo inashikiliwa na mchezaji wa zamani wa Iran, Ali Daei, ambaye ana mabao 109 aliyoifungia nchi yake.

Rekodi hiyo ni moja kati ya rekodi nyingi alizoziweka Ronaldo, ambaye ni mmoja wa wachezaji bora wa kizazi hiki pamoja na nahodha wa Barcelona, Lionel Messi.

Wawili hao kwa pamoja wameshinda mara 11 tuzo ya Ballon d'Or tangu waanze kucheza soka. Wanasoka wengi mara kwa mara wamekuwa wakiulizwa kuhusu nani ni bora zaidi kati ya wawili hao. Makala haya yanakuchambulia wanasoka nyota watano ambao wamemchagua Ronaldo kuwa bora zaidi ya Messi, twende sasa...

5. Gini Wijnaldum | Liverpool
Kiwango cha Gini Wijnaldum kimeimarika kwa kipindi cha miaka michache ya hivi karibuni. Raia huyo wa Uholanzi amekuwa kwenye nafasi nzuri katika safu ya kiungo mshambuliaji chini ya kocha, Jurgen Klopp. Wijnaldum ambaye alikuwa nguzo muhimu kwa 'Wekundu' hao alifunga mabao mawili wakati Liverpool ikiitoa Barcelona hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 29, aliulizwa kumchagua kati ya Messi na Ronaldo katika matukio kadhaa. Katika tukio la kwanza alijibu kidiplomasia kwa kusema; "Muda mwingine nasema Lionel Messi, wakati mwingine nasema Cristiano Ronaldo. Si haki kuchagua mmoja kati yao, kwa sababu alichonacho mchezaji mmoja, mwingine hana. Kwa upande wangu wote ni wachezaji bora duniani."
Hata hivyo, katika mahojiano ya 'lazima ujibu', Wijnaldum aliulizwa kuchagua mmoja kati ya Messi na Ronaldo. Na raia huyo wa Uholanzi alimchagua Ronaldo. Hivi sasa Wijnaldum amekuwa akihusishwa sana kuhamia kule Barcelona usajili ambao unatajwa unaweza kufanyika katika wiki chache zijazo.

4 Michael Owen | Nyota wa zamani Liverpool, Manchester United, Real Madrid

Mchezaji mwingine kwenye orodha hii ni gwiji wa zamani wa mabingwa wa Ligi Kuu ya England, Liverpool, Michael Owen ambaye amemchagua Ronaldo juu ya Messi. Owen mwenye umri wa miaka 40, kwa sasa alikuwa mchezaji wa mwisho wa Uingereza kushinda Ballon d'Or, tuzo ambayo Ronaldo ameitwaa mara tano hadi sasa.

Owen alielezea kwa nini amemchagua Ronaldo juu ya Messi. Muingereza huyo alisema;
“Kufunga mabao ni kazi ngumu kwenye soka na (Ronaldo) ameifanya kuwa rahisi. Anafunga kwa kichwa, mguu wa kushoto au kwa mguu wa kulia. Messi ni mchezaji mzuri sana, lakini ukiangalia kwa takwimu ya wawili hao Messi na Ronaldo, unatakiwa kumchagua Ronaldo kwa sababu ana vitu vingi tofauti."

Akaendelea kusema, "Pengine Ronaldo ndio mchezaji mwenye kasi zaidi akitumia mguu wa kulia na kushoto pamoja na kichwa. Nafikiri Messi amezidiwa na Ronaldo kwa mbinu."

3. Ruud van Nistelrooy | Nyota wa zamani Manchester United, Real Madrid
Katika orodha hii, Ruud van Nistelrooy ndiye mchezaji pekee aliyecheza na Cristiano Ronaldo katika timu moja. Gwiji huyo wa Uholanzi anabaki kama mmoja wa mshambuliaji bora zaidi wa kati kwa Manchester United, akiwa amefunga mabao 150 katika mechi 219 alizowachezea 'Mashetani Wekundu' hao.

Van Nistelrooy na Ronaldo walikuwa haziivi wakati wakicheza pamoja pale Old Trafford. Hata hivyo, licha ya tofauti zao hizo uwanjani, Van Nistelrooy alimchagua Ronaldo kuwa bora zaidi ya Messi.

Mchezaji huyo wa zamani wa Real Madrid, aliyecheza kwa misimu mitatu akiwa na Ronaldo pale Old Trafford, Van Nistelrooy, amesema:
"Hakuwa mjinga. Mara zote alikuwa tayari kupokea ushauri. Alikuwa mtu mzuri kwenye vyumba vya kubadilishia nguo."

2 Kylian Mbappe | Paris Saint-Germain

Huyu ni mmoja wa mashabiki wakubwa kwa Ronaldo, kwani wakati akikua Kylian Mbappe alikuwa akipenda zaidi kumwangalia nyota huyo wa Ureno. Nyota huyo wa Ufaransa anatajwa kwamba ndiye atakuwa mchezaji bora zaidi duniani baada ya kumalizika kwa zama za Messi na Ronaldo. Akizungumza kuhusu nani bora ambaye atamchagua kati ya Messi na Ronaldo, Mbappe alibainisha;

"Kutoka mwaka mmoja hadi mwingine, chaguo langu linabadilika kati ya Cristiano Ronaldo na Lionel Messi, ingawa naweza kukubali kwamba nimemchagua zaidi Ronaldo. Nilimpenda wakati nikiwa mdogo."

Mbappe amezungumza kuvutiwa na nyota huyo wa Juventus katika matukio kadhaa. Mfaransa huyo amebainisha kwamba wachezaji ambao walikuwa wanamvutia wakati akikua ni Zinedine Zidane na Cristiano Ronaldo.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 21, ambaye alichomoza Ulaya akitokea kule AS Monaco, alibainisha kwamba chumbani kwake aliweka picha nyingi sana za Ronaldo kwenye ukuta.

Mshindi huyo wa Kombe la Dunia anachukuliwa kama mmoja wa wachezaji wanaowaniwa sana na Real Madrid. Kama atahamia kwa miamba hao wa Hispania atakuwa amefuata nyao za Ronaldo na Zidane.

1. Pele | Nyota wa zamani Santos

Pele anatajwa kama ndio mchezaji bora wa wakati wote na mara zote amekuwa wazi kumchagua Ronaldo kama mchezaji bora na amekuwa akimfananisha na yeye wakati akicheza.

Ingawa gwiji huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Brazil anatambua ubora wa Messi, lakini Pele anaamini Ronaldo ndiye mchezaji bora zaidi duniani kwa sasa. Nyota huyo wa zamani wa Santos amesema kutoshuka kwa kiwango cha Ronaldo ndio kunamfanya kuwa bora zaidi ya Messi.

Akizungumza na chaneli ya YouTube kupitia Daily Mail kuhusu nyota hao wawili, Machi mwaka huu, Pele mwenye umri wa miaka 79, alieleza:

"Leo hii mchezaji bora duniani ni Cristiano Ronaldo. Nafikiri yeye ni bora kwa sababu ya kutoshuka kiwango chake, lakini huwezi kumsahau (Lionel) Messi, lakini yeye si straika."

Pele ana rekodi ya kubeba Kombe la Dunia mara tatu na ni mmoja wa wachezaji waliofunga mabao mengi zaidi kipindi akiwa mchezaji.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…