BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,165
Serikali yazirejesha nyumba 120 zilizouzwa
2009-02-12 10:35:12
Na Boniface Luhanga, Dodoma
2009-02-12 10:35:12
Na Boniface Luhanga, Dodoma
Serikali imefuta miliki ya nyumba zake zaidi ya 120 ambazo waliuziwa watumishi wake, taasisi na watu binafsi.
Kufuatia hatua hiyo, serikali sasa italazimika kuwalipa watu hao mamilioni ya fedha kama fidia kutokana na wamiliki hao wapya kuziendeleza huku wengine wakijengewa nyumba nyingine.
Hayo yalitangazwa jana bungeni na Waziri wa Miundombinu, Dk. Shukuru Kawambwa alipokuwa akiwasilisha taarifa ya serikali kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge juu ya uuzwaji wa nyumba za serikali.
Pamoja na mambo mengine, Bunge liliazimia na kuiagiza serikali kuzirejesha kwenye miliki yake nyumba zote zilizouzwa kinyume cha utaratibu.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa azimio hilo, Dk. Kawambwa alisema serikali imekamilisha tathmini ya maendeleo yaliyofanywa katika nyumba zote na sasa mikataba imefutwa.
Alifafanua kuwa, kwa nyumba zilizoko kwenye makambi kwa wanaoishi humo hadi sasa ni watumishi wa umma wenye stahili ya kupewa nyumba na serikali, wameandikiwa barua kuwajulisha kuendelea kuishi humo kama wapangaji kwa mujibu wa stahili zao za kiutumishi.
Alisema pamoja na hayo, bado hatua za kuwarejeshea fedha zao zinaendelea.
Waziri Kawambwa alizitaja nyumba hizo ambazo zimerejeshwa kwenye miliki ya serikali na wamiliki wake watalipwa fidia zao kuwa ni 53 zilizopo kwenye makambi ambazo hazikupaswa kuuzwa, nyumba 27 za taasisi mbalimbali zilizouzwa kwa watumishi wa serikali na nyumba 35 zilizouzwa ambazo zipo kwenye maeneo nyeti ya serikali.
Pia alizitaja nyumba nyingine kuwa ni nyumba nne zilizouzwa kwa watu ambao si watumishi wa serikali na familia sita na watumishi wanne waliouziwa nyumba zaidi ya moja.
Hata hivyo, alisema waliouziwa nyumba hizo, watalipwa fidia kutokana na kwamba walikuwa tayari wameziendeleza huku baadhi yao wakijengewa nyumba nyingine.
Watu hao watalipwa fidia ya kati ya Sh. milioni 13 na Sh. milioni 223 kutegemeana na mhusika alivyokuwa ameifanyia ukarabati nyumba husika.
Kuhusu utekelezaji wa maazimio juu ya mkataba wa Kampuni ya Kupakia na Kupakia Makontena (TICTS), Waziri Kawambwa alisema hatima ya kampuni hiyo sasa iko mikononi mwa Baraza la Mawaziri.
Alisema wizara yake imeandaa Waraka kwa Baraza la Mawaziri ili kupata maamuzi ya juu ya serikali kuhusu suala hilo.
Aidha, kuhusu suala la Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Dk. Kawambwa alisema serikali kwa sasa inapitia ripoti ya kikundi-kazi na kuona namna ya kuyafanyia kazi mapendekezo ya ripoti hiyo kwa lengo la kuimarisha shirika hilo.
Kuhusu suala la Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) alisema serikali imeunda kamati ya majadiliano ya kurekebisha mikataba ya ukodishaji na wanahisa.
Alisema kamati ya serikali imewasilisha mapendekezo mbalimbali ya kurejea vipengele mbalimbali katika mkataba wa ukodishaji.
SOURCE: Nipashe