Ongezeko La Mifuko Ya Pamoja Ya Uwekezaji Na Manufaa Yake Kwetu Wawekezaji

Ongezeko La Mifuko Ya Pamoja Ya Uwekezaji Na Manufaa Yake Kwetu Wawekezaji

Makirita Amani

JF-Expert Member
Joined
Jun 6, 2012
Posts
1,915
Reaction score
3,422
Habari njema Matajiri Wawekezaji,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya NGUVU YA BUKU, ambapo tunajifunza na kufanya uwekezaji kwa hatua ndogo ndogo na kujenga utajiri kwa uhakika.

Kauli mbiu yetu kwenye NGUVU YA BUKU, ambayo pia ndiyo imani yetu ni KILA MTU ANAWEZA KUWA TAJIRI. Hilo tuna uhakika nalo kwa sababu kwa fedha ndogo ndogo ambazo kila mtu anazipata, tukiziwekeza kwa muda mrefu kwa msimamo bila kuacha, tunaweza kujenga utajiri mkubwa.

Katika miaka ya hivi karibuni, mifuko ya pamoja ya uwekezaji (mutual funds) imepata umaarufu mkubwa nchini Tanzania. Ongezeko hili limekuja sambamba na ukuaji wa soko la mitaji na ongezeko la uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kuwekeza.

Mifuko ya pamoja ya uwekezaji inatoa fursa kwa wawekezaji wadogo na wa kati kuwekeza kwenye masoko ya fedha, na imekuwa njia mbadala inayorahisisha watu wengi kufikia ndoto zao za kifedha.

Mifuko ya pamoja ya uwekezaji ni mpango ambapo pesa za wawekezaji wengi hukusanywa pamoja na kuwekewa kwenye mali mbalimbali kama hisa, hati fungani, au mali nyinginezo za kifedha. Mifuko hii inaendeshwa na meneja wa mfuko ambaye ana jukumu la kufanya maamuzi ya uwekezaji kwa niaba ya wawekezaji wote. Kupitia mifuko hii, wawekezaji hupata faida ya uwekezaji wa kitaalamu bila ya kuwa na ujuzi maalumu wa masoko ya fedha.

INUKA-FUND.jpg

Kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU, tumechagua kuwekeza kwenye mifuko hii ya pamoja kwa sababu ya urahisi wake kuwekeza kwa kuweza kufanya hata kwa kiasi kidogo. Lakini pia ukuaji wake kwa muda mrefu ni mzuri.

Ongezeko la mifuko ya pamoja ya uwekezaji inamaanisha nini?

Kuwepo kwa ongezeko la mifuko ya pamoja ya uwekezaji ni kiashiria cha mambo mbalimbali yanayoendelea kwenye uwekezaji na uchumi kwa ujumla.


1. Ukuaji wa uchumi na fursa za uwekezaji.

Ongezeko la mifuko ya pamoja ya uwekezaji ni kiashiria kwamba uchumi unakua na fursa za uwekezaji zinaongezeka. Hilo ndiyo linazionyesha taasisi zinazoanzisha mifuko hiyo fursa ya kuingia kwenye soko na kuwapa wawekezaji faida nzuri kuliko ambayo wanaipata kwenye mifuko iliyopo.

2. Ushindani kwenye uwekezaji na faida zaidi kwa wawekezaji.

Kwa kipindi kirefu, sekta ya mifuko ya pamoja ya uwekezaji ilikuwa inatawaliwa na UTT AMIS na hilo liliwafanya kuendesha shughuli zao bila ya changamoto za ushindani. Uwepo wa mifuko mingi, inaleta ushindani mkali sokoni hivyo kila mfuko kuongeza ufanisi ili kuwashawishi zaidi wawekezaji kujiunga nao. Kadiri ufanisi unavyokuwa mkubwa, ndivyo faida kubwa inavyorudi kwa wawekezaji.

3. Fursa ya kutawanya uwekezaji ili kupunguza hatari.

Kanuni muhimu kwenye uwekezaji huwa ni kutawanya, usiweke mayai yako yote kwenye kikapu kimoja. Pamoja na mifuko ya pamoja ya uwekezaji kuwa inatawanya uwekezaji wake, bado kuwekeza kwenye mfuko mmoja tu ni hatari nyingine. Uwepo wa mifuko mingi inatoa fursa kwa wawekezaji kutawanya uwekezaji wao ili kupunguza hatari ya kupoteza.

Uwepo wa mifuko mingi ya uwekezaji wa pamoja ni kiashiria kizuri kwetu wawekezaji kuendelea kuwekeza kwa sababu ya ukuaji mzuri unaopatikana.

SOMA; Uwekezaji Na Usimamizi Sahihi Wa Utajiri Wako Kulingana Na Haiba Yako.

Jinsi ya kutumia ongezeko hili la mifuko ya pamoja ya uwekezaji.

Uwepo wa mifuko mingi ya uwekezaji unaleta fursa mbalimbali kwa wawekezaji, hivi ndivyo tunavyoweza kutumia fursa hiyo kwa manufaa kwetu.

1. Kuendelea kuwekeza kwenye mifuko tuliyoanza nayo.

Kwenye programu yetu ya NGUVU YA BUKU tumechagua kuwekeza kwenye mifuko ya pamoja iliyo chini ya UTT. Sababu kubwa ni ukongwe wake sokoni na malengo yetu ya muda mrefu ya uwekezaji. Uwepo wa mifuko hiyo kwa muda mrefu inatupa imani kwa safari yetu ya muda mrefu pia.

Hivyo kwenye programu yetu tutaendelea na mifuko ambayo tumeanza nayo.

2. Kutawanya uwekezaji baada ya kukuza mtaji.

Uwepo wa mifuko mingi ya pamoja ya uwekezaji kunatoa fursa ya kutawanya uwekezaji. Lakini kabla hujatawanya, lazima kwanza ukusanye. Hivyo hatupaswi kukimbilia kutawanya uwekezaji wetu kwa sababu tu fursa zipo. Badala yake tukusanye kwanza mitaji yetu kwa kuwekeza mahali pamoja na kikishafika kiasi fulani ndiyo tutawanye kwenda kwenye maeneo mengine.

Kwenye programu yetu tutaendelea na mifuko tuliyoanza nayo mpaka kufikia lengo la uhuru wa kifedha tuliloweka, kisha kuanza kutawanya uwekezaji ili kupunguza hatari.

Ongezeko la mifuko ya pamoja ya uwekezaji nchini Tanzania limekuwa ni mabadiliko muhimu katika tasnia ya uwekezaji. Inatoa fursa kwa watu wa rika zote, hata wale wasio na mtaji mkubwa, kuwekeza na kupata faida. Kwa kuwa na usimamizi bora, urahisi wa uwekezaji, na faida za kitaalamu, mifuko ya pamoja ya uwekezaji inazidi kuwa chaguo bora kwa wawekezaji wengi nchini. Ni dhahiri kwamba mifuko hii itakuwa na mchango mkubwa zaidi katika kukuza utamaduni wa uwekezaji na kufikia maendeleo ya kiuchumi kwa wawekezaji wa Tanzania.

Karibu kwenye SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2024 ambapo utakwenda kujifunza na kuweka mpango huu kwa vitendo kisha kusimamiwa kwenye kuutekeleza kwa msimamo bila kuacha. Tuma sasa ujumbe wenye maneno SEMINA 2024 kwenda namba 0752 977 175 upate nafasi ya kushiriki semina.

Kitabu kipya cha USIMAMIZI WA FEDHA BINAFSI kina nguzo saba muhimu kwa kila mtu kujijengea ili kuwa imara kifedha. Hiki ni kitabu muhimu kwa kila aliye makini na fedha zake kukisoma. Wasiliana sasa na namba 0752 977 175 kupata nakala yako ya kitabu.

SIKILIZA SOMO HILI KWENYE ONGEA NA KOCHA.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala mzuri wa somo hili ambapo washiriki wamekuwa na maswali na michango mbalimbali. Karibu usikilize hapo chini ili ujifunze na kuchukua hatua sahihi.


View: https://youtu.be/tBSewIM2ySk

MJADALA WA SOMO.

Karibu kwenye mjadala wa somo hili, shiriki kwa kutuma majibu ya maswali haya;

1. Ongezeko la mifuko ya pamoja ya uwekezaji inaashiria nini?

2. Tunatumiaje ongezeko la mifuko ya pamoja ya uwekezaji kwa manufaa?

3. Kwa nini kwenye NGUVU YA BUKU tumechagua kuendelea na mifuko ya UTT?

4. Upi mpango wako wa kutawanya uwekezaji kwenye mifuko mipya inayoongezeka sokoni?

5. Karibu kwa maswali, maoni, mapendekezo na shuhuda kuhusu somo hili na programu nzima ya NGUVU YA BUKU na UHURU WA KIFEDHA.

Tuma majibu ya maswali hayo kama uthibitisho wa kusoma, kuelewa na kutekeleza somo hili la uwekezaji.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.
 
Je security ya hiyo mifuko mingine isiyo ya kiserekali ikoje
 
Back
Top Bottom